Sunday, January 16, 2011

SAFI SANAA, JINO KWA JINO 2...

Wananchi wang'ang'ania wakabidhiwe polisi aliyeua kwa risasi Send to a friend

Baadhi ya Wananchi wa Ubaruku Wilayani Mbarali Mkoani Mbeya wakiangalia Gari pamoja na Kituo cha mafuta vilivyochomwa moto na wananchi katika vurugu zilizotokea baina ya wananchi na Polisi juzi.Picha na Brandy Nelson


SAKATA la polisi kuua raia kwa risasi katika kata ya Ubaruku Wilaya ya Mbarali Mkoani Mbeya limeingia katika sura Mpya baada ya wananchi kumtaka Mkuu wa Wilaya hiyo Kanali Kosmas Kayombo kumkamata na kumpeleka kwao askari polisi aliyemuua mwenzao kwa risasi, ili wamchukulie hatua za kisheria.

Wakizungumza kwenye mkutano na mkuu huyo wa wilaya jana, wanachi hao walisema kitendo alichokifanya askari huyo ni cha kinyama na haawamini kwamba kingeweza kufanywa na mtu kama huyo ambaye kazi yake ni kulinda usalama wa raia na mali zao.


Walimtahadharisha Mkuu huyo wa Wilaya kuwa endapo kama hatua hazitachukuliwa haraka ikiwa ni pamoja na kuwadhibiti wanaochochea uhasama wa kuwanyima haki wananchi, hali inaweza ikizidi kuwa mbaya kwa sababu wengi wao wana hasira.

Walidai kwamba baadhi ya viongozi wa wa serikali ngazi ya wilaya pamoja na baadhi ya polisi, ndiyo chanzo cha vurugu hizo zilizosababisha mauaji ya mtu mmoja.

Wakielezea jinsi mwezao alivyouawa, walisema kuwa aliyeuawa alikuwa akibiashana na polisi na baada ya mvutano ndipo alipochukua bunduki na kumpiga risasi kwenye paji la uso.

Walimweleza mkuu huyo wa wilaya kwamba tukio hilo liliwafanya wananchi wapandwe na hasira na kuanza kurusha mawe na polisi kurusha mabomu ya machozi na risasi za moto ambapo mwananchi mmoja alipigwa risasi kiunoni.

Majeruhi huyo ambaye risasi ilipenya kiunoni kwa nyuma na kutokezea mbele, Hassan Masila, amelazwa katika hospitali ya Wilaya ya Mbarali kwa matibabu.

Hassan aliliambia Mwananchi kuwa "nilipigwa risasi wakati nikikimbia baada ya kuona mwenzetu mmoja kauwawa kwa risasi".

Wananchi hao walionekana kujawa na jazba kwenye mkutano huo ulioitishwa na Mkuu wa Wilaya, na kupaaza sauti zao huku wakipiga kelele kiasi cha kufanya kutokuwepo kusikilizana.

Hali hiyo ilimpa wakati mgumu Mkuu wa Wilaya na kumfanya mbunge wa jimbo hilo Dickson Kilufi na Diwani wa kata ya Ubaruku George Mbila kunyanyuka na kufanya kazi ya kuwatuliza na kuwasihi wapunguze jazba.

“Tunakuambia Mkuu sisi tunataka shamba letu na huyo polisi aliyefanya mauaji kwa sababu tunamfahamu. Nyie serikai ndiyo mmechangia haya mauaji kwani mmekuwa mkitunyanyasa sisi weusi na kuwapendelea weupe. Sasa tunasema tumechoka, tupo tayari kufa kwa lolote hivyo tunalitaka shamba letu na huyo polisi aliyeua,” walilalamika.

Shamba hilo ni moja kati ya yale yaliyokuwa yakimilikiwa na serikali wilayani Mbarali ambayo wamepewa wawekezaji mbalimbali.

Mkuu huyo wa Wilaya alipata nafasi finyu ya kuzungumza na wananchi hao ambapo alisema kuwa malalamiko yao ameyachukua na atakwenda kuyafanyia kazi.

Alisema serikali tayari imeruihusu magari ya aina yoyote kuingia Wilayani humo kauli ambayo hata hivyo wananchi waliendelea kupaza sauti zao za kumataka Mkuu huyo atoe kauli ya mwisho ya mkumuondoa Mwekezaji huyo.

