Wednesday, June 1, 2011

KUTANA NA MZEE WA SHABA 'ORIGINO'...



SAID BAJIA; Mpishi mahiri wa pilau aliyewahi kuwapiki Rais KIKWETE na MAMA SALMA!
HANA mipaka, anawapikia viongozi, watu wenye majina makubwa katika jamii na watu wa kawaida, ili mradi wamekubaliana, huyu ni mpishi asiyekuwa na ubaguzi, Awadh Ahmed Omary maarufu kama Said Bajia.

Mpishi huyu aliyezaliwa miaka 65 iliyopita katika Kijiji cha Kwahani, Kisiwani Zanzibar alianza kwa mara ya kwanza kujishughulisha na masuala ya upishi akiwa na umri wa miaka 17.

HABARILEO Jumapili, baada ya kusikia habari za mpishi huyo hodari, kama kawaida haikusita kumtafuta ili kufahamu ni kitu gani kimemwezesha kufanya kazi hiyo ya upishi kwa muda wa miaka zaidi ya 40 sasa bila kupoteza mwelekeo.

Saidi anasema mara ya kwanza alianza kujishughulisha na kazi ya upishi mwaka 1963 akiwa nyumbani kwao Kwahani baada ya dada yake ambaye wamechangia mama alipofariki, hii ni baada ya mama yake kumuita mpishi anayemtaja kama Hassan Mula Bai mwenye asili ya Kihindi na Kiarabu kuja kupika msibani.

“Mpishi huyo alipofika alimuomba mama yangu aniruhusu nimsaidie shughuli ndogo ndogo wakati akiandaa chakula cha msiba…aliniambia wewe mdogo nisikilize mimi. Roho yangu iligawanyika sehemu mbili huku nilikuwa nataka huku ninasita,” anasema.

Anasema siku hiyo mpishi huyo alipika sufuria ya pilau ya ratili 30 ambayo ni sawa na pishi 10 na kwamba yeye (Saidi) alifanya kazi ya deiwaka na jukumu lake lilikuwa kutwanga vitunguu swaumu, kuosha mchele na kazi nyingine ndogo ndogo.

“Ingawa mama yangu aliniruhusu, lakini alikuwa na wasiwasi, hivyo aliniita pembeni na kuniuliza ‘unaendeleaje, vipi moto?’ mimi kwa ujasiri nikamjibu mama hakuna shida naendelea vyema tu na kazi,” anasema na kuongeza baada ya kukamilisha kazi yao Bai alimpa asante ya shilingi moja kwa kazi aliyofanya.

Kwa mujibu wa Said, siku nyingine Bai akawa na zabuni nyingine ya kwenda kupika na alimuomba waende naye, hata hivyo mama yake alisita, lakini baada ya mpishi huyo kumshawishi sana mama huyo alikubali.

“Mama yangu alisita kuniruhusu, lakini Bai alimuomba sana na kumuahidi kuwa atanifundisha kazi hiyo na kwamba itakuja kunifaa baadaye…alimwambia mama, huyu mwanao ana kichwa kizuri na anaonekana anaipenda kazi hii. “Niliporudi mama aliniuliza kuhusu moto, na mimi niligangamala na kujibu hakuna shida nimeweza tu.

Baada ya kufanya kazi tena kwa mara nyingine mpishi huyo alinipa asante ya Shilingi mbili na nikampa mama shilingi moja,” anasema. Said anasema Bai alipata tena zabuni ya kupika Jamatini (Msikiti wa Wahindi) kwa siku 12, hivyo alimchukua tena na walifanya kazi kubwa sana ya kupika siku zote hizo na kutaja baadhi ya vyakula walivyopika kuwa ni pamoja na ladu, silo, mchuzi, mseto wa wali na choroko, biriani na pilau.

Mpishi huyo anasema Novemba mwaka 1964 alikuja Dar es Salaam kutafuta maisha na anakumbuka kipindi hicho nchi ya Zambia ndiyo ilikuwa ikipata pia uhuru wake.

