|  kocha wa Taifa Stars   Jan PoulsenKUTOELEWANA  kwa wachezaji  wa Taifa Stars  katika dakika 20 za mwanzo juzi ndiko  kulikoiponza timu hiyo na kuisababishia kipigo kikali cha mabao 5-1  kutoka kwa Misri.
 Hata hivyo, kocha wa Stars   Jan Poulsen  ambaye  aliungana kikosi hicho mjini Cairo akitokea kwao Denmark alisema kipigo  hicho kimewapa funzo,  lakini  watasahihisha makosa yao.
 Akizungumza  mjini hapa baada ya mchezo baina ya timu hizo kwenye Uwanja wa Arab  Contractors, Poulsen alisema timu yake ilifungwa na timu bora Afrika.
 
 “Tumecheza  na timu bora, huwezi ukalinganisha nafasi yetu ya 116 tuliyopo sisi  (Tanzania) na wao wakiwa katika 20 bora za dunia, pia ndiyo namba moja  Afrika.
 
 "Misri ni timu nzuri, imecheza vizuri, ni mabingwa mara  tatu mfululizo Afrika, vijana wangu walipambana vilivyo, lakini  walikutana na timu bora, naamini michezo ijayo tutaimarika,” alisema  Poulsen.
 
 Kocha huyo alieleza kuwa makosa machache waliyoyafanya  wachezaji wake yalitumiwa vizuri na wapinzani wao kufunga na hiyo  ilitokana na kucheza bila kuelewana dakika 20 za mwanzo.
 
 “Naamini hata Watanzania wamejifunza mengi kwa mechi ya leo (juzi), faida yake itaonekana mechi zijazo,” alisema Poulsen.
 
 Kocha  wa Misri, Hassan Shehata aliisifu Stars na kusema inahitaji marekebisho madogo, lakini itakuwa nzuri.
 
 Alisema  mchezo  ambao Stars ilicheza kipindi cha pili, kama ingefanya hivyo  kipindi cha kwanza, hana shaka kwamba mchezo ungekuwa mgumu kwao na  kusisitiza kuwa timu yake licha ya kupata ushindi mnono, lakini  ilikabiliana na upinzani mkali .
 
 Kwa upande wake, nahodha wa  Stars, Shadrack Nsajigwa  alisema hali ya hewa ya baridi kali nayo  iliwaathiri kwa kiasi fulani wachezaji wenzake hasa kipindi cha  kwanza,lakini baadaye walichangamka wakati tayari mambo yameharibika.
 
 Aliwaomba  Watanzania wasikatishwe tamaa na matokeo hayo na kukumbusha kuwa hata  kwenye michuano ya Chalenji iliyomalizika mwezi uliopita jijini Dar es  Salaam, timu ya  Tanzania Bara ‘Kilimanjaro Stars’ ilianza kwa kufungwa  bao 1-0 na Zambia lakini ikaibuka bingwa.
 
 Nahodha wa Misri, Wael  Gomaa alisema michuano hiyo ya soka kwa nchi za Bonde la Mto Nile ni  migumu na kwamba Tanzania si timu ya kubezwa, kwani ina wachezaji wenye  miili midogo, lakini wana vipaji.
 
 Juzi,  Stars juzi ilikubali  kipigo ambacho bao la kwanza lilifungwa na Said Khamdi dakika ya nne,  kisha dakika kumi baadaye Mohammed Aboutrika alifunga la pili na dakika  tisa baadaye beki Nadir Haroub  kujifunga.
 
 Bao la nne lilifungwa  na Said Khamdi tena dakika ya 57, wakati lile la mwisho lilifungwa na  Ahmed Ally, dakika ya 74 na la kufuatia machozi la Stars likifungwa na  mchezaji aliyetokea  benchi, Rashid Gumbo, dakika ya 77.
 
 Kesho  Stars itacheza na Burundi ambayo nayo juzi ilifungwa mabao 3-1 na  Uganda, hivyo ili Stars iweke hai matumaini ya kufuzu nusu fainali  italazimika kushinda na kusubiri mchezo wa mwisho dhidi ya Uganda.
 
 Michuano  hiyo inashirikisha timu saba zilizogawanywa katika makundi mawili,  ambapo timu mbili za juu kila kundi zitacheza nusu fainali, wakati timu  zitakazoshika nafasi ya tatu kila kundi zitacheza kuwania mshindi wa  tano.
 
 Bingwa wa michuano hiyo atazawadiwa zaidi ya Shilingi 200  milioni za Tanzania.
 
 | 
1 comment:
Na bado tumeshazoea kuona Taifa Stars ikifungwa na misri 5-1 au 4-1 ni kitu cha kawaida tu, tunajua wanapokwenda kucheza misri result inakua imeshajulikana haitaji hata wacheze, wachezaji wetu longolongo nyingi hapa Bongo katika club zao haswa Simba na Yanga lakini katika Taifa Stars ni wapo ziro bin sufuri kabisaaa, wanakimbizana hovyo kiwanjani hawajui wanachofanya na bila kutumia akili.
Post a Comment