|  Wanafunzi  wa darasa la pili na tatu wa shule ya Msingi Magwalasi katika Kata ya  Rujewa, wilayani Mbarali, mkoani Mbeya wakiwa darasani wakiendelea na  masomo kutokana na uhaba wa vyumba vya madarasa shule hapo imewalazimu  chumba kimoja kutumiwa na wanafunzi wa madarasa mawili kwa kila darasa  kugeukia upande wake kama walivyokutwa na mpigapicha wetu jana. Picha na  Brandy NelsonUHABA wa vyumba  vya madarasa umewalazimu wanafunzi wa madarasa tofauti katika Shule ya  Msingi Magwalasi iliyoko Kata ya Rujewa wilayani Mbarali, Mkoa wa Mbeya  kusoma katika chumba kimoja kwa kugeuziana migongo.
 Waandishi wa  habari walifika hapo jana na kukuta shule hiyo yenye wanafunzi 269 na  walimu saba wa kuanzia chekechekea, darasa la kwanza hadi la saba ikiwa  na vyumba vinne pekee vya madarasa.
 
 Mwalimu Mkuu wa shule hiyo,  Jonathan Chengula aliwaambia waandishi wa habari kuwa katika shule hiyo  iliyoanza na kusajiliwa mwaka 2003, wanafunzi wa darasa la kwanza  wanasoma chumba kimoja kwa wakati mmoja na wale wa chekechea, darasa la  pili wanasoma pamoja na wenzao wa darasa la tatu, la sita na la tano,  huku wale wa darasa la saba wakitumia chumba kimoja na wa darasa la nne.
 
 “Tatizo kubwa ambalo linatusumbua katika shule yetu ni upungufu  wa madarasa. Tuna madarasa manne tu hivyo imetulazimu kuweka mbao za  kufundishia mbili katika chumba kimoja ili madarasa mawili yaweze  kutumia kwa wakati mmoja,” alisema.
 
 Kwa mujibu wa mwalimu mkuu  huyo, ili kukabiliana na upungufu huo wa madarasa na kutokana na  mazingira ya shule hiyo, ndiyo maana wameramua wanafunzi wa madarasa  mawili tofauti wasome katika chumba kimoja kwa kugeuziana migongo kwa  maana ya kuwa wengine wanageukia upande wa kulia na wengine kushoto.
 
 “Kama  mnavyowaona hawa waliogeukia huko ni darasa la saba na hawa wengine ni  darasa la nne na katika darasa hili jingine wanasoma darasa la  pili na  tatu ndivyo tunavyo kwenda," alisema.Alisema kuwa mwalimu wa darasa la  saba anapoingia kufundisha, wa darasa la nne anasubiri mwenzake amalize  huku wanafunzi hao wa darasa la nne wakiwemo humo humo ndani  wakisikiliza wale wa darasa la saba wanavyofundishwa.
 
 Alisema  wakati mwingine walimu huamua kuwatoa nje na kuwaweka chini ya mti kama  umefika wakati wa kusoma kitabu cha Kiswahili ili wasome wakiwa nje na  wengine waendelee na masomo.
 Mwalimu aliyekuwa darasani  akifundisha, Shufaa Ramadhani alisema mazingira hayo ya ufundishaji ni  magumu kwani kuna athari kubwa kwa  wanafunzi na upande wa mwalimu kwani  kufundisha wote kwa pamoja pia ni vigumu.
 Alisema kuwa  utaratibu huo unawaathiri watoto kisaikolojia kwani kuna uwezekano wa  kusahau yale ambayo wamefundishwa na mwalimu wao na badala yake kusikia  ya upande wa pili ambayo ni masomo ya darasa jingine ambalo tayari  walishayapitia au bado hawajapitia.
 
 Mwalimu Shufaa alisema  walimu wanaathirika kwa kupoteza vipindi vingine kwa mujibu wa uandaaji  wa masomo na vipindi kwani inamlazimu asubiri mwenzake amalize  kufundisha na ndipo aingie na kufundisha somo lake.
 
 Mkurugenzi  wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali, George Kagomba hakupatikana  kuzungumzia tatizo hilo na alipotafutwa kwa simu alijibu kuwa yuko  kwenye kikao cha maandalizi ya Mbio za Mwenge.
 
 Mkurugenzi huyo  aliwataka waandishi kwenda kwa Ofisa Elimu wa Wilaya ya Mbarali. Hata  hivyo, aliyekuwa akikaimu ofisi hiyo hakuwepo. Ofisa elimu wa Wilaya  alikuwa amesafiri kikazi.
 
 | 
1 comment:
Haihitaji mtu makini kuhoji sababu ya matokeo ya darasa saba au kitado cha nne kuwa mabaya kitaifa. Sababu hizi zipo wazi kabisa angalia hili la kuchangia darasa. Halafu tunakadhani mambo yasiyo na tija kabisa, sasa mwenge una nini badala ya kutatua matatizo yaliyopo katika jamii? Na ndo maana Dr.Slaa(PhD.) alisema yeye angeuweka mwenge kwenye jumba la makumbusho. Mbali na hilo semina nyingi zisizokuwa na manufaa kwa jamii ni kazi bure, ona ambao wanaotakiwa kutolea majibu ya hilo tatizo wote wamesafiri kikazi. Kweli bongo tambarale. Kinyaiya usije ukashangaa siku moja ukisikia huyo mwalimu mkuu amepewa uhamisho wa kwenda kijijini ndani zaidi kwa sababu ameiaibisha serikali(kwa mtazamo wa viongozi we2)kwa kusema hayo yanaotokea katika shule yake.
Post a Comment