Monday, May 23, 2011

HUYU NDIE PARIS HILTON NA 'VITUKO' VYAKE...


Paris Hilton
KAMA kuna namna unaweza kumwelezea Paris Hilton, basi ni tajiri asiyeona haya.
Hii inatokana na ukweli kwamba, Paris hugonga vichwa vya habari duniani kwa habari nzuri na zile mbaya.
Hana kipaji chochote cha maana, pengine kufuatiliwa kwake na paparazzi na utajiri wa famili yake umemsaidia kujijengea jina duniani.

Pamoja na kutoka familia ya kitajiri, lakini Paris amefanya kazi nyingi zinazofanywa na watu wa kawaida kabisa.

Paris, ambaye alizaliwa Februari 17, 1981 nchini Marekani, ni mtoto wa kike wa familia ya Hilton, inayomiliki mahoteli mbalimbali duniani maarufu yanayokwenda kwa jina la Hilton.
Ni kati ya warithi wanaotambuliwa wa mali za familia hiyo.
Ni kitukuu cha Conrad Hilton, ambaye ni muasisi wa hoteli za Hilton ambazo alianza kujenga mwaka 1943.

Familia hiyo inamiliki hoteli 540 katika nchi zaidi ya 76 duniani.
Pamoja na kutoka katika familia iliyosheheni fedha, hajabakia nyuma kusubiri fedha za nyumbani bali ana shughuli nyingi anazofanya.

Mambo anayofanya ni pamoja na utangazaji wa televisheni, mwanamitindo, mwanamuziki, mtunzi wa vitabu, mbunifu wa mavazi na muigizaji.

Amefanya tamthiliya ya televisheni ya Simple Life, ambayo aliigiza na rafiki yake Nicole Richie.
Katika kipindi hicho wanafanya shughuli mbalimbali za jamii ikiwamo kusafisha mji.

Hilton ana ubia na kampuni ya Japan ya kutengeneza pochi za wanawake ya Samantha Thavasa na pia anatengeneza vito akishirikiana na mtandao wa Amazon.com.
Pia Hilton anabuni manukato akishirikiana na kampuni ya Parlux Fragrances.

Hilton pia alitoa manukato mengine Oktoba 2007, yanayoitwa Can Can.
Ana mkataba na Kampuni ya Antebi wa kutengeneza viatu. Pia ana kampuni ya kutengeneza nguo.
Hilton ana klabu za usiku anazoshirikiana kuziendesha na Fred Khalilian.

Hata hivyo, kwa upande wa pili wa shilingi, maisha ya Hilton ni utata mtupu.
Anatajwa kuwahi kuwa na uhusiano wa mapenzi na wanaume kadhaa akiwemo mwanasoka nyota wa Real Madrid, Cristiano Ronaldo.
Hata hivyo, alizua gumzo zaidi baada ya mpenzi wake wa zamani Rick Salomon kuamua kuvujisha mkanda wao wa video wakifanya mapenzi kwenye vyombo vya habari.
Pia amekumbwa na mikasa kadhaa iliyomfanya wakati fulani kutupwa ndani, kwa mfano kukamatwa na bangi nchini Marekani na Afrika Kusini mwaka jana wakati wa Fainali za Kombe la Dunia.
Mali za Paris zinakadiriwa kufikia Dola 50 milioni (Sh. 75 bilioni) ikiwa zaidi ni urithi kutoka katika kampuni za Hilton.
Kutokana na shughuli zake mbalimbali mapato ya mwaka ya Paris ni kiasi cha Dola 16 milioni (Sh. 24 bilioni).
Hilton ana nyumba tatu, mbili zikiwa jijini New York na moja iko katika jiji la Los Angeles.
Nyumba yake ya Los Angeles ndiyo kubwa zaidi ikiwa na thamani ya Dola 5.9 milioni (Sh. 8.85 bilioni).
Nyumba hiyo iliyojengwa mwaka 1991, ina vyumba vitano vya kulala, sehemu tano za kuogea na chumba maalum cha mazoezi.
Pia Hilton ana ndege yake binafsi, ambayo huitumia kwa safari mbalimbali duniani. Pia ana boti yake.
Ana magari kadhaa aina ya Lexus, Bentley, Rolls Royce, Mercedes Benz, Ferrari 360 Spyder na Aston Martin.
Hilton ana mchumba, ambaye ni Cy Waits, ambaye anamiliki klabu za usiku jijini Las Vegas.

1 comment:

Anonymous said...

ana gonolia huyu mtoto wametangaza mapaparazi. hajui kujisopu ikulu.ana visaa huyu balaaa tupu

Website counter