Thursday, March 31, 2011

OOHOOOO 'BABU' NINI SASAA...

Babu ataka miundombinu atakakohamia Send to a friend


Mchungaji Ambilikile Masapila (kulia) akimuombea mmoja wa wagonjwa toka nje ambaye alifikishwa jana na familia yake katika Kijiji cha Samunge, Loliondo, mkoani Arusha kupata tiba. Picha na Fidelis Felix


MCHUNGAJI Ambilikile Masapila wa Loliondo ameitaka Serikali na taasisi zinazojipanga kuboresha huduma za miundombinu katika Kijiji cha Samunge anakotolea tiba ya magonjwa sugu, kuelekeza nguvu hizo katika Bonde la Mtalija kwa kuwa atahamia huko hivi karibuni.

Akizungumza jana, Mchungaji huyo alisema anasubiri maelekezo ya Mungu kujua lini atahama Samunge lakini akasisitiza kwamba hana muda mrefu kwa kuwa eneo hilo ni finyu na halikidhi matakwa ya wingi wa watu wanaofika kupata tiba hiyo.

Alisema tayari Mungu amemwonyesha eneo jingine mbadala atakalohamia ijapokuwa anasubiri maelekezo ya lini anatakiwa kwenda huko na utaratibu utakaotumika kuhamisha makazi ya tiba hiyo kutoka eneo alipo sasa.
"Hili eneo linakuwa finyu sasa kutokana na wingi wa watu wanaofika kupata tiba. Lazima tuhame na Mungu ameshanionyesha eneo ambalo huduma hii itahamia, ila nasubiri tangazo lake kujua ni lini nitahama,"alisema Mchungaji huyo.

Kwa mujibu wa Mchungaji huyo, eneo analokusudia kuhamishia tiba hiyo ambayo imekuwa ikiwavuta maelfu ya watu kutoka ndani na nje ya nchi, lipo nyuma ya kilima kiitwacho Makazi ambacho ni miongoni mwa vilima kadhaa vinavyozunguka Kijiji cha Samunge.

Bonde la Mtalija ambalo lipo umbali wa kilometa kama mbili kutoka eneo anapotolea tiba hivi sasa, halijawahi kuwa makazi ya watu na zamani lilikuwa likitumiwa na wenyeji wa eneo la Sonjo kutupa maiti za watu waliokuwa wakifariki dunia kwa sababu mbalimbali.

"Hapo kale wenyeji wa eneo hili hawakuwa na utamaduni wa kufanya maziko ya wafu, hivyo watu walipokufa walitupwa kwenye bonde hili," alisema.

Akijibu swali kwamba ni nini maoni yake kuhusu tiba hiyo kuhamishiwa eneo la wafu, Mchungaji Masapila alijibu kwa kifupi akisema; "Lilikuwa ni eneo la wafu, lakini Mungu anataka sasa pawe ni mahali pa ufufuo."

Hali katika eneo la sasa
Eneo la sasa linalotumiwa na Mchungaji Masapila katika Kijiji cha Samunge ni finyu ikilinganishwa na idadi ya watu wanaofika kupata tiba hiyo, hali inayosababisha hata udhibiti wa usafi kuwa mgumu.

Watu wanaofika kwa magari wanapewa dawa kwa kupelekewa kwenye magari yao. Hali hiyo inatokana na ufinyu wa nafasi kwani iwapo wataruhusiwa kushuka kwenye magari yao, hali inaweza kuwa mbaya zaidi kwani wapo wengine wanaopewa dawa nyumbani kwa Mchungaji huyo ambao hawakufika kwa magari.

Mbali na wanaofika Samunge wakiwa kwenye magari, Mwananchi mara kadhaa limeshuhudia makundi ya watu, wengi wakiwa wanawake na watoto wakitumia njia za mkato, za porini na kwenye vichaka kwenda kijijini Samunge kupata tiba hiyo.

"Tunatembea kwa miguu kutoka huko makwetu hadi kwa babu kunywa dawa na kutoka huko hadi hapa ni saa tano wakati wa kwenda na saa sita kurudi. Tunatumia saa sita kurudi kwa sababu ni kupanda milima," alisema mkazi wa Kijiji cha Sale, Kibasisi Ole Saitoti.

Kundi hili la wenyeji pia linapatiwa dawa katika eneo maalumu lililotengwa pembezoni mwa makazi ya Mchungaji Masapila, sambamba na wale walioko
kwenye msururu wa magari.

Dk Huvisa na fagio kwa babu
Hali ya uchafu wa mazingira ilimlazimu Waziri wa nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), Dk Terezya Huvisa kurejea Samunge kwa mara ya pili, safari hii kuzindua kampeni ya usafi.

Katika uzinduzi huo waziri huyo aliwatupia lawama watendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro kwa kile alichokiita uzembe unaofanya hali katika eneo hilo iendelee kuwa mbaya.

"Kuna mambo mengine hayahitaji vikao. Kwa mfano, kununua chelewa na vifaa vya kuwekea takataka, haya nayo tusubiri hadi vikao wakati tunaona hali ilivyo? Mimi nadhani tunahitaji kuwa na watu wanaochukua hatua za haraka pale tunaposhuhudia hali inakuwa mbaya kama ilivyo hapa," alisema Dk Huvisa. Dk Huvisa ambaye alishiriki katika kusafisha eneo linalozunguka makazi ya mchungaji huyo, alisema kwa kuwa anashughulikia zaidi sera ya mazingira,
atawasiliana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi), George Mkuchika kuhusu uzembe unaofanywa na Halmashauri ya Ngorongoro hasa kwa kushindwa kuchukua hatua za kuweka mazingira katika hali ya usafi.

