Saturday, June 4, 2011

ASANTE SANA KAKA ISSA KWA KUTUFUNDISHA JAMBO HILI LA KUTIMIZA NDOTO HATA KAMA KUNA 'KIZINGITI' KIKUBWA...


Maambukizi ya Ukimwi siyo mwisho bali changamoto!

Issa athumani Juma

“KUISHI kwangu na virusi vya ukimwi si sababu ya kunifanya nibweteke na kuniachisha kazi. Nilipovunja ukimya na kujitangaza niliamua kujikita katika kilimo na biashara ya kuuza mkaa na muhogo na biashara hii imenisaidia kuendesha maisha yangu bila matatizo.

Nawashangaa wale wanaoona kwamba kupata virusi vya Ukimwi ndiyo mwisho wa safari ya maisha na wengine wakianza kujinyanyapaa wenyewe au kukata tamaa na hata kuamua kukaa nyumbani bila kujishughulisha wakisubiri kufa, hii si sahihi jamani acheni fikra potofu.”

Hizi ni kauli na ushauri wake Issa Juma (40), mkazi wa Luhangai, Kata ya Msimbu, Kisarawe Pwani anapoeleza kuwa anaishi na virusi vya ukimwi (VVU) kwa miaka 12 hadi sasa akiwa amepitia safari ndefu.
Katika ushuhuda wake kwa timu ya waandishi wa habari waliotembelea eneo hilo ili kujua mafanikio na changamoto za utoaji wa huduma za afya chini ya uratibu wa Shirika la Utu Mwanamke (WD), Issa ana simulizi ndefu.

Kwa utulivu mkubwa anaeleza kuwa alizaliwa mwaka 1970 na kusoma elimu ya msingi kijijini hapo ambako hakubahatika kuendelea na masomo ya sekondari.

Kama kijana alianza kusaka maisha na ndipo alipokutana na mkasa huo mwaka 1997 alipokwenda Chalinze kwa ajili ya kutafuta maisha. Huko ndipo alipokutana na msichana mmoja waliyependana na kuishi pamoja kama mume na mke.

“Niliishi naye kwa upendo mkubwa kwa kipindi cha miaka mitatu na ndipo mwaka 1999 mwenzangu akafariki dunia, tukamzika sote tukijua kuwa alikufa kwa kuugua malaria na si ugonjwa wowote mwingine,” anasema.

Anaongeza kuwabaada ya kumzika mpenzi wake huyo ukaanza kuenea uvumi katika mitaa ya mji ule wa kibiashara wa Chalinze kwamba mwenzake huyo alikuwa amekufa kwa ukimwi kwani wakati akiugua alikuwa na vipele wote na mwili
wake ulikuwa umevimba.

Anasema kuwa hakuyatilia maanani madai hayo kwani hakuwa na wasiwasiwowote kutokana na ukweli kwamba yeye binafsi bado alikuwa na afyanzuri, tena bila kusumbuliwa na maradhi yoyote.

Mwaka uliofuata, Issa anasema aliamua kwenda kituo cha afya Chalinze ili kupima na kujua hali yake kiafya, lakini hata hivyo wakatiakifanya maamuzi hayo hakuwa na wasiwasi kama angekutwa na maambukizi.

Baada kupima majibu, anasema aliyopewa yalionyesha kuwa akiishi na virusi vya ukimwi, lakini hakuwa na hofu kwani afya yake ilikuwa nzuri na alikuwa akifanya kazi za nguvu bila tatizo.

Ulipofika mwaka 2002, anaeleza kuwa hali yake kiafya ikaanza kubadilika taratibu kwa mwili kudhoofu na kusakamwa na magonjwa nyemelezi ndipo akaamuakurejea nyumbani kwao Kisarawe.

Akiwa kijijini hapo, Issa anasema aliamua kwenda kupima tena kwa mara ya pili katika zahanati ya Sungwi , Masaki ambako vipimo vilionyesha kwamba anaishi na virusi vya ukimwi na
akapewa maelekezo ya kwenda Hospitali ya Wilaya ya Kisarawe kwa ajili ya kupima kiwango cha kinga iliyopo mwilini mwake (CD4).

Kilichomsukuma hadi akaamua kupima kwa mara ya pili anasema ilitokana na kusumbuliwa kwa maradhi ya kikohozi cha mara kwa mara na kuumwa na kichwa pamoja na kiuno.

Hata hivyo, Issa anasema hakwenda Hospitali ya Kisarawe kama alivyoelekezwa na wauguzi wa zahanati ya Sungwi bali alifanya maamuziya kwenda kituo cha afya cha Chanika ambako alipewa idadi kubwa ya vidonge na kuchomwa sindano.

“Nilipopima kiwango cha kinga ya mwili, yaani CD 4 nikaonekana ninazo 180 tu nikatakiwa niende Hospitali ya Kisarawe kwa ajili ya kuanza kupewa mafunzo ya kuanza kutumia dawa za kurefusha maisha, ARVs kwa bahati
nzuri nilifuzu na kuanza kutumia na hadi leo ninaendelea nazo,” anasema.

Maisha mapya na virusi

“Kama kuna kipindi kigumu katika maisha yangu ni wakati wa kuanzakuishi maisha mapya baada ya kupimwa na kubainika kuwa na maambukizi ya virusi vya ukimikwi, kwanza ndugu zangu hawakukubali kabisa walisema nimerogwa,” anasimulia.

