Monday, May 9, 2011

KAZI NI KAZI BANAA MRADI 'MAMBO' YANANYOOKA HOME...


Tutatupa: Mbogamboga zimenitoa kimaisha!
KAZI ni kazi bora mkono uende kinywani. Huu ni usemi wa Kiswahili ambao utausikia kila mara katika maisha ya kila siku. Usemi huu una maana kwamba maisha ni popote, kinachotakiwa ni kujituma kwa moyo na kutafuta mafanikio kupitia shughuli zozote halali.

Hivyo ndivyo ilivyo kwa Habib Ally (46), maarufu Tupatupa, mkazi wa Sinza kwa Mwaibula jijini Dar es Salaam ambaye anajishughulisha na biashara ya kuuza mbogamboga.

Anasema kuwa aliianza biashara hiyo mwaka 1985, wakati huo akiwa na umri wa miaka 20 ambapo alijikuta akifanya biashara hiyo baada ya wazazi wake kufariki dunia na hivyo kumwacha yatima.

Anasema kuwa awali alikuwa akifanya kazi za ufundi kwa kusaidia mafundi wakati wa kujenga, kuchanganya saruji, kufyatua matofali na kazi nyingie za kusaidia kujikimu ambazo zilimwingizia kipato.

Anasema kuwa kutokana na kutokuwa na elimu hata ya shule ya msingi ugumu wa maisha ulimwandama kwa kuwa kazi hiyo ya ufundi ilukuwa ngumu na upatikanaji wake ulikuwa wa shida na hivyo kulazimika kukimbilia jijini Dar es Salaam.

“Hata nilipohamia Dar es Salaam niliendelea na kazi yangu hiyo ya kufyatua matofali kwa zaidi ya miaka miwili hadi hapo nilipokutana na rafiki yangu ambaye alinishauri kuachana na kazi za ujenzi na kunishawishi nijiunge naye kulima mbogamboga.

“Nilianza kwa kulima aina mbalimbali za mboga katika Bonde la Chakula Bora Tandale, Uzuri ambapo wafanyabiashara wa mbogamboga walikuja kununua kwangu kwa bei ya jumla na wao kuuza mitaani na kwenye masoko mbalimbali,” anaeleza.

Aidha, anaongeza kuwa kazi ya kilimo cha mboga ilikuwa ngumu kwake, lakini kutokana na shida zilizokuwa zinamkabili kimaisha kwa wakati huo hakuwa na jinsi na kujikaza kwa kuongeza bidii ambapo hata hivyo baadaye aliizoea.

Anasema kuwa wakati huo alikutana na chanamoto nyingi ikiwa ni pamoja na kupata kiasi kidogo cha fedha ukilinganisha na kazi kubwa aliyoifanya kunzia katika maandalizi ya bustani hadi kuvuna.

“Ni kweli kazi yangu niliifanya kwa moyo mmoja, lakini kwa upande fulani iliniumiza sana kwa kuwa kazi ya kulima siyo lelemama, sikuwa na muda wa kupumuzika na hiyo ilikuwa ni jambo baya kwangu,” anasema.

Anaongeza kuwa baada ya kuoa, mke wake alimshauri kuachana na kilimo badala yake aanze kununua na kuuza kwani wafanyabiashara wengi wa mboga mboga waliokuwa wakifanya hivyo walipata faida kubwa kuliko hata wakulima wenyewe.

“Nilianza kununua kwa bei ya jumla na kuuza kwa kutembeza mitaani na tenga langu kichwani, mafanikio nikaanza kuyaona tena nilipata faida tofauti na wakati nilikuwa nalima, wakati huu nilipata hata muda wa kupumzika kwa kuwa biashara yenyewe nilifanya asubuhi,” anasema.

Anasema kuwa biashara hiyo inamlipa kwa kuwa hununua tuta zima la mboga mboga kwa kiasi cha Sh 60,000 na kupata zaidi ya Sh 100,000, jambo ambalo kwake humpatia faida kubwa karibu mara mbili ya bei ya manunuzi.

Akizungumzia ushindani katika biashara hiyo hasa kwa kuwa watu wengi wanafanya biashara kama hiyo, Tupatupa anasema kuwa ubunifu mkubwa alionao katika kuifanya biashara yake ndiyo ambao unawafanya wateja wakimbilie kwake.

“Kuna mambo mengi ambayo nayafanya ili kuwavutia wateja wangu, ikiwa ni pamoja na kuwaongeza mboga kila wanaponunua kwangu, lakini pia lugha nzuri ambayo naitumia huwafanya wazidi kunifagilia na kuona kuwa nawajali na kuwathamini,” anasema.

Pia, anasema kuwa aliamua kubuni sauti mahsusi kwa kuwatangazia wateja wake ili watambue wakati akipita katika mitaa yao, maneno ambayo yamekuwa yakitumiwa pia na watoto wadogo na kumwongeza umaarufu.

Maneno hayo ambayo huyaimba kwa mbwembwe ni kama, “ Unasema…unasema…eeeh nikungoje, mboga zote ziiipoooo, shangazi wangu mwenyewe, hata kinababa, kinadada, zoote zipo, unasema unasema, nikungoje”.

Anasema kuwa mbali na kutumia sanaa hiyo pia usafi wa mboga zake kutokana na kuziosha na maji safi ni nyenzo kubwa ya kuwapata wateja na kuwafanya kila siku waendelee kununua mboga kwake.

Anasema kuwa mboga ambazo huuza ni pamoja na majani ya kunde, mchicha, maboga, spinachi, sukuma wiki, kisamvu, tembele figiri na nyinginezo nyingi.

Mafanikio

Aidha, anasema kuwa kupitia kazi yake hiyo amefanikiwa kujenga nyumba maeneo ya Uzuri Sinza ambapo pamoja na jitihada zake katika biashara sifa nyingi anazipeleka kwa mkewe kwa ushauri wake mzuri ambao umesaidia kumfikisha katika malengo yake.

“Namshukuru sana mwenyezi Mungu kwa kunipatia mke mwenye busara ambaye kwa kweli amenishauri mambo mengi mema ambayo yamefanikisha mimi kufika hapa, tumepita shida nyingi za hapa na pale, lakini Mungu ametusaidia kufika hapa,” anasema

Mafanikio mengine ni kwamba sasa anafanya biashara yake hiyo ya mboga mboga kwa kutembeza mitaani kwa kutumia baiskeli tofauti na awali ambapo alijitishwa tenga kichwani na kutembea kwa miguu katika mitaa yote ya Sinza.

“ Kwa siku natengeneza zaidi ya Sh15,000, si haba, inatosha kwa matumizi yangu ya kila siku pamoja na familia.
Anaongeza, kuwa kazi yake imemwezesha kusomesha watoto wake ambapo mtoto wake mmoja yuko sekondari wakati wawili wanasoma katika shule ya msingi huku mmoja akiwa ameolewa na ana familia yake.

Hata hivyo, anasema kuwa wafanyabisra wengi wa mbogamboga hawana elimu ya kutosha juu ya namna ya kutoa huduma kwa wateja wao na kuyaomba mashirika mbalimbali kuwasaidia kutoa elimu hiyo ili kuwaimarishia uwezo wao katika biashra.

“Tunaona wafanyabiashara wengine wanapewa mafunzo ya ujasiriamali, lakini sisi tukiachwa, hii si nzuri kwa kuwa hata sisi tunahitaji kupata elimu hiyo ili kuboresha uwezo wa kufanya biashra zetu” anasema

No comments:

Website counter