Tuesday, March 8, 2011

KAMA ULIKUWA 'MWOGA' BASI IGA MFANO WA MKAKA HUYU...Mashili: Mhitimu kidato cha sita mwenye miaka 45Image
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Bariadi, Deogratius Hela akimpongeza Mashili. • SOKO la Pamoja la Afrika Mashariki limeanza kazi katika nchi wanachama, changamoto inakuja kwa wajasiriamali ambao hawana elimu ya kutosha kufanya biashara ndani na nje ya nchi,” anasema mjasiriamali Peter Mashili.

  Kauli ya Mashili (45), inatokana na mtazamo wake wa mbele kuhusu elimu ambapo kwa kutambua umuhinu wake amelazimika kwenda shule licha ya kuwa na umri mkubwa, ili aweze
  kusimamia vyema biashara zake sambamba na kujiandaa kukabiliana na soko hilo.

  Anasema soko hilo linaonekana kuwa tishio kwa wafanyabiashara wa Tanzania ambao wamekuwa wakidai hawajaandaliwa kulipokea.

  Anasisitiza kama Serikali haijawaandaa kukabiliana na soko hilo wafanyabiashara wanatakiwa kuwa na malengo ya muda mrefu pamoja na kujiandaa na changamoto zinazoweza kujitokeza wakati wowote.

  “Nimeliona hilo na kwa kuwa sikupata nafasi ya kusoma vizuri nilipokuwa mtoto, niliamua hivyo sasa na nimehitimu kidato cha sita nitatimiza malengo yangu na familia yangu,”
  anasema Mashili.

  Anasema wajasiriamali wasiokwenda shule watapata wakati mgumu katika kulimudu Soko
  la Pamoja la Afrika Mashariki lililoanza hivi karibuni. Mashili amehitimu kidato cha sita katika
  Sekondari ya Hillcrest ya jijini Mwanza, ambapo alikuwa anasoma masomo ya biashara.

  Anasema umri sio kigezo cha yeye kutosoma, na kuongeza kwamba wajasiriamali na Watanzania waoga ambao hawapendi kujiendeleza watapata wakati mgumu kwenye soko hilo.

  “Natoa rai kwa wajasiriamali wenzangu kutoogopa kwenda shule hata kama umri wao ni
  mkubwa, huenda kwa siku za nyuma hawakupata nafasi hiyo kutokana na sababu mbalimbali,
  sasa waamke wasome Elimu haina Mwisho”, ni kauli ya Mashili.

  Dunia ya leo ni ya utandawazi, dunia kama kijiji, elimu ya maisha inayopatikana mitaani
  haitoshi ambapo wakati umefika kwa Watanzania kuona kuwa elimu ndiyo msingi wa maisha
  ya kila siku na kulazimika kujiendeleza.

  Mjasiriamali asiye na elimu katika Soko la Pamoja atajenga hofu pamoja na kutojiamini,
  hivyo kutoweza kushindana na wajasiriamali wengine, kwa kuwa pamoja na vigezo vya soko
  hilo suala la elimu lina umuhimu wake.

  Nchi nyingine zilizoingia kwenye Soko hilo la Pamoja wamepata maandalizi mapema sambamba na mifumo yao ya elimu lakini hapa kwetu udhaifu wa lugha ya Kiingereza unatoa
  mwanya kwa wenzetu kupata nafasi zaidi ya kushinda.

  Anatoa mfano unapozungumza na raia wa Kenya, mara nyingi hutumia lugha ya Kiingereza, anapoona unayumba kwenye lugha hiyo, huwa na wasiwasi ya kutofaa kwenye soko hilo .

  Biashara zote hivi sasa zinaendeshwa kwa kusaini mikataba na iwapo mjasiriamali hana uelewa ni wazi atashindwa kufanya biashara vyema na kupata hasara kila kukicha ama atalazimika
  kutafuta watu wenye elimu ili waweze kumsaidia.

  “Shughuli za kiuchumi ninazofanya zinaambatana na elimu mfano ujenzi, dawa ambapo
  nilibaini kuwepo kwa changamoto hiyo, wakati mwingine ilinilazimu kusaini mikataba nisiyoielewa mingi imeandaliwa na wenye taaluma au ufahamu wa lugha,” anasema Mashili.

  Huku akionesha furaha yake kwenye mahafali ya kumaliza kidato cha sita katika shule hiyo, Mashili anasema hivi sasa ana uwezo wa kusoma nyaraka zote na kuzielewa vizuri kabla ya kuzisaini.

  Wakati akisoma shuleni hapo, alimkabidhi mkewe majukumu ya kusimamia shughuli zake
  wakiwamo wataalamu aliowaajiri. Mashili anasema hakubahatika kusoma elimu ya sekondari akiwa na umri wa kufanya hivyo kama ilivyozoeleka, kutokana na hali ya uchumi ya wazazi wake.

  Hivyo alijikita zaidi kwenye ujasiriamali ambapo alipata fedha ila kwa kuwa hakuwa na elimu hakuweza kuziendeleza ipasavyo, hadi alipoamua kurudi darasani. Mwaka 2005 alijiunga na kidato cha kwanza katika Sekondari ya Bupandagira iliyopo wilayani Bariadi, Mkoa wa Shinyanga baada ya kupata mafunzo ya Kiingereza.

  Mwaka 2008 alihitimu kidato cha nne na kupata daraja la tatu kisha alijunga na Sekondari ya
  Hillcrest kwa masomo ya kidato cha tano na sita kwa mchepuo wa Biashara. Anasema aliamua kusoma masomo ya biashara ili yamsaidie kuendesha biashara zake ambapo tayari amezianzisha lakini amelazimika kuajiri wataalamu wa kumsaidia kutokana na
  kutokuwa na elimu ya kutosha.

  Lengo la Mashili ni kufika chuo kikuu na ili aweze kufanya kazi zake kwa ufanisi na uelewa,
  hivyo kutosaini au kudanganywa kwenye nyaraka mbalimbali za biashara. Anasema akiwa shuleni alipata changamoto mbalimbali kutokana na umri wake, ambapo wapo baadhi ya wakuu wa shule walimkataa asijiunge na shule hizo kwa kuwa umri wake ni mkubwa.

  Alipopata nafasi kwenye shule hizo,wanafunzi wenzake walimshirikisha kwenye mijadala
  ambayo yeye aliiona kuwa ni ya kitoto na wakati mwingine alikuwa akipewa chakula kingi ikilinganishwa na wanafunzi wengine kutokana na umri wake.

  Peter Mashili ni mwenyeji wa Wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza na mkazi wa Wilaya ya
  Nzega mkoani Tabora ni mtoto wa saba kati ya watoto 11, wa mzee Andrew Mashili alipata
  elimu ya msingi mwaka 1982 hadi 1988.


  No comments:

  Website counter