Tuesday, July 19, 2011

JAMANI TUMSAIDIE MTOTO HUYU ANAYETAABIKA...


Mtoto huyu, Abdulaziz Abbas (2), alizaliwa akiwa hana sehemu ya kutolea haja kubwa. Anaishi vipi? Mama yake mzazi, Salma Sehho (26) anasimulia kuwa baada ya kujifungua Februari 26, 2009, hakujua kama mtoto wake hakuwa na sehemu ya kutolea haja kubwa.

Anasema hata Mkunga wa jadi aliyemsaidia kujifungua mtoto huyo, Ashura Seif naye hakujua tatizo hilo, hivyo alianza kumnyonyesha huku akiwa na furaha ya kupata mtoto huyo wa kiume. Salma anasema furaha yake iligeuka masikitiko kesho yake asubuhi baada ya mtoto kuanza kulia huku tumbo likiwa linaonekana kujaa. Wakati mtoto huyo akiendelea kulia kwa nguvu, Mkunga Ashura alimkagua kila sehemu ya mwili wa mtoto huyo ndipo alipogundua kuwa hana sehemu ya kutolea haja kubwa kabisa. "Kwa kweli nilichaganyikiwa baada ya kugundua kuwa mtoto wangu alikuwa hana sehemu ya kutolea haja kubwa kama ilivyo kwa watu wengine," anasema. Salma anasema baada ya kungudulika tatizo hilo, kwa msaada wa shemeji yake, Mzee Kapela, Februari 28 walimpeleka mtoto Hospitali ya Mission ya Dareda, iliyopo Wilaya ya Babati kupatiwa matibabu.

"Kwa hakika hatukuwa na matumiani kama mtoto huyo ataweza kupona kutokana na hali aliyokuwa nayo kwa wakati huo," anasimulia. Wakiwa katika hospitali hiyo, madaktari walipomchunguza waliamua kumpa huduma ya kwanza ambayo ni kumfanyia operesheni ya kutoboa utumbo sehemu ya tumbo lake ili aweze kujisiadia kwa muda. Baada ya kufanyiwa operesheni hiyo na kuwekewa sehemu ya muda ya kujisaidia mtoto alitulia, walilazwa katika hospitali hiyo kwa siku tatu. Hata hivyo, Salma anasema madaktari wa hospitali hiyo walimweleza kuwa mtoto huyo anatakiwa kupelekwa haraka Hospitali ya KCMC, iliyopo mjini Moshi kwa ajili ya kufanyiwa operesheni ili apatikane sehemu ya kutolea haja kubwa.

"Madaktari walituambia kwamba ingawa amepata huduma hii ya muda, ili aweze kuishi anatakiwa kufanyiwa operesheni haraka ya kutobolewa sehemu ya kujisaidia kwenye makalio," anasema. Walipoulizia gharama za operesheni hiyo katika hospitali KCMC kupitia baadhi ya madaktari wa hospitali hiyo ya Dareda waliambiwa ni Sh 800,000. Hata hivyo, ushauri huu wa madaktari wa hospitali ya Dareda ulikuwa ni sawa na pilipili kwenye kidonda, hawakuwa na uwezo wa kumpeleka katika hospitali hiyo.

Gharama za matibabu walizotumia katika hospitali hiyo kiasi cha sh 350,000 ambazo shemeji yake Mzee Kapela alikopa kutoka kwa majirani, ndio uwezo wao ulipoishia. Ingawa walihangaika kutafuta msaada wa fedha kutoka kwa watu mbalimbali, lakini walishindwa kupata kiasi hicho, wakaamua kumkabidhi mwenyezi Mungu mtoto huyo aweze kumlinda. Hatua hiyo ya kumwachia mungu amlinde mtoto wake ilichangiwa zaidi na mama huyo kuwa mzazi peke yake, kwani baba wa mtoto huyo, Abbas Safari alifariki dunia akiwa bado mjamzito.

"Uwezo mdogo ndio ambao umemfanya mtoto wangu mpaka leo sijampeleka Hospitali ya KCMC, nitatoa wapi kiasi hicho wakati mimi mwenyewe niko peke yangu mzazi mwenzangu alifariki nikiwa na mimba," anasema Salma. Mtoto anaishije? Abdulaziz anaishi kwa kufungwa kipande cha kanga kuzunguka tumbo na kifua, ili kuzuia anapojisaidia haja kubwa kumwagika chini.

Kipande hicho cha kanga, hubadilishwa kila baada ya muda ili kumfanya asikae na kinyesi muda mrefu. "Tunamfunga kitambaa cha nguo ili kuzuia kinyesi kisidondoke ovyo chini, " anasema Salma na kuongeza kuwa pamoja na kumfunga kitambaa pia humvalisha shati kuhakikisha kuwa hakuna uchafu unaoweza kuingia katika sehemu anayopitisha haja kubwa.

Salma anaomba wasamaria wema wamsaidie kumpatia fedha za kugharimia matibabu yake katika Hospitali ya KCMC ili mtoto wake aweze kuishi maisha ya kawaida. "Sina uwezo, ninaishi kwa shemeji yangu, ninaomba wenye uwezo wanisaidie mtoto wangu afanyiwe operesheni ili aishi kama watoto wengine," anasema.

Kwa upande wake, Mzee Kapela ambaye ni shemeji yake na Salma anawaomba wasamaria wema kujitokeza kumsaidia mwanamke huyo ambaye hana uwezo. "Mimi kwa sasa nawalea Salma na mtoto wake,lakini hata mimi sina uwezo wowote wa kumsaidia kumpatia matibabu mtoto Abdulaziz," anasema Mzee huyo. Anayeguswa kumsaidia mtoto Abdulaziz anaweza kutumia namba 0788 535130 au 0655 304336 kwa mawasiliano.

4 comments:

Anonymous said...

Kinyaiya sambaza ujumbe huu kwenye blogs na vyombo vingine vya habari.

Hiyo gharama ya matibabu, bado malazi, usafiri nk. Jaribu kufanya utafiti zaidi, ili watakaochangia wapate ujumbe uliokamilika.

Anonymous said...

imenisikitisha,nchi nyengine zilizoendelea unapewa vifuko maalum vinakaa vizuri kwenye tumbo,na kila baada ya muda unavibadilisha

Anonymous said...

kiukweli kama una mtoto lazima ulie,namshukuru mungu sana kwa kunipa kiumbe kilichokamilika mpaka sasa.tumsaidie huyu mtoto,kumbuka hujafa hujaumbika!!!
hii gharama ni ndogo sana twaweza msaidia.....tujitolee kumsaidia maisha yake naye awe mtu akisimama mbele za watu.

mama zarique

Anonymous said...

imenisikitisha sana hii habari kama mzazi lazima uumie,so far ben umefikia wapi katika kumsaidia huyu mama?naimani kama utaanzisha page itakayomuhusu yeye kuchangiwa au ukaitangaza na kumuombea misaada katika makampuni hiyo hela ni ndogo sana am sure watu wenye uwezo watajitokeza kumsaidia na its better now ambako bado mdogo isitoshe tusijekujilaumu please do something for the sake of that child wengine tutafanya tutakachoweza
kuna alot of people maarufu,alot of blogs,wasanii na watu wa kawaida watakaojitolea kumsaidia pia tigo hua wana ile special programme ya tigo they announce special number ambayo watu wanachanga any amount just kwa kutuma msg if people watakua aware of this atasaidia while the situation can stil be solved
thanks

Website counter