Monday, May 16, 2011

SHIME WADAU TUMSAIDIE KIJANA MWENZETU HUYU ALIYE KWENYE MAUMIVU MAKALI JAMANI...Zuberi Juma Bora: Ugonjwa huu wa ajabu unanitesa!
“NIMESHINDWA kuendelea na masomo ya sekondari baada ya kumaliza shule ya msingi na miguu yangu kuanza kuwasha na kisha baadaye ikawa hivi, " anaeleza Zuberi Juma Bora (36). "Kwa kweli ninapata shida kubwa siwezi kutembea ukikanyaga unaumia na michanga pamoja na mawe, kuvaa viatu siwezi miguu kila kukicha inakua, nawaombeni wasamaria wema wanisaidie kama upo uwezekano, wanipeleke nje nikatibiwe,” anaeleza

Bora alipata tatizo la kuvimba miguu chini ya unyayo hadi miguu yakeugonjwa ambao ulimpata mwaka 1985 akiwa darasa la nne katika Shule ya Msingi Komsala, kata ya Kwamatuku wilayani Handeni mkoani Tanga.

Anaeleza tatizo lake hilo lilianza na kuwashwa kwenye sehemu ya chini ya nyayo zake za miguu , kisha ikavimba yote na kupasuka na kuanza kutoa maji maji ambayo hayakuwa ya kawaida.

“Huwezi kuamini, maana wakati ikiwasha nilidhani nimekanyaga majani ambayo hupatikana mashambani, hivyo nilipojikuna na kadri nilivyoendelea muwasho ulizidi na hatimaye miguu yote ikavimba na kupasuka, ilitoka maji yaliyokuwa na harufu kali.

Kwa kweli kila aliyekuwa akiniona alinionea huruma, ndugu zangu walishindwa wafanye nini na uwezo wetu ni mdogo,” anaeleza Bora.

Anaongeza kuwa bada ya kupasuka huko kwa miguu wazazi wake walimpeleka katika Hospitali ya Kwamkono ambako timu ya madaktari walimfanyia uchunguzi bila mafanikio na hali yake iliendelea kuwa mbaya baada ya miguu yake kuanza kuwa na nyama ambazo zilikuwa zikimsababishia maumivu ambayo yanaendelea hadi sasa.

Mama mzazi wa kijana huyu, Mwasiti Rashidi (58), anasema kijana wake alipatwa na maradhi hayo akiwa shule ya msingi na alikuwa miongoni mwa watoto wake tegemezi sana na aliyekuwa akifanya vizuri darasani, lakini baada ya kupata ugonjwa huo alianza kufanya vibaya darasani na katika mitihani yake.

“Zuberi alikuwa siyo mtundu shuleni alikuwa akifanya vizuri na nilikuwa na mategemeo naye kwa vile ni mtoto wangu wa kwanza ambaye nilijua atafika mbali, lakini alipopata ugonjwa huu hata maendeleo yake darasani yalizorota kabisa, sisi wazazi hatuna cha kufanya, tumemwachia Mungu,” anasema mzazi huyo.

Anaongeza kuwa mwanae huyo tangu alipoanza kuumwa na miguu na baada ya kumfikisha hospitali bila mafanikio walijaribu tiba za mitishamba kwa waganga wa jadi wilayani na zile za jirani, lakini hawakupata mafanikio na bado miguu ya kijana wake inaendelea kuota nyama na kuoza.

Huku machozi yakimtoka mama huyo ambaye anaeleza kuwa kila anapofikiria maumivu ya mwanae na mategemeo makubwa kwake anajisikia uchungu.

Anaongeza kuwa kwa miaka miwili iliyopita amepatwa na upofu wa kutokuona baada ya kuumwa kichwa kwa muda mrefu bila ya mafanikio.

“Kwa kweli nyumba yetu imeingia katika mtihani mkubwa, mimi nimepata upofu sioni tena sasa na mwanangu huyu wa kwanza niliyekuwa nikimtegemea ndiye huyu miguu yake imeota nyama kila kukicha zinazidi kuongezeka, hatujui itafika hadi wapi na majaliwa yake yatakuwa vipi.
Kila nikifikiria yote haya nakosa amani katika moyo, naomba wasamaria wajitokeze na watusaidie kupata tiba ya mwanangu,” anasihi mama yule.

“Hapa unapouona kila siku tunatumia Sh800 ambazo pia ni vigumu kuzipata, uwezo wetu kiuchumi mdogo, unavyotuona hapa, tunanunua dawa za kupunguza maumivu ili tuweze kupungza maumivu yake, vinginevyo tukikosa hatulali usiku kucha kwa maumivu.


"Mme wangu kazi zake za kuuza kuni kuna siku hawezi kwenda kuuza kutokana na matatizo mbalimbali ya kutuhudumia,” anasema Mwasiti.

Baba mzazi wa kijana huyo, Juma Zuberi Bora (68), anasema tangu mwanae huyo na mkewe wapate maradhi hayo amekuwa na wakati mgumu katika maisha yake kwani licha ya kuwasaidia wagonjwa wake bado analo jukumu la kukata kuni porini kwa ajili ya kwenda kuuza ili kupata fedha za kujikimu.