Hata alipojaribu kuwahakikishia kwamba amepima mara mbili nakubainika kuwa na virusi hawakukubaliana naye kwani kwa kipindi hicho hakuwa amedhoofu bali alikuwa na nguvu zangu akiendelea na kazi tena za kutumia nguvu.

Anaongeza kuwa iliwachukua muda mrefu ndugu zake kuamini kwamba anaishi na virusi vya ukimwi kwani baada ya kumweleza kaka yake nayealifikisha ujumbe kwa baba yake mkubwa.

Baaada ya kufikisha ujumbe huo kwa ngazi ya familia yake Issa anasema alianza kuonja joto ya jiwe kwani unyanyapaa ulikuwa ukijionyesha waziwazi, ndugu zake wengine walianza kumtenga, hawakuwa wakimpa taarifa hata kwenye shughuli za harusi na misiba na hata alipokwenda mezani wakati wa kula walikuwa wakimtengea chake peke yake mbali na wengine.

Tatizo la kutengwa huko na ndugu zake lilimtesa kwa muda mrefu, lakini baadaye akaamua kwenda kutoa taarifa kwa washauri wake nasihi wa Hospitali ya Kisarawe alikokuwa akichukulia dawa za ARVs.

Ushauri alioupata kutoka kwa mshauri wake ni kwamba alitakiwa arudipo kijijini kwake avunje ukimya kwa kujitangaza rasmi kwa watu mbalimbali ili wamtambue rasmi.

“Ushauri huu ulinisaidia sana kwani ndiyo ulionipa ujasiri ambao ninaohadi sasa wa kuzungumzia wazi wazi juu ya afya yangu. Kwanza, nilipofika kijijini nikaanza kupita kwenye maskani za kahawa za watu wazima na vijiwe vya vijana na kuwaeleza wazi kuwa naishi na virusi na niliwataka nao waende kupima afya zao,” anaeleza.

Kuvunja huko kimya anasema kulimweka njia panda kwani wachachewalikubaliana na ushauri wake, lakini idadi kubwa ya wazee kwa vijanawalianza kumsema na kumnyanyapaa wakimwimbia, ‘anao’

Miongoni mwa waliokuwa mstari wa mbele katika kumsakama na kunyanyapaa ni rafiki wa kaka yake ambaye hata nyumbani aliwashauri wakati wa kula chakula wasile naye kwani anaweza kuwaambukiza.

Hali hiyo anasema ilimweka katika wakati mgumu mno,lakini kaka yake alikuwa akimfariji na kumtaka asisikilize maneno ya watu kwani hilo ni tatizo mtambuka.

Anasema alikaa na hali hiyo kwa kipindi cha mwaka mmoja, lakini ghafla alipokuwa akihudhuria kliniki ya kuchukua dawa Hospitali ya Kisarawe alikutana na rafiki wa kaka yake aliyekuwa mstari wa mbele kumnyanyapaa naye akiwa katika foleni ya kusubiri ARVs.

"Aliponiona alinifuata huku akilia machozi na kuniomba radhi akitakanimsamehe kwa aliyokuwa amenitendea kwani hakujua kama tatizo hilolinaweza kumkumba mtu yeyote,lakini mimi nilimwambia kuwa nimemsamehena tukaanza maisha mapya,” anasimulia.

Hata hivyo, Issa anasema rafiki huyo wa kaka yake hivi sasa ni marehemu amefariki kutokana na kushindwa kufuata masharti ya matumizi ya ARVs nakujikinga na maambukizi mapya.

Kimaisha, Issa anasema anaendesha shughuli zake za kilimo cha mahindi, muhogo, kunde, maharage na maboga na wakati wa kiangazi hujishughulisha na biashara ya kuuza mkaa akiusafirisha kwa baiskeli kuutoa Luhangai hadi Chanika, Manispaa ya Ilala mkoani Dar es salaam.

Anasema anashika mwenyewe jembe na kulima mashamba yake na wakati mwingine huamua kulima vibarua ili kujiongezea kipato na kwamba kituambacho hapendi katika maisha yake ni kubweteka eti kwa sababu anaishi na virusii na kusubiri misaada.

Mbali ya shughuli hizo za kilimo, Issa anasema kuwa yeye ni mwelimishaji rika kiongozi wa kituo cha afya cha Masaki ambacho kinawahudumia wanavijiji wa Sungwi na maeneo mengine yakiwamo pia ya mkoa wa Dar es Salaam na Pwani akiwa amepewa baiskeli,tochi viatu vya mvua na mwavuli .

Jukumu hili la uelimishaji rika alikabidhiwa tangu mwaka 2009 baada ya wataalamu wa International Columbia University
Program (ICAP) kupitia mafaili yake na ambapo amekuwa akipewa posho kwa kila mwezi

Issa amekuwa akihamasisha kwa kutumia kauli mbiu ya, ‘Dozi
Kamili, Muda Sahihi Kila Siku Kwa Maisha Yote’ na anasisitiza kuwa kupata maambukizi siyo mwisho wa maisha, bali ni changamoto ambayo inatakiwa kupokewa na mhusika na kuikubali huku akiondoa wasiwasi juu ya maisha yake.

Issa anaeleza kuwa kwa sasa anafanya maandalizi ya kuoa mke kwani amempata mchumba ambaye pia anaishi na virusi na kwamba anatarajia maisha yao yatakuwa ya furaha kwani wote wanajitambua.

Anawashauri wananchi wote kujitokeza na kupima ili kujua mapema afya zao kabla ya kuachia virusi kushambulia kabisa kinga za mwili na wanapobainika wasikate tamaa.

No comments:

Website counter