"Kwa bahati nzuri ninavyofahamu, fedha zipo kwani wanakusanya mapato kutokana na magari yanayoingizwa hapa. Sasa sioni tatizo ni nini, nitamwambia Waziri Mkuchika kuhusu hawa watu wake kwa sababu yeye ndiye mwenye dhamana," alisema.

Mbali na kutapakaa kwa takataka za aina mbalimbali katika Kijiji cha Samunge, nyingi zikiwa ni chupa tupu za maji na mifuko ya plastiki, wakazi wa kijiji hicho na vijiji vya jirani wanalalamikia watu wanaokwenda kunywa dawa kujisadia ovyo, hali inayohatarisha afya zao.

Hali inaelezwa kuwa mbaya pembezoni mwa barabara ya kuingilia Samunge kwani katika umbali wa zaidi ya kilometa zaidi ya 30 za msururu wa magari, hakuna huduma za vyoo wala maji, hivyo watu wamekuwa wakijisaidia vichakani.

"Labda tuombe mvua zisinyeshe kwani huko kote ni vinyesi tu, lazima wenyeji wa hapa wataathirika sana. Watu wanajisaidia ovyo, hakuna vyoo vya kudumu wala vya muda," alisema mkazi wa Morogoro, Ramadhan Libenanga.

Vyoo vyachimbwa
Hata hivyo, tatizo hilo la vyoo limeanza kupatiwa ufumbuzi baada ya Shirika la Mazingira na Nishati (Solar Oven Society Africa) kuanza kuchimba vyoo vya muda pembezoni mwa barabara kuu ya kuingia Samunge jana.
Mkurugenzi wa Shirika hilo kanda ya Afrika, Profesa Solomon Mwenda aliliambia Mwananchi kwamba tayari vifaa vya kutekeleza mpango huo vimeishafika katika eneo la njiapanda ya Samunge - Arusha na kwamba idadi ya vyoo vitakavyochimbwa ni 24, vikiwa ni vyoo vinne ndani ya umbali wa kilometa moja.

Barabara Samunge zaombewa Sh400 milioni
BARAZA la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro mkoani Arusha, limeomba Sh400 milioni kutoka Serikali Kuu ili kukarabati na kufungua njia zaidi za kwenda Samunge. Mwenyekiti wa Halmashauri ya Ngorongoro, Elias Ngorisa alisema juzi kijijini Samunge kwamba hiyo inatokana na hali ya miundombinu kufika Samunge kuwa mbaya, hivyo kuhitaji ukarabati haraka.

"Sisi kama halmashauri fedha za routine maintanance (matengenezo ya kawaida), tumetenga lakini bado hazitoshi na tumeomba Serikali Kuu itupatie Sh400 milioni mapema iwezekanavyo ili kubadilisha hali hii," alisema Ngorisa.
Alisema miongoni mwa barabara ambazo zinatarajiwa kutengenezwa ni pamoja na ya Mgongomageri, Tinaga, Msusu, Kigongoni wilayani Monduli kupitia Ngaresero hadi Samunge, Serengeti, Maaloni, Malambo kupitia Kijiji cha Sale hadi Samunge.

Barabara ya Vigogo
Wakati Halmashauri ya Ngorongoro ikijipanga kuboresha barabara za kwenda Samunge, baadhi ya wakazi wa Kijiji cha Mgongomageri inakopita moja ya barabara hizo wamesema Serikali inapaswa kujifunza kuwaunga mkono wananchi wanapokuwa wakitekeleza miradi ya maendeleo.

Mmoja wa wakazi hao, Boniphace Nambena alisema Barabara ya Mgongomageri ambayo inajulikana kama VIP ilitengenezwa na kikosi cha mgambo mwaka 2002 na kwamba tangu wakati huo, hakuna jitihada ambazo zimewahi kufanywa kuiboresha.

"Hii barabara tulijenga kwa miezi sita, hapa hapakuwa na barabara kabisa.Sasa kipindi kile tusingejitolea kujenga leo ingekuwaje? Viongozi wetu wajifunze kutuunga mkono maana leo VIP (watu mashuhuri) wanapita hapa ili kwenda kwa Babu lakini
hawajawahi kuikumbuka barabara hii kwenye bajeti zao," alisema Nambena.

Ushuru wa magari juu
Serikali imeongeza kodi ya magari yanayokwenda Samunge. Ngorisa alisema kodi ambayo itaanza kulipwa kuanzia kesho ni Sh5000 kwa kila gari litakalokuwa likiingia kijijini hapo. Mwenyekiti huyo, alisema katika fedha hizo, Serikali kuu itakuwa ikichukua Sh2,000 na halmashauri Sh3,000.

"Kutokana na kuanza utaratibu wa magari kuja kutoka kila kanda, itabidi uwepo uratibu mzuri na hivyo tuna imani sasa fedha hizi zitasaidia kuboresha hali ya huku," alisema Ngorisa.
Inakadiriwa kuwa wastani wa magari kati ya 300 na 400 yanaingia Kijiji cha Samunge kila siku.
Habari hii imeandaliwa na Neville Meena na Mussa Juma, Samunge, Filbert Rweyemamu, Loliondo

1 comment:

Anonymous said...

Lini itagunduliwa dawa ya kutoa au kuponyesha ufisadi??????????

Website counter