|  Baadhi  ya Wananchi wa  Ubaruku Wilayani Mbarali Mkoani Mbeya wakiangalia  Gari  pamoja na Kituo cha mafuta vilivyochomwa moto na wananchi  katika  vurugu zilizotokea baina ya wananchi na Polisi juzi.Picha na Brandy  Nelson  SAKATA la polisi kuua raia   kwa risasi katika kata ya Ubaruku Wilaya ya Mbarali Mkoani Mbeya  limeingia katika sura Mpya baada ya wananchi kumtaka Mkuu wa Wilaya hiyo  Kanali Kosmas  Kayombo kumkamata na kumpeleka kwao askari polisi  aliyemuua mwenzao kwa risasi, ili wamchukulie hatua za kisheria.
 
 Wakizungumza  kwenye mkutano na mkuu huyo wa wilaya jana, wanachi hao walisema  kitendo alichokifanya askari huyo ni cha kinyama na haawamini kwamba  kingeweza kufanywa na mtu kama huyo ambaye kazi yake ni kulinda usalama  wa raia na mali zao.
 Walimtahadharisha Mkuu huyo wa Wilaya  kuwa endapo kama hatua hazitachukuliwa haraka ikiwa ni pamoja na  kuwadhibiti wanaochochea uhasama wa kuwanyima haki wananchi, hali  inaweza ikizidi kuwa mbaya kwa sababu wengi wao wana hasira.
 
 Walidai  kwamba baadhi ya viongozi wa wa serikali ngazi ya wilaya pamoja na  baadhi ya polisi, ndiyo chanzo cha vurugu hizo zilizosababisha mauaji ya  mtu mmoja.
 
 Wakielezea jinsi mwezao alivyouawa, walisema kuwa  aliyeuawa alikuwa akibiashana na polisi na baada ya mvutano ndipo  alipochukua bunduki  na kumpiga risasi kwenye paji la uso.
 
 Walimweleza  mkuu huyo wa wilaya kwamba tukio hilo liliwafanya wananchi wapandwe na  hasira na kuanza kurusha mawe na polisi kurusha mabomu ya machozi na  risasi za moto ambapo mwananchi mmoja alipigwa risasi kiunoni.
 
 Majeruhi  huyo ambaye risasi ilipenya kiunoni  kwa nyuma na kutokezea mbele,  Hassan Masila, amelazwa katika  hospitali ya Wilaya ya Mbarali kwa  matibabu.
 
 Hassan aliliambia Mwananchi kuwa "nilipigwa risasi wakati nikikimbia baada ya kuona mwenzetu mmoja  kauwawa kwa risasi".
 
 Wananchi  hao walionekana kujawa na jazba kwenye mkutano huo ulioitishwa na Mkuu  wa Wilaya, na kupaaza sauti zao huku wakipiga kelele kiasi cha kufanya  kutokuwepo kusikilizana.
 
 Hali hiyo ilimpa wakati mgumu Mkuu wa  Wilaya na kumfanya mbunge wa jimbo hilo Dickson Kilufi na Diwani wa kata  ya Ubaruku George Mbila  kunyanyuka na kufanya kazi ya kuwatuliza na  kuwasihi wapunguze jazba.
 
 “Tunakuambia Mkuu sisi tunataka shamba  letu na huyo polisi aliyefanya mauaji kwa sababu tunamfahamu. Nyie  serikai ndiyo mmechangia haya mauaji kwani mmekuwa mkitunyanyasa sisi  weusi na kuwapendelea weupe. Sasa tunasema tumechoka, tupo tayari kufa  kwa lolote hivyo tunalitaka shamba letu na huyo polisi aliyeua,”  walilalamika.
 
 Shamba hilo ni moja kati ya yale yaliyokuwa yakimilikiwa na serikali wilayani Mbarali ambayo wamepewa wawekezaji mbalimbali.
 
 Mkuu  huyo wa Wilaya alipata nafasi finyu ya kuzungumza na wananchi hao  ambapo alisema kuwa malalamiko yao ameyachukua na atakwenda kuyafanyia  kazi.
 
 Alisema serikali tayari imeruihusu magari ya aina yoyote  kuingia Wilayani humo kauli ambayo hata hivyo wananchi waliendelea  kupaza sauti zao za kumataka Mkuu huyo atoe kauli ya mwisho ya  mkumuondoa Mwekezaji huyo.
 