Akizungumzia tukio hilo kwa ujumla Mbunge Kilufi alisema wananchi wa Ubaruku wana kero kubwa mbili ikiwa ni pamoja na polisi kuzuia magari makubwa yasichukue mazao yao na kupeleka katika masoko ya nje na nadani ya nchi.

Kero nyingine akasema ni mwekezaji mmoja kung'ang'ania mashamba yaliyopo nje ya shamba alilokabidhiwa na serikali, huku akionekana kulindwa na baadhi ya watendaji serikalini.

Alisema kuwa vurugu hizo ni matokeo ya baadhi ya watendaji wa serikali kutokuwa makini na kutosikiliza ushauri ambao wanapewa kabla ya kutokea matukio ya hatari na badala yake kusikiliza maneno ya watu wachache kwa masilahi yao binafsi.

Kilufi alisema awali alimhoji Mkuu wa Polisi Wilaya (OCD) kuwa nani ametoa kibali cha kuzuia magari makubwa yasiingie kubeba mazao ya wakulima ambapo alijibu kuwa, amepewa amri kutoka kwa wakubwa.

“Baada ya kupata majibu hayo nilikwenda kwa mkuu wa Wilaya na kuuliza kama kuna barua yoyote yenye tamko la ambayo inaeleza kuzuia magari hayo.

"Lakini naye alinijibu kuwa hakuna barua yoyote na ndipo tilipomdhirishia Mkuu wa Mkoa wa Mbeya John Mwakipesile ambapo aliruhusu kwa siku saba magari hayo uandelee kuingia Wilayani humo ambapo baada ya kupita siku hizo polisi walianza tena kuzuia magari hayo,” alisema Kilufi.

Alifafanua kuwa hadi kufikia juzi, akiwa njiani akitokea nyumbani alifika njia panda ya Madibira na Rujewa ambapo alikuta lori la kubeba mafuta likiwa limezuiwa na Askari mmoja wa usalama barabarani ambaye alimshirikisha mbunge huyo kwa kumwambia kuwa gari hilo lilikotoka kwani haliruhusiwi kuingia huko.

“Yule Askari alivyonieleza hivyo nami nikamueleza kuwa asiende na gari lake huko kwani wananchi hawatakubali kutokana na kuwa wiki iliyopita walilizuia gari la mwekezaji lililokuwa limebeba kokoto," alisema Kilufi na kuongeza.

"Mimi niliwasihi waliache lakini dereva huyo alisema yeye ameruhusiwa na Mkuu wa Polisi wa Wilaya (OCD) basi mimi nikaendelea na safari yangu,” alisema

Mbunge huyo aliendelea kufafanua kuwa akiwa mjini alipigiwa simu kuwa kuna vurugu zimetokea Ubaruku ambapo alirudi na kukutana na yule askari na kumhoji sababu za kuruhusu gari hilo liondoke na kwamba alimjibu kuwa ni OCD.

“Magari ya kubeba mazao yetu yanakataliwa kuingia lakini haya ya wenzetu (wawekezaji) yanaruhusiwa hivyo sisi kama wananchi tulikuwa tunamuhitaji OCD na Mkuu wa wilaya wafafanue kuhusu hali hiyo.

"Lakini polisi wao walivyokuja hawakutaka kutusikiliza na badala yake wakawa wanalitaka hilo gari liondoke hapo na sisi wananchi hatukutaka na ndipo mabishano yalipoanzia hapo,” alisema mmoja aliyejitambulisha kwa jina John Mwambuku


1 comment:

Anonymous said...

hao wananchi wa ubaruku mbarali ni wauaji wkubwa na hawana huruma,wanaweza kuuwa kwa dakika moja.polis wanasababu kubwa yakuzuiia magari yasiende kubeba mazao yao.polis wamechoka na hao wanainchi kazi yao kujichukulia sheria mkononi,yaani hapo ukigonga mtu hata kwa bahati mbaya na wewe lazima uuliwe,ninao ushahidi wakutosha,na fikili madereva wengi wanalielewa eneo hilo,wanasababisha ajari zikitokea wanakuja kundi unavamiwa gari litachomwa moto wtaiba vitu au wanapasua vioo vya gari.yaani unashuhudia mamayangu mdogo anapigwa mawe km mwizi kisa amewambia mmpiga gari limewakosea nini....polis wamechoka na vitendo vyao....kamwe sitakuja sahau eneo hilo la ubaru mbarali.

Website counter