Tuesday, October 5, 2010

SIKIA KILIO CHA DADA YETU HUYU MWENYE UPOFU....


Bonitha Bangi


“TANGU nianze kutumia dawa za kupunguza makali ya Ukimwi (ARV’s) hali yangu kiafya inazidi kuwa mbaya siyo kwa sababu dawa hizi zinanidhuru la hasha! Ila ni kwa kuwa sina uwezo wa kufanya kazi ili nipate fedha za kununulia chakula kutokana na ulemavu wangu wa kutoona.”

Hayo ni maneno ya mkazi wa Kijiji cha Mazombe-Ilula, wilayani Kilolo, Iringa, Bonitha Bangi ambaye ambaye ameishi na maradhi hayo kwa miaka tisa sasa anavyoeleza.

“Muda wote nafikiria wapi nitapata chakula ili nikimeza dawa nisijisikie vibaya lakini mara zote huwa sipati jibu… mbaya zaidi tangu mume wangu afariki, familia pia imeyumba na wanangu wanaishi kwa kutangatanga, wengine wamekimbilia mjini.”

Ukibahatika kuzungumza naye, unaweza kutoa machozi na hayaji kwa sababu Bangi anaishi na VVU hapana, ila ni kutokana na ukweli kwamba, machozi na kwikwi ndizo zinazosindikiza maelezo yake.

“Sitakufa kwa sababu ya ukimwi ila kwa sababu ya njaa kwani nakunywa dawa bila kula chochote jambo ambalo naamini ndilo litakaloniharakisha kuonja mauti,” anasema.

Aligunduaje kuwa na maambukizi?
Tangu kifo cha mumewe mwaka 2002, afya yake ilianza kuyumba jambo ambalo lilianza kuitia shaka familia yao wakidhani kuwa pengine wamerogwa.

“Kila mtu nyumbani kwetu alijua kuwa mume wangu amerogwa kwani maisha yetu yalikuwa mazuri ndiyo maana nilipoanza kuumwa sikujua kama nimeathirika, niliamini kuwa nimerogwa,” anasema.

Alitibiwa katika hospitali mbalimbali bila kupata naafuu na baadaye akaamua kwenda kwa waganga wa kienyeji ambao walimweleza kuwa amerogwa. Alipewa dawa nyingi na kutimiza masharti yote ya waganga hao lakini hakukuwa na nafuu yoyote zaidi ya kuendelea kupoteza nguvu na kukonda kila kukicha.

“Mapunye yalikuwa yakiniota mwili mzima na kila nikitibiwa ugonjwa huu, mwingine unajitokeza na ikafikia hatua nikachoka nikijua mwisho wangu wa maisha umefika,” anasema.

Baada ya miaka mitatu, hali ilikuwa mbaya zaidi hivyo akaamua kwenda tena hospitali ambako wataalamu wa afya wakamshauri apime ili ajue kama amepata maambukizi ya VVU au la.

Ushauri wao niliupinga kwa sababu nilijua siwezi kuwa na Ukimwi kwanza ningeutoa wapi wakati nilikuwa mwaminifu kwenye ndoa yangu, siku zote nilijua mume wangu amerogwa na hakuwa na maradhi yatokanayo na ukimwi,” anasema.

Bangi ambaye amezaliwa mwaka 1979, katika Kijiji cha Ifunda, Iringa anasema baadaye aliamua kupima ndipo alipopata majibu kwamba ameathirika.

“Sikuamini, nilishikwa na butwaa na nikahisi madaktari wanidanganya kwa sababu niliamini kwamba siwezi kuwa na VVU kwani nilijua huo ni ugonjwa watu wenye tabia mbaya hasa za kimalaya. Nashukuru elimu kuhusu ukimwi niliyoipata ilinipa mwanga nikajua nini maana ya ukimwi."

Mwaka 2008, Bangi alianza kutumia ARV akipata huduma hiyo katika hospitali ya misheni inayomilikiwa na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) iliyopo Ilula.