Akiwa ameshafika katika maskani Dar es Salaam alipata kazi katika Hoteli ya Rubi mkabala na ulipokuwa ukumbi wa Sinema wa Cameo ambapo alifanya kazi ya upishi kwa malipo ya Sh 150.

Anasema baadaye yule mwalimu wake wa upishi (Bai) naye aliamua kuja Dar es Salaam kutafuta maisha na alipata zabuni ya kupika katika Msikiti wa Jamatini uliopo barabara ya Morogoro na Zanaki na alimwalika (Said) kwenda kufanya naye kazi maana alijua sasa anaye mwanafunzi aliyepikika.

“Tulifanya kazi hapo Jamatini, lakini baadaye Bai aliamua kustaafu na kuniuliza kama nitaendelea, lakini nilikataa kubaki hapo kwa sababu nilifahamu kuwa wale waliompa tenda hawawezi kunichukulia kama mtu waliyekuwa wanamfahamu,” anasema.

Said anasema aliendelea kufanya kazi za upishi kwa kupata zabuni mbalimbali na siku moja aliitwa kupika chakula mtaa wa Pemba na Lumumba na kumbe ilikuwa ni shughuli za jamaa wa mwalimu wake mpishi Bai na walipokutana alimwambia maneno haya, “usiharibu kazi yangu,” hivyo alipika chakula kwa ufundi wake wote na waliokula walifurahia.

Anasema bahati mbaya, Bai alifariki dunia lakini pia ameacha urithi kwa mtoto wake mmoja anayemtaja kwa jina la Abdallah Hassan ambaye ni mpishi anayeishi Msasani na kwamba amekuwa akimuenzi mwalimu wake huyo kwa kushirikiana na familia yake.

Kwa mujibu wa Said alikaa mtaa wa Mchikichini karibu na Msikiti wa Mtoro alipokuwa akifanya kazi yake ya upishi akiwa na msaidizi aliyemtaja kwa jina la Salum Dassi, hata hivyo kijana huyo baada ya kupata fedha aliamua kwenda nchini Pakistani kutafuta maisha, lakini akafia huko.

Alipata msaidizi wa pili anayemtaja kwa jina la Kassim Makilika. Akikumbuka anasema alipata zabuni ya kwenda kupika wilayani Nzega, Tabora katika sherehe ya Maburushi mwaka 1971 lakini walipofika huko Makilika akaanza kuugua na mwisho alifariki.

Hata hivyo, Said hakukata tamaa aliporudi aliendelea na kazi, huku akifundisha vijana wengine na hadi anaondoka eneo la Mchikichini ameacha vijana zaidi ya 20.

Mpishi huyo anasema miaka ya 1980 alipata kazi ya kupika katika kantini za mashirika, alianza kwa kupata tenda kantini ya RTC iliyopo barabara ya Pugu na kwamba alipika chakula kwa ajili ya wafanyakazi na kingine kilikuwa kwa ajili ya wanamgambo waliokuwa kambini, huko alifanya kazi kwa kushirikiana na Omary Abdallah.

Said anasema kuna rafiki yake ambaye pia ni mpishi anayemtaja kwa jina la Abdulbari Abubakari aliyepata zabuni katika kantini ya Kampuni ya General Tyre kwa ajili ya kupikia maofisa na wafanyakazi walioko katika maghala na hivyo alimuomba washirikiane kupika wote, hata hivyo baada ya muda alipata zabuni sehemu nyingine na alimuacha msaidizi wake anayemtaja kama Zakaria.

Anasema vijana aliokuwa akiwaacha alikuwa anawaamini kwa sababu alikuwa amewapa mafunzo ya kutosha ya namna ya kupika.

‘Mungu hamtupi mja wake’, mwaka 1982, Said alipata tenda NASACO ambapo alipewa jukumu la kwenda kufanya kazi ya upishi katika meli ya Kigiriki anayoitaja kwa jina la Mantle Line na hivyo alipandishwa ndege anaikumbuka Lufthansa Airline na kwenda Ujerumani ilipokuwepo meli hiyo na alifanya kazi kwa miezi sita.

