Thursday, May 5, 2011

JE HII NI HALALI KUWADHULUMU 'WAHUDUMU' WETU WA NDANI...



WATU wengi majumbani mwetu tunakaa na wasaidizi wa kazi ambao tumewapa majukumu ya kutusaidia kazi na shughuli mbalimbali wakati tukiwa katika mihangaiko yetu ya kila siku kutafuta mapato ya kujikimu.

Wasaidizi hao tumezoea kuwaita 'MAHAUSIGELI' au 'MAHAUSIBOI' ambao wamekuwa wakibaki na nyumba zetu, wakilea watoto wetu na kutupikia wakati wenye nyumba tukiwa hatupo.

Watu hawa tunawapa dhamana kubwa na tunawaamini sana ndio maana hatusiti au hatuogopi kuwaachia himaya zetu watulindie, tena mara nyingine tunasafiri na kwenda mbali, tukiwaachia watoto wetu na vitu vya thamani vingi tu.

Hata hivyo kilichonisukuma hasa kuzungumzia kundi hili la watu ni kutokana na tabia ya baadhi ya waajiri ambao wamekuwa hawathamini kazi za watu hao, hivyo kuwafanyia vitendo au dhuluma kwa kuwalaghai na kutowalipa fedha zao kama walivyokubaliana.

Kuna hii tabia ya baadhi ya waajiri kutowalipa watumishi hawa fedha mwisho wa mwezi kwa madai kuwa wanawahifadhia, lakini ikifika wakati wenyewe wanataka fedha zao kwa ajili ya mahitaji mbalimbali lugha inabadilika.

Hii si tabia nzuri hata hidogo, mtu anajitoa anakufanyia kazi za nyumbani halafu humlipi chochote kwa kumhadaa unamhifadhia fedha lakini siku anapotaka fedha zake unamgeuka ukimpa sababu kibao!

Kilichonisukuma kuandika habari hii ni tukio la hivi karibu la mama mmoja ninayemfahamu ambaye amekaa na hausigeli wake karibu mwaka sasa na anamdai mwajiri wake karibu Sh 300, 000 lakini alipomwambia nataka kwenda kusalimia nyumbani hapo ndipo habari ilibadilika.

Mama huyo mwajiri bila aibu alimwambia mtumishi wake, ‘kwani si unanidai Sh 100,000 tu?” dada akabaki na mshangao na kumjibu mwajiri wake, “hapana mama mbona ni Sh 300,000.” Mwajiri akahamaki “laki tatu!” Eti mama mwajiri anajifanya hizo 200,000 hazikumbuki na ana kumbuka 100,000 na kibaya zaidi ili kukwepa kulipa fedha za hausigeli wake akaanza kumuorodheshea nguo alizowahi kumnunulia, vyombo alivyowahi kuvunja na vitu alivyopoteza binti wa watu akabaki ametoa macho haelewi.

Wewe mwajiri mbona wakati wa kuajiri hausigeli au hausiboi wako hamkukubaliana au kuingia mkataba kama atavunja kitu au kupoteza au ukimnunulia kitu basi mtakatana kwenye mshahara mwisho wa mwezi.

Kitendo cha mwajiri wa namna hiyo sio haki hata kidogo, kama una masharti yako ya namna hiyo kwa nini msikubaliane tangu mwanzo kabla kazi hazijaanza ili mwisho msijegombana bila sababu.

Lakini pia ni fundisho ama tahadhari kwa watumishi kama hawa kutomuamini sana mwajiri akuwekee fedha kwa sababu huyo ni mwanadamu, huenda kweli akawa anakuhifadhia lakini akipata shida na fedha anazo unadhani atashindwa kuzitumia? Inahitaji moyo wa ujasiri usiokuwa na tamaa!

Kama ni mwajiri mwenye mapenzi mema basi muombe hausigeli au hausiboi wako kuwa unaazima fedha zake kwa dharura utarudisha, lakini sio kuzitumia halafu siku ukidaiwa unabadilika na kuwa mkali au unakataa madeni haipendezi.

Ikiwezekana basi ni vizuri mwajiri na mfanyakazi mkawekeana mkataba au mkaingia makubaliano vizuri ili msijekugeukana ikifika wakati wa kudaiana mshahara na masuala ya kuwekeana ama kukopana yasiendekezwe ili msinyimane haki huku kila mmoja akimheshimu mwenzake kwa kile anachomfanyia.

No comments:

Website counter