Anasema kuwa matumizi ya dawa hizo yalirejesha matumaini ya kuendelea kuishi kwani hakujua kama angeweza kupata nafuu kutokana na hali aliyokuwa nayo.

Anasema kabla hajaanza kutumia dawa hizo, alikuwa akihudumiwa na ndugu zake hivyo chakula haikuwa tatizo jambo lililomfanya apate nafuu na baadaye kupona maradhi yote yaliyokuwa yakimwandama.

Anasema matunda ya dawa hizo yalimfanya arejee nyumbani kwake akiwa na wanae watatu ambao walikuwa wakisoma shule ya msingi kwake kwa ajili ya kuanza maisha mapya ya uzima.

Anasema ili akidhi mahitaji yake na wanae, ilimpasa aanze kufanya vibarua vya kulima mashamba ya nyanya licha ya kuwa hakuwa na uwezo wa kufanya kazi kubwa kama watu wanaoona.

Malipo duni kwa kazi hiyo hayakuweza kukidhi mahitaji yake ikiwemo kununua chakula jambo lililomfanya aamue kuingia mtaani kuomba.

“Niliamua kuanza kazi ya ombaomba nilijisikia aibu kuifanya hasa pale nilipokuwa nikikutana na watu ambao wananitukana na kunikebehi bila kujua tatizo langu. Maisha yalizidi kuwa magumu na ikafika wakati tukaanza kupata mlo mmoja kwa siku,” anasema.

Watoto wake waliamua kuacha masomo kutokana na njaa kwani hawakuwa na uwezo wa kumudu masomo bila kula na mmoja wao akaamua kukimbilia mjini ili asake maisha.

“Mwanangu alikimbia baada ya kugundua mama yake sina uwezo wa kumhudumia, mpaka leo sijui yuko wapi na anahali gani, naamini kuwa ni miongoni mwa watoto wanaozurura huko mjini,” anasema.

Anasema hofu yake kubwa siyo ukimwi ambao zamani alijua akibainika kuwa nao atakufa. Hofu yake kubwa ni kukosa chakula wakati anatumia ARV’s.

“Dawa bila chakula ni hatari sana na zinanifanya nijisikie kichefuchefu na wakati mwingine nakosa nguvu kabisa,” anasema.

Changamoto nyingine kubwa anayokabiliana nayo ni kutokuwa na uhakika wa kulipa pango la nyumba anayoshi. Anasema huenda akatimuliwa wakati wowote ikiwa mwenye nyumba atachoka kumvumilia.

Maisha kabla ya maradhi
Kabla mumewe hajafariki dunia, alikuwa akipata mahitaji yote muhimu kutokana na ukweli kwamba mumewe alikuwa akimpenda, na kumjali licha ya ulemavu wake wa kutoona.

Anasema haikuwa rahisi kwa familia hiyo kushinda au kulala njaa kutokana na baba huyo wa familia kutimiza wajibu wake hasa ikizingatiwa kwamba mkewe hakuwa amebahatika kupata elimu na hakuwa na uwezo kufanya kazi ngumu kama kilimo.

“Nilikuwa na uwezo wa kupika na kufanya kazi zote za nyumbani kama kawaida, nililetewa mahitaji yangu na sikuwahi kujua kama siku moja nitaishi kwa kuhangaika na watoto, sikujua kama mwanangu anaweza kuja kunikimbia,” anasema.

Anachoomba
“Naomba kusomeshewa watoto wangu walau waje kunikoa siku za usoni maana wenzangu wote wanaona. Kama wakiendelea kutangatanga mtaani kwa kazi ya kuomba, maisha yanaweza kuja kuwa magumu zaidi ya hayo.”

Mbali na kusomeshewa watoto hao, Bange anasema kuwa anatamani kufanya biashara ambayo anaamini kupitia hiyo anaweza kuondokana na ugumu wa maisha.

No comments:

Website counter