Mmoja wa watu walioathirika na Ukimwi mkoani Iringa kwa kuwahudumia wagonjwa wa Ukimwi ni Dorotea Maliatabu (58) mkazi wa Ilula Wilayani Kilolo.
Maliatabu, anasema aliambukizwa virusi hivyo kutokana na kumuhudumia binti yake na dada yake, bila kujikinga. Kwa mujibu wa Maliatabu, alianza kumuuguza binti yake kuanzia mwaka 2005 mpaka alipofariki dunia 2006.
Baada ya binti yake huyo kufariki mwaka 2007 alianza kumuuguza dada yake ambaye mwaka huohuo alifariki.
“Huyu binti yangu alikuwa akiishi hapa Iringa lakini yeye dada alitoka Dar es Salaam akaja huku akiwa anaumwa,” anaeleza Maliatabu.
Anasema alikuwa akiwapa huduma zote wagonjwa hao bila kuchukua tahadhari yoyote na kuwa hiyo ndiyo sababu ya yeye kupata maambukizi ya Ukimwi.
“Nilikuwa nafua nguo zao, kuwaosha na kuwafunga vidonda bila kuvaa ile mipira ya mikononi (cloves)” anafafanua.
Maliatabu anasema, aliwahudumia wagonjwa hao bila tahadhari kutokana na kutoamini kuwa binti yake ama ndugu yake wa damu anaweza kumuambukiza ukimwi kwa kumuhudumia.
“Nilikuwa naona kufanya hivyo ni sawa na kuwadharau, lakini pia hata vifaa venyewe havipatikani kwa urahisi huku,” anaeleza.
Mama huyu anasema baada ya mgonjwa wake wa mwisho kufariki, ndipo na yeye alipoanza kuugua.
Baada ya kuugua kwa muda mrefu, huku afya yake ikiwa inazorota, aliamua kwenda katika kituo cha afya cha Ilula ambako aligundulika kuwa na kifua kikuu.
Kwa mujibu wa Maliatabu, hata baada ya kutibiwa na kupona kifua kikuu afya yake iliendelea kuzorota na ndipo alipoamua kumtafuta muhudumu wa wagonjwa wa Ukimwi majumbani aliye katika eneo hilo, ili amsaidie angalau ushauri.
“Afya yangu wakati huo ilikuwa siyo nzuri kabisa, nilipokwenda kwa Kindole (muhudumu wa wagonjwa wa Ukimwi majumbani), nilimweleza hali halisi ya afya yangu na ndipo alipoita wataalam wakaja wakanipima na nikagundulika kuwa nimeambukizwa Ukimwi,”:
“Inaniuma sana, yaani ugonjwa umenifuata nyumbani kwangu na uzee wote huu,” anaeleza kwa masikitiko Maliatabu.
Maliatabu ambaye kwa sasa anaishi na mjukuu wake wa kike, anayemsaidia mambo mbalimbali. Anasema afya yake imeanza kuimarika tangu alipoanza kutumia dawa za kurefusha maisha (ARVs).
Muhudumu wa wagonjwa majumbani, Laudi Kindole anayefanya kazi chini ya taasisi ya Tunajali inayofadhiliwa na shirika la misaada la Marekani (USAID), anaeleza kuwa maambukizi ya virusi vya Ukimwi katika eneo la Ilula yapo juu mno hasa kwa wazee.
Anasema, sababu inayofanya vikongwe hawa waambukizwe virusi vya ukimwi kwa wingi ni kutokana na kutotumia tahadhari wakati wakiwauguza wagonjwa na haswa ndugu zao wa damu.
“Wengine tumewapa elimu lakini utakuta wanasema kutumia vifaa kwa watoto ni dharau na matusi kwa hiyo wanaamua kufanya shughuli hizo bila tahadhari,” anaeleza Kindole.
Anaeleza pia kuwa, katika eneo hilo la Ilula Sokoni ambalo kaya zake hazizidi sabini, anahudumia zaidi ya wagonjwa wa Ukimwi 120.
“Hapa Ilula Sokono kuna kaya kama 70, katika hizi kaya mimi ninahudumia wagonjwa zaidi ya 120, na kuna mashirika mengine ambayo pia yana wahudumu hapa,” anaeleza Kindole.
Kwa mujibu wa Kindole, mbali na wagonjwa hao wanaohudumumiwa na wahudumu wa kujitolea kutoka katika mashirika mbalimbali, pia idadi ya watu walioathirika ambao hawajajitangaza ni kubwa kuliko ya wale waliojitangaza.
Anasema kuwa, katika eneo hilo wagonjwa wengi wakiwemo walioambukizwa kwa kuwahudumia ndugu zao ni wanawake.
“Wanaume walioathirika pia ni wengi lakini hawajitangazi na wengi wao wanasambaza virusi kwa makusudi,” anaeleza.
Akieleza sababu nyingine za kupanda kwa maambukiz hayo anasema ni pamoja na ulevi uliokithiri na baadhi ya watu kuambukiza virusi kwa maksudi.
“Wapo ambao hata sisi tunawapa dawa, wakisha pata nafuu huanza kufanya ngono zembe wakiamini wamepona na wengine wakijua kabisa kuwa wanasambaza virusi vya ugonjwa huo,” anaeleza.
Kwa mujibu wa Kindole, katika kata ya Ilula kuna zaidi ya wahudumu 35 kutoka katika mshirika mbalimbali wanaojitolea kuwahuduma zaidi ya wagonjwa 300.
Naye Mkurugenzi wa Kituo cha Allamano kinachohudumia watu waishio na virusi vya ukimwi na familia zao Sista Mikela Astegiano, anasema maambuki ya ukimwi yataendelea kupanda kila kukicha mkoani humo kutokana na baadhi ya watu kusambaza virusi hivyo kwa makusudi.
Sista Astegiano anasema, hata baadhi ya wagonjwa wanaohudumiwa na kituo hicho kilichopo chini ya Shirika la Masista wa Konsolata, mara wakianza kutumia dawa na kupata nafuu huanza kusambaza virusi kwa maksudi.
“Sisi tuna watumishi wengi katika eneo hili ambao wanawafahamu vizuri watu hawa, utakuta tanawahudumia vizuri kwa kuwapa dawa na baadhi yao hata chakula, lakini wakipata nafuu tuu wanaingia mitaani na kuanza kusambaza ukimwi,” analeza.
Kwa mujibu wa Sista Astegiano, sheria ya ukimwi inatakiwa iwabane watu hawa ili waache tabia hiyo lakini pia iwape frusa wadau wa ukimwi kufikisha taarifa za watu wenye tabia hizo katika ngazi za juu ili wachukuliwe hatua.
Wakati wadau hawa wakitoa maelezo hayo, Meneja wa kanda za Nyanda za juu wa Shirika la Tunajali Dk John Kahemele, anasema bado tafiti za kina zinahitajika kubaini sababu ya maambukizi ya VVU kuwa juu katika Mkoa wa Iringa.
“Kama ni ujwaji wa pombe, kupita barabara kuu, kurithi wajane, baridi, na mambo mengine yanayosemwa yapo katika maeneo mengi, labda utamaduni wa jamii ya watu wa huku kutotairiwa inaweza kuwa sababu kwakuwa tafiti mbalimbali zinaonyesha kutotairi hurahisisha maambuki ya Ukimwi,” anaeleza Dk Kahemele.
No comments:
Post a Comment