Saturday, August 20, 2011

JAMANI TUMSAIDIE MWITA, ANAHITAJI MSAADA WENU WAUNGWANA...“ILIKUWA siku ya huzuni kubwa kwangu. Niliamka asubuhi na mapema ili nijiandae kwenda kibaruani kwangu na mara nikasikia kelele zilizokuwa zikitokea kwenye mgodi wa North Mara.”Hiyo ni kauli ya Samwel Nyangoye Mwita (35), mkazi wa Sirari, Wilaya ya Rorya Mkoani Mara ni ambaye ni mmoja kati ya watu waliopigwa risasi katika tukio hilo. Yeye alipigwa risasi kifuani na risasi hiyo ikatokea mgongoni na hadi sasa hali yake siyo nzuri.Mwita anakumbuka tukio hilo la Mei 16 mwaka huu ambalo lilimkumba yeye akiwa mkazi wa Nyabirama.Anasema: “ Niliamka mapema kwa ajili ya kujiandaa kwa kazi zangu na wakati nikipiga mswaki nikasikia kelele kutoka eneo hilo la mgodi.”

Anaeleza kuwa kutokana na kelele hizo aliacha kupiga mswaki na kuelekea katika eneo hilo ili kuangalia ni kitu gani kilikuwa kimetokea kule kwani si kawaida kwa muda huo watu kupiga kelele.“Kwa kuwa nilikuwa naishi jirani na mgodi wa North Mara ambapo mtu akipiga kelele lazima nisikie, niliposikia kelele hizo za watu zikiashiria kuwapo kwa jambo, nikaitika ili kujionea,” anaeleza.

Anasema alielekea kwenye eneo hilo na ndipo aliwakuta watu wamejazana kwenye mgodi huo ulioko Nyamongo naye akasimama mbali kidogo na eneo lile.Anaeleza kuwa wakati akishangaa na kutaka kujua ni nini kimetokea kwa wale watu ambao wamejikusanya kwenye mgodi huo, mara aliona magari sita ya polisi yakiingia kwenye eneo la mgodi kwa kasi.

“Katika magari hayo aina ya landrover defender walishuka askari polisi wengi na waliposhuka walianza kufyatua risasi za moto kuelekea kwa watu waliokuwa wamesimama nje ya uzio wa mgodi,”anasimulia.
Anasema alipoona risasi zinapigwa ovyo aliamua kuondoka na katika kufanya hivyo alishtukia akipigwa risasi ya kifua.

Anaeleza kuwa kulingana na alivyosimuliwa na wenzake waliokuwapo kwenye tukio hilo, Mwita anasema baada ya kupigwa risasi ile alipoteza fahamu na kuanguka na wenzake walimsaidia wakidhani amekufa.Anaongeza kuwa walimkokota na kumpeleka walipokuwa wamesimama askari polisi na kumkabidhi kwao huku wakiamini amekufa.

