Saturday, January 8, 2011

JAMANI KUFUNGWA 'HAMSA' NI HALI YA KAWAIDA KWENYE SOKA...

Dakika 20 zilitosha kuimaliza Stars- Poulsen Send to a friend

kocha wa Taifa Stars Jan Poulsen


KUTOELEWANA kwa wachezaji wa Taifa Stars katika dakika 20 za mwanzo juzi ndiko kulikoiponza timu hiyo na kuisababishia kipigo kikali cha mabao 5-1 kutoka kwa Misri.

Hata hivyo, kocha wa Stars Jan Poulsen ambaye aliungana kikosi hicho mjini Cairo akitokea kwao Denmark alisema kipigo hicho kimewapa funzo, lakini watasahihisha makosa yao.

Akizungumza mjini hapa baada ya mchezo baina ya timu hizo kwenye Uwanja wa Arab Contractors, Poulsen alisema timu yake ilifungwa na timu bora Afrika.

“Tumecheza na timu bora, huwezi ukalinganisha nafasi yetu ya 116 tuliyopo sisi (Tanzania) na wao wakiwa katika 20 bora za dunia, pia ndiyo namba moja Afrika.

"Misri ni timu nzuri, imecheza vizuri, ni mabingwa mara tatu mfululizo Afrika, vijana wangu walipambana vilivyo, lakini walikutana na timu bora, naamini michezo ijayo tutaimarika,” alisema Poulsen.

Kocha huyo alieleza kuwa makosa machache waliyoyafanya wachezaji wake yalitumiwa vizuri na wapinzani wao kufunga na hiyo ilitokana na kucheza bila kuelewana dakika 20 za mwanzo.

“Naamini hata Watanzania wamejifunza mengi kwa mechi ya leo (juzi), faida yake itaonekana mechi zijazo,” alisema Poulsen.

Kocha wa Misri, Hassan Shehata aliisifu Stars na kusema inahitaji marekebisho madogo, lakini itakuwa nzuri.

Alisema mchezo ambao Stars ilicheza kipindi cha pili, kama ingefanya hivyo kipindi cha kwanza, hana shaka kwamba mchezo ungekuwa mgumu kwao na kusisitiza kuwa timu yake licha ya kupata ushindi mnono, lakini ilikabiliana na upinzani mkali .

Kwa upande wake, nahodha wa Stars, Shadrack Nsajigwa alisema hali ya hewa ya baridi kali nayo iliwaathiri kwa kiasi fulani wachezaji wenzake hasa kipindi cha kwanza,lakini baadaye walichangamka wakati tayari mambo yameharibika.

Aliwaomba Watanzania wasikatishwe tamaa na matokeo hayo na kukumbusha kuwa hata kwenye michuano ya Chalenji iliyomalizika mwezi uliopita jijini Dar es Salaam, timu ya Tanzania Bara ‘Kilimanjaro Stars’ ilianza kwa kufungwa bao 1-0 na Zambia lakini ikaibuka bingwa.

Nahodha wa Misri, Wael Gomaa alisema michuano hiyo ya soka kwa nchi za Bonde la Mto Nile ni migumu na kwamba Tanzania si timu ya kubezwa, kwani ina wachezaji wenye miili midogo, lakini wana vipaji.

Juzi, Stars juzi ilikubali kipigo ambacho bao la kwanza lilifungwa na Said Khamdi dakika ya nne, kisha dakika kumi baadaye Mohammed Aboutrika alifunga la pili na dakika tisa baadaye beki Nadir Haroub kujifunga.

Bao la nne lilifungwa na Said Khamdi tena dakika ya 57, wakati lile la mwisho lilifungwa na Ahmed Ally, dakika ya 74 na la kufuatia machozi la Stars likifungwa na mchezaji aliyetokea benchi, Rashid Gumbo, dakika ya 77.

Kesho Stars itacheza na Burundi ambayo nayo juzi ilifungwa mabao 3-1 na Uganda, hivyo ili Stars iweke hai matumaini ya kufuzu nusu fainali italazimika kushinda na kusubiri mchezo wa mwisho dhidi ya Uganda.

Michuano hiyo inashirikisha timu saba zilizogawanywa katika makundi mawili, ambapo timu mbili za juu kila kundi zitacheza nusu fainali, wakati timu zitakazoshika nafasi ya tatu kila kundi zitacheza kuwania mshindi wa tano.

Bingwa wa michuano hiyo atazawadiwa zaidi ya Shilingi 200 milioni za Tanzania.


1 comment:

Anonymous said...

Na bado tumeshazoea kuona Taifa Stars ikifungwa na misri 5-1 au 4-1 ni kitu cha kawaida tu, tunajua wanapokwenda kucheza misri result inakua imeshajulikana haitaji hata wacheze, wachezaji wetu longolongo nyingi hapa Bongo katika club zao haswa Simba na Yanga lakini katika Taifa Stars ni wapo ziro bin sufuri kabisaaa, wanakimbizana hovyo kiwanjani hawajui wanachofanya na bila kutumia akili.

Website counter