 Akizungumzia tukio hilo kwa ujumla  Mbunge Kilufi alisema wananchi wa Ubaruku wana kero kubwa mbili ikiwa ni  pamoja na polisi kuzuia magari  makubwa yasichukue mazao yao na  kupeleka katika masoko ya nje na nadani ya nchi.
 
 Kero nyingine  akasema ni mwekezaji  mmoja kung'ang'ania mashamba yaliyopo nje ya  shamba alilokabidhiwa na serikali, huku akionekana kulindwa na baadhi ya  watendaji serikalini.
 
 Alisema kuwa vurugu hizo ni matokeo ya  baadhi ya watendaji wa serikali  kutokuwa makini na kutosikiliza ushauri  ambao wanapewa kabla ya kutokea matukio ya hatari na badala yake  kusikiliza maneno ya watu wachache kwa masilahi yao binafsi.
 
 Kilufi  alisema awali alimhoji Mkuu wa Polisi Wilaya (OCD) kuwa nani ametoa  kibali cha kuzuia magari makubwa yasiingie kubeba mazao ya wakulima  ambapo alijibu kuwa, amepewa amri kutoka kwa wakubwa.
 
 “Baada ya  kupata majibu hayo nilikwenda kwa mkuu wa Wilaya na kuuliza kama kuna  barua yoyote  yenye tamko la ambayo inaeleza kuzuia magari hayo.
 
 "Lakini  naye alinijibu kuwa hakuna barua yoyote na ndipo tilipomdhirishia Mkuu  wa Mkoa wa Mbeya John Mwakipesile ambapo aliruhusu kwa siku saba magari  hayo uandelee kuingia Wilayani humo ambapo baada ya kupita siku hizo  polisi walianza tena kuzuia magari hayo,” alisema Kilufi.
 
 Alifafanua  kuwa hadi kufikia juzi, akiwa njiani akitokea nyumbani alifika njia  panda ya Madibira na Rujewa ambapo alikuta lori la kubeba mafuta likiwa  limezuiwa na Askari mmoja wa usalama barabarani ambaye alimshirikisha  mbunge huyo kwa kumwambia kuwa gari hilo lilikotoka kwani haliruhusiwi  kuingia huko.
 
 “Yule Askari alivyonieleza hivyo nami nikamueleza  kuwa asiende na gari lake huko kwani wananchi hawatakubali kutokana na  kuwa wiki iliyopita walilizuia gari la mwekezaji lililokuwa limebeba  kokoto," alisema Kilufi na kuongeza.
 
 "Mimi niliwasihi waliache  lakini dereva huyo alisema yeye ameruhusiwa na Mkuu wa Polisi wa Wilaya  (OCD) basi mimi nikaendelea na safari yangu,” alisema
 
 Mbunge  huyo aliendelea kufafanua kuwa akiwa mjini alipigiwa simu kuwa kuna  vurugu zimetokea Ubaruku ambapo alirudi na kukutana na yule askari na  kumhoji  sababu za kuruhusu gari hilo liondoke na kwamba alimjibu kuwa  ni OCD.
 
 “Magari ya kubeba mazao yetu yanakataliwa kuingia lakini  haya ya wenzetu (wawekezaji) yanaruhusiwa hivyo sisi kama wananchi  tulikuwa tunamuhitaji OCD na Mkuu wa wilaya wafafanue kuhusu hali hiyo.
 
 "Lakini  polisi wao walivyokuja hawakutaka kutusikiliza na badala yake wakawa  wanalitaka hilo gari liondoke hapo na sisi wananchi hatukutaka na ndipo  mabishano yalipoanzia hapo,” alisema mmoja  aliyejitambulisha kwa jina  John Mwambuku
 
 | 
1 comment:
hao wananchi wa ubaruku mbarali ni wauaji wkubwa na hawana huruma,wanaweza kuuwa kwa dakika moja.polis wanasababu kubwa yakuzuiia magari yasiende kubeba mazao yao.polis wamechoka na hao wanainchi kazi yao kujichukulia sheria mkononi,yaani hapo ukigonga mtu hata kwa bahati mbaya na wewe lazima uuliwe,ninao ushahidi wakutosha,na fikili madereva wengi wanalielewa eneo hilo,wanasababisha ajari zikitokea wanakuja kundi unavamiwa gari litachomwa moto wtaiba vitu au wanapasua vioo vya gari.yaani unashuhudia mamayangu mdogo anapigwa mawe km mwizi kisa amewambia mmpiga gari limewakosea nini....polis wamechoka na vitendo vyao....kamwe sitakuja sahau eneo hilo la ubaru mbarali.
Post a Comment