"Nilipoanguka nilipoteza fahamu na walinipeleka kwa polisi wakidhani nmekufa na kwa hasira za wananchi hao waliwaambia polisi hao kuwa wauchukue mwili wao ambao wameua,"anaeleza Mwita. Anaeleza kuwa kulingana na simulizi za wenzake, polisi walimchukua na kumwingiza kwenye gari lao ambalo lilibeba maiti tano akiwamo pia yeye na walipelekwa kwenye kituo cha afya katika mgodi huo.Anaeleza zaidi baadaye maiti hizo akiwamo yeye walihamishiwa Hospitali ya Wilaya ya Tarime ili wakahifadhiwe katika chumba cha maiti. "Maiti ziliposhushwa nikiwamo nami, lakini wakati wakinishusha walitokea watu ambao walikuwa wamekuja kuzitambua maiti zao,waliponiangalia wakagundua kuwa nilikuwa napumua, ijapokuwa kwa shida, "anasimulia Mwita. Naye Suleiman Marwa ambaye ni kaka yake (Mwita) anasema baada ya kumwona anapumua walimchukua na kumpeleka katika wodi namba saba katika hospitali ya Temeke ambako alilazwa na kupatiwa matibabu. "Watu wa kwanza kufika wodini alikuwa shemeji yake , shangazi na mke wake ambao walielezwa wamtolee damu ili aweze kuwekewa pindi damu chafu inapotolewa na damu nyingine kuwekwa,"anasema .Anangeza: "Waliotoa damu alikuwa shemeji yake nyingine ilinunuliwa hospitalini hapo ambapo aliwekewa lita tano." Baada ya hapo, Mwita anasema alihamishiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando, Mwanza ambako walikodi gari na walikwenda na muuguzi kutoka Hospitali ya Wilaya ya Tarime ambaye aliondoka baada ya kufika Bugando. Anasema alipofikishwa katika hospitali hiyo alipatiwa matibabu alishonwa mgongoni katika sehemu ilipotokea risasi na sehemu ya kifuani ilipoingilia risasi walimwekea mpira wa kutolea damu chafu.Anaeleza kuwa alipatiwa matibabu katika kipindi cha wiki mbili baada ya wiki hizo walisimamisha matibabu yote huku hali yake ikiwa bado siyo nzuri. "Nilimwuliza daktari kwanini sikuwa nikipatiwa matibabu, naye akanijibu kuwa wao wanachotibu ni majeraha na kwamba wanaangalia kifua change kama napumua vizuri na kwamba walionifikisha pale ilikuwa ni kwa ajili ya matazamio,"anasema. Anasema alielezwa na daktari(Angela) aliyekuwa akimtibu kuwa kipimo cha x-ray kilionyesha risasi imepita kwenye uti wa mgongo, hivyo si mtu wa kupona haraka. Anasema baada ya kusikia maneno hayo ilimlazimu aombe kuruhusiwa kwenda nyumbani akiamini kwamba hata akibaki hospitali asingeweza kupona. "Nilimwomba daktari ammruhusu mdogo wangu arudi nyumbani na nilikubaliwabaada ya kuwa hospitali kwa siku 27,"anasema Marwa.“Nilimwona daktari ili anieleze kama kuna uwezekano wa kumhamishia katika hospitali nyingine, lakini nilikutana na muuguzi nikiomba kumwona daktari wake (Angela), naye alinijibu kuwa alikuwa kwenye chumba cha upasuaji. “Muuguzi alipoenda kwa daktari alimwagiza atuulize kama mgonjwa wetu alikuwa ameanza kunyanyua mguu name nilimjibu kuwa bado hajaweza, naye aliondoka na kurudi kwa daktari.Nesi alipotoka kwenye chumba cha upasuaji alitoka na jibu ambalo alipewa na daktari kuwa maagizo alishayatoa na alishawaeleza kama tuna fedha za kupoteza tufanye tunavyotaka. "Yeye alishasema mgonjwa hawezi kupona kutokana na vipimo vya x-ray kuonyesha kuwa risasi ilikuwa imepita katika uti wake wa mgongo,"anasema Marwa.Baada ya majibu yake nilimwuliza nesi huyo kama vipimo vyote alivyotakiwa mdogo wangu afanyiwe alikuwa mefanyiwa vyote, lakini alinijibu na kumwambia kuwa hakupimwa kipimo cha CT- SCAN ambacho kimeharibika na hakifanyi kazi. Marwa anaongeza kuwa kipimo cha x- ray nacho aliambiwa kimeharibika na kwamba walikuwa wakitumia x- ray ya Hospitali ya Jeshi kwa mgonjwa aliyeandikiwa kipimo hicho. Anasema waliamua kumwomba daktari wao ili awape barua ya kwenda Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), lakini alikataa na kusema hawawezi kumtoa mgonjwa kutoka Bugando na kumpeleka MNH."Daktari alitunyima barua akisema kuwa Bugando ni ya rufaa, hamwezi kwenda MNH kwani zote ni rufaa kama sisi tumeshindwa ndio wao wataweza?" Anasema. Julai 15 walifika MNH kwa kutumia karatasi waliyoruhusiwa kutoka Bugando na walipokelewa vizuri. "Sisi tulitoka kwa dis-charge ambayo ilitusaidia katika kupokelewa pale MNH na walimpeleka katika kipimo kiitwacho MRI ambacho gharama yake ni Sh350,000,"anasema. Walipoenda kufuata majibu ya kipimo hicho waliambiwa kipimo hakijaonyesha vizuri hivyo mgonjwa wao alitakiwa arudie tena kipimo hicho.Anasema kwa hali aliyokuwa nayo kwa sasa kuanzia kwenye kitovu kurudi kwenye miguu imepooza, yeye amekuwa ni mtu wa kubebwa na hivyo hawezi hata kusogeza mguu. "Nimeshapooza siwezi kwenda sheemu yeyote ni mtu wa kubebwa kama choo kikubwa ni hapa hapa na kidogo natumia mpira,"anasema. Anaongeza kuwa hajaanza kupata tiba MNH na vipimo anavyotakiwa kupima si kimoja bali ni zaidi ya vitatu, hivyo anawaomba wasamaria wema wamsaidie.Vile vile, anaiomba Serikali imsaidie katika matibabu, kutokana na ukweli kuwa hafanyi tena kazi na maisha yake ni magumu, ndugu zake hawana uwezo . Anasema ana mke na watoto watatu ambao wanamtegemea na hivyo kuhitaji msaada.Anayetaka kumsaidia- Mwita -Simu- 0753-518773 au 0759-315584 au 0789-905060 (Selemani Marwa(kaka yake)


No comments:

Website counter