Sunday, March 20, 2011

WEE KAKA DEDE FANYA KAZI ACHA KUJIFANANANISHA NA 'BABU WA LOLIONDO BANAA...'

Image
Shaaban Dede ‘Super Motisha’


Habari zinazosomwa zaidi:

MWIMBAJI mkongwe Shaaban Dede ‘Super Motisha’ ametangaza rasmi kujiunga na bendi ya Msondo Ngoma na kutamba kuwa bendi hiyo ni nyumbani kwake.

Kutokana na hali hiyo amewaahidi raha mashabiki wake na kwamba amerudi kuongeza furaha huku akijifananisha na Babu wa Loliondo Mchungaji mstaafu Ambilikile Mwaisapile.

Dede ametambushwa rasmi katika bendi hiyo kwa kuanza mazoezi na wenzake ikiwa imesalia siku moja kabla ya kufanyika mpambano wa Nani Zaidi kati ya bendi kongwe za muziki wa dansi hapa nchini Msondo Ngoma na Mlimani Park Orchestra utakaofanyika kesho ukumbi wa Diamond Jubilee, Dar es Salaam.

Alisema kuhamia kwake Msondo akitokea Mlimani ni kwenda kupona na kuponyesha watu katika burudani.

Mchungaji Mwaisapile amekuwa gumzo siku za karibuni akidaiwa kutibu magonjwa sugu, hivyo maelfu ya watu wamekuwa wakimiminika kwenda kupata kikombe cha dawa yake.

“Nimeamua kurudi nyumbani kwa mapenzi yangu binafsi na mnaponiuliza kwanini nimerudi hebu jiulizeni watu wanakwenda Loliondo kufanya nini?

“Hapa (Msondo) ni Loliondo nimekuja hapa kupona na kuponyesha watu katika burudani kwa hiyo wapenzi wa Msondo wategemee furaha zaidi.

“Mkataa kwao ni mtumwa ,nimerudi Msondo ambako ni nyumbani na nitakuwa hapa milele,”alisema Dede, ambapo alipoulizwa kuhusiana na suala la mkataba na bendi hiyo alijibu amerudi nyumbani kwani bendi hiyo alipata kuimbia miaka ya nyuma.

Naye msemaji wa bendi ya Msondo, Rajabu Mhamila ‘Super D’ alibainisha kuwa nyota huyo ambaye ameng’ara katika muziki wa dansi kwa muda mrefu kutokana na tungo zake mahiri atatambulishwa kesho katika mpambano wa Nani Zaidi.

Alieleza kuwa kurudi kwa nyota huyo katika bendi hiyo kutaharakisha kazi ya bendi hiyo kukamilisha albamu yake mpya ambayo tayari ina nyimbo nne za Lipi Jema, Kwa Mjomba Hakuna Urithi, Dawa ya Deni Kulipa na Baba Kibe.

Alisema Dede tayari ana nyimbo mbili ambazo zitajumuishwa kwenye albamu hiyo na kuifanya iwe na jumla ya nyimbo sita , nyimbo hizo ni Suluhu na wimbo mwingine ambao unazungumzia athari na ubaya wa utumiaji dawa za kulevya bado hajapewa jina.

Dede amekwishaanza mazoezi na wanamuziki wenzake.

1 comment:

SENETA WA MSONDO said...

Mwenda kwao si mtoro karibu,karibu kakangu SUPER MOTISHA SHABAN DEDE a.k.a.kikombe cha babu,Msondo ni nyumbani kwako tunakukaribisha sote,kariibu.

Website counter