
Mchungaji Ambilikile Mwasapile
Ni tukio lililoitikisa na linaloendelea kuitikisa nchi yetu wakati maelfu kwa maelfu ya wananchi, wazee kwa vijana, wanaume kwa wanawake wa itikadi na imani zote wakielekea kijijini Samunge kumuona Mchungaji Ambilikile Mwasapile ili awapatie tiba ya magonjwa hayo sugu. Ndio maana tunasema kuwa hilo ni tukio kubwa na la kihistoria, na ukubwa wa tukio hilo hasa unatokana na ukweli kwamba ni tukio la kiimani.
Kwamba Mchungaji huyo alioteshwa  katika ndoto mwaka 1991 kuwa kuna dawa itakayoshushwa kwake ili aitumie  kutibu  magonjwa ambayo yameshindikana kutibiwa na binadamu. Mashuhuda  wengi wanasema walitibiwa na dawa ya mchungaji huyo tangu alipoanza  kutoa huduma hiyo mwaka 2009. Baadhi wamejitokeza hivi karibuni na  kusema kuwa wamepona maradhi hayo sugu.
Na kama hiyo haitoshi,  watu waliopata dawa ya Mchungaji Mwasapile tangu habari za tiba yake  zilipochapishwa na gazeti hili kwa mara ya kwanza wiki iliyopita,  wamesema dawa hiyo imewatibu na sasa wanaona wako fiti. Baadhi ya  madaktari wamethibitisha kuwa wateja wao ambao awali walikuwa  wanasumbuliwa na magonjwa hayo wamethibitika kupona baada ya kutumia  dawa hiyo inayojulikana kwa jina la Mugariga.
  
Hicho hasa  ndicho kielelezo cha sababu ya maelfu kwa maelfu ya wananchi kumiminika  Loliondo wakitokea kila pembe ya nchi yetu wakifuata dawa hiyo  inayosemekana ni ya ajabu. Pia hicho ndicho kielelezo cha akili, mawazo,  macho na masikio ya Watanzania wote kuelekezwa katika Kijiji cha  Samunge na kutekwa na nguvu anayosemekana kuwa nayo Mchungaji Mwasapile.
  
Na  hasa hiyo ndio sababu ya Serikali kujikuta njia panda pasipo kujua la  kufanya. Katika kuonyesha hali ya kuchanganyikiwa, Serikali kwanza  ilitangaza kupiga marufuku shughuli za Mchungaji  Mwasapile na baada ya  wananchi kupaza sauti wakitaka huduma hiyo iendelee, Serikali ilisalimu  amri mara moja hasa baada ya kutambua kuwa sauti za wananchi zilikuwa za  kiimani zaidi.
  
Ni kwa sababu hiyo tunaipongeza Serikali kwa  kutambua kuwa badala ya kuweka vizuizi ili maelfu kwa maelfu ya watu  wasifuate tiba hiyo kijijini Samunge, ilikuwa busara kuwawezesha watu  wapate tiba hiyo. Serikali ilifanya vyema kugundua kuwa maelfu ya watu  waliokuwa wanafuata tiba hiyo wasingeogopa vizuizi au vitisho vyake,  kwani baadhi yao walikuwa wamekata tamaa kutokana na maradhi sugu  yaliyokuwa yanawasumbua, hivyo walikuwa tayari kwa lolote, hata kufa.
  
Vilevile,  Serikali iligundua kuwa isingekuwa na askari wa kutosha kusimamia amri  zake kwa sababu askari wengi walikuwa njiani kuelekea kijijini Samunge  na wengine tayari walikuwa wamewasili huko kupata dawa hiyo. Pia, baadhi  ya  mawaziri, wabunge na watendaji wakuu serikalini walikuwa miongoni  mwa wananchi waliokuwa wanafuata dawa hiyo.Ndio sababu tangazo la  Serikali kuruhusu shughuli hizo za tiba kuendelea ziliwapa watu wengi  faraja na matumaini makubwa.
  
Sisi tunawahadhalisha wananchi na  Serikali kuwa, pamoja na tiba hiyo kuwa suala la kiimani, tusifanye  makosa kuanza kufanya sherehe. Tunawashauri wananchi wote kwanza waipe  dawa hiyo muda wa kutosha ili itoe matokeo na baadaye wataalamu wa afya  wayathibitishe pasipo shaka.
  
Kwa upande mwingine,  tunawashauri wale wanaohisi wameponywa au hawajaponywa na dawa hiyo  wajitokeze kutoa ushuhuda ili mamlaka husika ziweze kufanya tathmini na  kuwapa wananchi maelekezo stahiki. Ni imani yetu kuwa watakaoponyeshwa  na dawa hiyo hawatafanya vitendo hasi, bali watamshukuru Mwenyezi Mungu  kwa kuwaletea nuru mpya.
   
 
No comments:
Post a Comment