Pia, anaeleza kuwa anakabiliwa na jukumu jing hiyoine la kulima shamba lao ambako hivi sasa ameshindwa kufanya hivyo kwa kiasi cha kuridhisha kutokana na kukosa usaidizi wa familia yake.

“Kwa kweli maisha katika familia yangu yamekuwa magumu sana, wenzangu walikuwa msaada kwangu wakinisaidia katika shughuli za shamba, lakini sasa mimi nimeachwa peke yangu nikakate kuni za kuuza huko Korogwe Mjini ili tupate fedha na wakati huo huo nikalime kwa ajili ya kupata chakula, kweli ni tabu,” anasema mzee huyo.

Anaeleza kuwa wakati mtoto wake akianza na maradhi hayo na baada ya kumfikisha Hospitali ya Kwamkono, ilibidi wasamaria wema wa kijiji cha Komsala wamsaidie kwa fedha kiasi cha Sh10,000 ambazo zilimwezesha kumsafirishia kijana wake hadi hospitali ya wilaya ya Korogwe, Magunga ambako hata hivyo hakuweza kupona.

Anaiomba serikali na wadau wengine wajitokeze kumsadia katika kuhakikisha anaweza kufikishwa katika hospitali kubwa zilizopo kama Muhimbili, Dar es Salaam au KCMC iliyoko Moshi, Kilimanjaro au hata nje ya nchi ili wakajaribu namna ya kumponya mwanae huyo.

Anaeleza kuwa maumivu aliyo nayo kijana wake yanampa mtihani mkubwa kwani yanazidi kuwa makubwa kila uchao.

“Ninaomba wasamaria, mashirika mbalimbali ya dini na serikali watusaidie hata ikiwezekana mwanangu aweze kupelekwa katika hospitali kubwa na hata nje ya nchi kwa ajili ya kuchunguzwa zaidi pengine, naamini ataweza kupona,” anasema mzazi huyo ambaye anakiri kuzaa watoto 12, lakini walioko hai ni watano.

Mzazi huyo anasema kuwa katika kazi yake ya kuuza kuni amekuwa akikutana na changamoto mbalimbali ikiwemo kufukuzana na watendaji kata na wakati mwingine kukosa vibali vya kusafirishia kuni na mkaa ambao wakati mwingine amekuwa akiuza katika mji wa Korogwe kwa ajili ya kupata fedha za kujikimu za kumwezesha kumudu maisha yake na familia yake.

Anasema kuwa mzigo wa kuni anaosafirisha kwenda Korogwe ambako ambako hupata kati ya Sh1,000 hadi 1,500 kwa siku, fedha anazozitumiakwa matumizi ya chakula na dawa za tiba kwa mke na mtoto wake huyo.

Anaeleza pia kwa siku ambazo haendi Korogwe amekuwa akizitumia kwa ajili ya kupumzika na kwenda shambani, hivyo suala la msaada kwa familia hiyo linahitajika mno kwani hivi sasa tatizo limeongezeka baada ya mkewe kupata upofu.

Kwa wale wanaotaka kumsaidia yeye na familia wanaweza kuwasiliana naye kupitia kwa Hussein Semdoe kwa namba za simu- 0715-694443/ 0784-694443 au kwangu mimi mwenyewe BEN KINYAIYA kwa simu namba 0655 705 055, ntauwasilisha mchango wako wa hali na mali kwa kijana mwenzetu huyu ambaye kwa hakika anateseka sanaaa jamani, mbona kwenye Vikao vya harusi mnatoa 'malaki kwa malaki' ya Fedha iweje tushindwe kumsaidia kijana mwenzetu huyu aliye kwenye maumivu makali na usiku halali kwa vilio vya maumivu...

5 comments:

Anonymous said...

ushauri wangu ben mtumie na michuzi kule maana kuna watu wengi wanaangalia huwezi jua

Anonymous said...

nikweli uyo anonymous said mtumie michuzi na blog nyingine zote mana ni huruma sana kwakweli watu watajitokeza na ww pia unajuana na watu wengi naimani pia utakuwa msaada mkubwa hata mm takuwa msaada

Anonymous said...

ni kweli mtumie michuzi na jide na blog nyingine kuhusu ili mana inasikitisha sana tena sana anaitaji msaada wa haraka na kama umeguswa na ww beni pleas unajuana na watu wengi unaweza ukawa msaada mkubwa pia

Anonymous said...

KIKOMBE KIMOJA CHA BABU MAMBO YOTE SHWARI....

Anonymous said...

na hakika binadamu yeyote atakayeona picha hii basi labda awe ana moyo wa plastiki ndo hatoumia kuona picha hii jamani naomba tumsaidie huyu mtoto chochote tulichokuwa nacho tuchangie kumuokoa huyu kijana hebu imagine ungekuwa ni wewe au mwanao amepata tatizo hili au nduguyo? inshaalah atapona tutazidi kumuombea kwa mungu Ameen

Website counter