Saturday, August 27, 2011

KWENYE KONA YA MAHABA LEO HII...


KAMA ilivyo ada leo kwenye 'KONA YA MAHABA' nitazungumzia faida na hasara za uongo katika mapenzi, unaweza kushangaa kusikia uongo una faida yake.

Kila akifanyacho mwanadamu kina faida na hasara lakini kiimani kila lililokatazwa na Muumba lina hasara halina faida.

Katika maisha yetu ya kila siku tumekuwa tukitumia uongo asilimia kubwa kuliko ukweli ili kuyaficha ambayo mtu si vigumu kukutambua unasema uongo.
Naweza kusema kuna baadhi ya watu hupenda kudanganywa kuliko kuambiwa ukweli.

Wanawake wengi wamewafanya wanaume waishi kwa uongo ili kulinda penzi lao, kwani kama atasema ukweli basi penzi halitakuwepo au kuingia katika migogoro kwa kuonekana huna uwezo wa kummiliki.

Wanawake wengi hupenda wanaume wenye uwezo wa kifedha ambao huamini wanaweza kuwatatulia matatizo yao na kuwaogopa wanaume wanaosema kweli juu ya maisha yao na kuwaona hawawafai.

Hata baadhi ya wanaume hupenda wasichana wa hadhi fulani ili apate ‘ujiko’ hasa anapomtambulisha kwa watu.

Wanaume hupenda wanawake wenye majina au watoto wa mawaziri, wabunge au wa vigogo fulani. Pia hata makazi yao huwa na ujiko, mfano ukisikia msichana anatoka Masaki unajua mambo yao supa hata kama hatembelei gari.

Lakini msichana hata akiwa mrembo akikueleza anatoka Tandika au Tandale kwa Mtogole unajua ndiyo wale wale ‘mademu wa mizinga na vichwa vya kuku’.

Hii imekuwa ikiwafanya watu wengi kuuziwa mbuzi kwenye gunia na kuchanganyikiwa mbele ya safari baada ya kuujua ukweli wakati huo umekwisha chelewa.Faida ya uongo katika mapenzi;

Kupata ulichokusudia kwa urahisi kwa kumdanganya kuwa vyote ulivyomuahidi utamtimizia.

Kwa mfano mwanaume mtanashati hudanganya chochote kwa mwanamke kama ana fedha pia hata kukupeleka kwenye chumba cha rafiki yake mwenye uwezo kwa kuogopa kukupeleka kwake utabadili uamuzi.

Kwa vile moyo wa mwanamke unapenda vitu vizuri udanganyika kirahisi, akiisha timiza dhamira yake humuoni tena hata ukienda alipokuelekeza kwake unaambiwa pale si kwake aliomba kwa mazungumzo tu.

Wapenzi wasio wakweli wapo kwa ajili ya tamaa ya kitu na si mapenzi ya kweli, uongo wake huwa kama turufu itakayomfanya akupate kwa urahisi na akiisha kukupata anaingia mitini.

Wapo wanaume ambao huazima nguo au gari ili kutongozea wanawake ambao hupenda maisha ya juu kwa kuamini penzi tamu ni la mtu mwenyewe uwezo na kusahau upendo wa mtu haubebwi kwa fedha au utanashati wake.

Mtego huu huwanasa wenye tamaa ambao hutaka kwa haraka bila kuchunguza historia ya mwanaume kwa vile wameahidiwa kitu basi anaingia kichwa kichwa mwisho wa siku kilio cha kusaga meno.

Hata kama umempenda, inabidi uchukue muda kidogo kufanya uchunguzi wa taratibu ili kumjua kwa undani. Jiepushe kutaka penzi la gharama ambalo hulindwa na uongo wa kuahidiwa mpaka kunakucha hakuna ulichokipata.

Punguza tamaa, acha uamuzi wa haraka kwani utaweza kugundua mambo mengi.

No comments:

Website counter