Mpango wa Mwasapila kuhama Samunge | Send to a friend |
|
VIONGOZI wa mila wa kabila la Wasonjo au Batemi wanaojulikana kama Wanamiji, wamegomea mpango wa Mchungaji Mstaafu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Ambilikile Mwasapila kuhamisha tiba ya magonjwa sugu kutoka eneo inapotolewa hivi sasa kwenda katika eneo Mtalija. Kiongozi Mkuu wa Wanamiji, Peter Dudui, aliliambia Mwananchi kijijini Samunge kuwa wanamshauri mchungaji Mwasapila kutohama kwani eneo la Mtalija ni la kimila ambalo lilikuwa likitumika kama maziko ya watu wasiokuwa na ndugu pamoja na watoto. "Lile eneo ni la kimila na halina maji pia lipo mpakani mwa kijiji chetu na kijiji kingine cha Digodigo, hivyo akihamia huko kuna uwezekano wa kuzuka mgogoro wa mipaka na kijiji hicho, sisi kama wanamiji, hatupendelei huduma ya mchungaji ipelekwe kule," alisema Dudui. Dudui alisema, wapo tayari kumuongezea eneo Mchungaji Mwasapila katika sehemu anayotolea tiba yake hivi sasa, hata kama watalazimika kuhamisha baadhi ya wakazi wa eneo hilo. Viongozi hao wa kabila la Kisonjo au Batemi, wana nguvu kubwa za kimamlaka na heshima katika eneo zima la Sonjo na uongozi wao umekuwa ukitokana na kurithiana katika koo maalumu ambazo ndizo zimekuwa zikitoa viongozi wanaounda jopo la Wanamiji. Mchungaji Mwasapila akizungumza katika mahojiano maalumu na timu ya waandishi wa mwananchi walioweka kambi Kijiji cha Samunge, alisema ameoteshwa na Mungu kuhamia eneo hilo la Mtalija kutolea huduma zake kutokana na ufinyu wa nafasi katika eneo la sasa. Alisema eneo hilo, ni kubwa na linaweza kurahisisha sana utolewaji wa huduma kwa watu wa mataifa mbalimbali na pia historia yake jinsi lilivyokuwa linatumika, anaamini Mungu anataka kulibadili. "Mtalija ni eneo ambalo wenyeji walitumia kutupa wafu kwa sababu hawakuwa na utamaduni wa kuzika enzi za zamani, lakini sasa Mungu anataka liwe eneo la ufufuo wa watu waliokata tamaa kutokana na maradhi mbali mbali," alisema Mwasapila. Mchungaji Mwasapila aliwataka watu, wanaotaka kupanua maeneo yake ya kutoa huduma , kuweka miundombinu katika eneo hilo la Mtajila kwani mahali alipo ni pa muda tu. "Katika eneo hili pia wanaweza kusaidia kuweka miundombinu ila ni ya muda tu, kule ndipo Mungu amenionyesha kwenda, ila nasubiri tangazo lake ili niweze kuanza kuhamia huko," alisema Mwasapila. Eneo hilo la Mtalija lipo takriban kilometa tatu kutoka Samunge anapotolea huduma sasa Mchungaji Mwasapila. Eneo hilo ni dogo na limekuwa likisababisha msongamano wa magari kutokana na kuwa pembezoni mwa barabara. Babu aonya Siku chache baada ya kutokea malalamiko ya wagonjwa na madereva wa magari kupata urasimu wa kupata vibali na pia kuombwa rushwa, Mchungaji Mwasapila amewaonya watendaji hao kuacha mara moja kujinufaisha nawagonjwa. Akizungumza na timu ya waandishi wa Mwananchi Kijiji cha Samunge kwa niaba ya Mchungaji Mwasapila, Msaidizi wa mchungaji huyo, Fredrick Nisajile alisema Mwasapila amesikitishwa na taarifa za kuwepo kwa vitendo hivyo na kuonya kuwa kama taarifa hizo ni za kweli wahusika waache mara moja. "Mchungaji anasema anasikitishwa sana na taarifa hizo kwamba maeneo ya kutolea vibali yamegeuzwa kuwa sehemu ya watu kujipatia rushwa isivyo halali, utaratibu tuliouweka ulikuwa ni wa kuwasaidia wagonjwa na si kuwaumiza," alisema Nisajile. Nisajile alisema pia kuwa wanasikitishwa na malori kuendelea kutumika kuwasafirisha watu wanaokwenda Samunge kunywa dawa, hali inayodhalilisha utu wa watumiaji wa magari ya aina hiyo.Alisema ni vyema wasimamizi wa maelekezo ya Serikali wakasimamia suala hilo ili kuepusha watu dhidi ya unyanyasaji wanaoupata, pia ajali zinazotokana na matumizi ya magari ya aina hiyo. Mkono atimiza ahadi Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini, Nimrod Mkono, juzi alitimiza ahadi yake ya kutoa maturubai katika eneo analotolea huduma Mchungaji Mwasapila. Mkono akiwa ameongozana na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Mahusiano ya Jamii), Stephen Wassira, mara baada ya kupata tiba. |
No comments:
Post a Comment