“Ndani ya meli hiyo nilifanya kazi kama Msaidizi wa Mpishi Mkuu, Kigiriki waliniita Palamagra…nilipata uzoefu wa kupika vyakula vya Kigiriki,’ anasema.

Baada ya kumaliza zabuni hiyo ya miezi sita ndani ya meli, Said alirudi Tanzania na rafiki yake anayemtaja kwa jina la Nassoro Buheri aliyekuwa akifanya kazi kama Msimamizi Mkuu wa Stoo wa Shirika la Ndege la Tanzania alimuunganishia tenda ya kupika katika mgahawa wa shirika hilo uliokuwa ukijulikana kama Ndege Restaurant.

“Nakumbuka tulikuwa tukipika siku ya Jumatano Pilau na siku ya Jumamosi Biriani na watu walikuwa wakipenda sana chakula changu,” anasema mpishi huyo ambaye anapozungumza unaona hasa anaipenda kazi yake.

Nassoro alimpatia tena zabuni nyingine ya kwenda kufanya kazi ya upishi katika meli nchini Dubai na hivyo mwaka 1986 aliondoka na vijana wengine 10 kwenda Dubai yeye akiwa kama mpishi na wengine walikwenda kwa shughuli nyingine mbalimbali.

“Unajua ukipata kazi usifanye hiana, kama kuna nafasi wape na wengine na hayo ndio maisha,” anasema. Saidi anasema baadaye alirudi Tanzania na ameendelea kufanya shughuli zake za upishi kwa kupata mialiko ya kupikia watu mbalimbali wakiwemo viongozi na watu maarufu.

Anawataja watu maarufu aliowahi kuwapikia na wengine ambao hadi leo bado wanamuita wakiwa na shughuli zao mbalimbali.

Mpishi huyo anasema aliwahi kumpikia John Malecela wakati huo akiwa Waziri wa Mawasiliano na Uchukuzi, alipika nyumbani kwa Malecela Oysterbay chakula cha wageni aliokuwa amewaalika baada ya kuunganishiwa zabuni na Ibrahim Raha (Jongo) wa Redio Tanzania.

Anasema pia alipika chakula cha usiku kwa ajili ya Harusi kati ya Rais Jakaya Kikwete na Salma Kikwete (wakati huo Kikwete hajawa bado Rais) nyumbani kwa marehemu Ditopile Mzuzuri ambaye alikuwa Naibu Waziri wa Mawasiliano na Uchukuzi.

Amewahi kumpikia pia Rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi wakati akimuozesha binti yake Fatma, lakini alifahamiana na Mwinyi wakati akiwa Waziri wa Mambo ya Ndani katika shughuli iliyofanyika katika mtaa wa Livingstone.

Hakuishia hapo Said amewahi kupika katika shughuli mbalimbali za Mama Anna Mkapa kwanza wakati mama huyo akifanya kazi Ofisi za Umoja wa Mataifa na siku Rais Mstaafu Benjamin Mkapa akiapishwa, Said alipata zabuni ya kupika chakula cha wageni nyumbani kwa Mkapa eneo la Upanga.

“Nimeshawahi kwenda Old Moshi na Mama Mkapa kwa ajili ya kupika kwenye msiba wa mdogo wake na mpaka leo huwa ananiita katika shughuli zake mbalimbali zikiwepo semina za wajasiriamali anazofanya mara kwa mara,” anasema na kuongeza kuwa kutokana na kuthamini kazi yake anasema hata wakati wa msiba wa Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere Mama Mkapa alimtafuta na kumpa kazi ya kupika siku mbili msibani.

Said amewahi pia kumpikia Bhoke Munanka (marehemu) miongoni mwa mawaziri katika Baraza la Mawaziri la kwanza la mawaziri wa Tanganyika huru, akiwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais akishughulikia Usalama wa Taifa nyumbani kwake Kimara wakati wa harusi ya mwanawe anayemtaja kwa jina la Sila.

Mpishi huyo anasema ameshatembelea wilaya na mikoa 17 ya Tanzania na kuitaja mikoa ambayo hajawahi kwenda kuwa ni Kigoma, Ruvuma na Mara. Hivi sasa anasema anaendelea na kazi yake ya upishi kwa kupata mialiko ya kupikia watu mbalimbali ndani na nje ya Mkoa wa Dar es Salaam au mara nyingine amekuwa akiunganishiwa zabuni na watu aliowahi kuwapikia.

Said ana mke anayemtaja kama Halima Mohammed Kassim aliyefunga naye ndoa mwaka 1998 na wamebahatika kupata watoto wanne, watatu wa kiume na mmoja wa kike anaowataja kuwa ni Ahmed, Mohammed, Omary na Barke.

Anamtaja Ahmed aliyeko darasa la saba katika Shule ya Msingi Upanga kuwa na muelekeo wa kupenda kazi ya baba yake. Anasema ametoka katika familia ya watoto saba wakiwemo wanawake watano na wanaume wawili, yeye akiwa kitindamimba na kwamba baba yao alifariki wakati akiwa na miezi sita.

Hivi sasa anasema katika familia yao wamebaki wanawake wanne na mwanamume mmoja. Mpishi huyo anasema amesoma mpaka darasa la nne na anawataja baadhi ya viongozi aliowahi kusoma nao kuwa ni pamoja na Rais wa Zanzibar Dk. Ali Mohammed Shein na Waziri wa zamani wa Fedha wa Zanzibar Suleiman Nyanga aliosoma nao madrasa.

Akizungumzia mtazamo wa watu kuhusu upishi anasema upishi ni taaluma kama taaluma nyingine na kuongeza, “bora kufanya kazi ukapata kipato kuliko kupiga watu roba barabarani.”

Kutokana na shughuli zake za upishi anasema anaweza kupika vyakula vya aina mbalimbali vikiwepo vyakula vya Kihindi, Kifilipino, Kiarabu, Kizungu na Kigiriki, lakini pia anafahamu kuoka mikate na keki.

Akikumbuka anasema, “mfano nilipokuwa katika meli ya Kigiriki sikufahamu lugha lakini tuliwasiliana kwa macho tukaelewana na nikawa nawapikia wanachopenda.” Nini kimewezesha aweze kudumu katika kazi hiyo mpaka leo, Said anasema, “uaminifu na ukweli ndio vimenifanya niendelee kufanya kazi hii hadi leo.

Kama napewa kazi ya kupika chakula fulani iwapo sikiwezi nasema ukweli siwezi, ninachoweza nasema naweza.”

Said anasema ana uwezo wa kupika chakula cha watu 2,000 hadi 3,000 na kutoa mfano wa gharama za mapishi kuwa kilo 30 za mchele kupika biriani ni Sh 20,000 wakati pilau ni Sh 10,000 na kazi nyingine au mapishi ya vitu vingine kama mboga, mchuzi ni maelewano na kisha mnakubaliana naye pia gharama za mapishi, ingawa anasema sio kubwa na inalingana na ukubwa wa kazi.

Anataja mafanikio yake aliyopata kuwa ni fedha za kula na kutunzia mke na watoto wake pamoja na kuwasomesha. Mpishi huyo mahiri mwenye makazi yake katika Mtaa wa Muhoro, Kariakoo anamalizia kwa kusema, “sitastaafu kazi yangu ya upishi mpaka nione nimepinda mgongo.”

3 comments:

Anonymous said...

jamani naomba contact zake nina shughuli mwezi wa saba nimuwahi mapema.plzzzzzzzzzzzz

Anonymous said...

Yaani wewe mdau ulijuaje, nikwenda kwenye hitma ya mama wa rafiki yangu akapika biriani yaani ilikuwa tamu kiama. Naomba namba ya simu Ben tafadhali

Irene said...

Hongera sana baba kwa kazi nzuri unayoifanya. Mungu azidi kukupa kheri na maisha marefu. Nimefurahia sana historia yake hadi alipo sasa.

Website counter