Wednesday, March 30, 2011

HII NAYO IMEKAAJE JAMANI...

Pinda akerwa na malumbano ya Sumaye, UVCCM Send to a friend


Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akijibu maswali kwenye mkutano na Wahariri wa Vyombo vya Habari uliofanyika jana Ofisini kwake, Dar es Salaam. Picha na Emmanuel Herman

Mwandishi Wetu
WAZIRI Mkuu, Mizengo Pinda amesema malumbano ya kisiasa yanayoendelea ndani ya CCM kati ya mawaziri wakuu wastaafu na viongozi wa Umoja wa Vijana wa chama hicho (UVCCM), hayana tija kwa chama na taifa kwa jumla.

Pinda alisema hayo katika mkutano wake na wahariri wa vyombo vya habari nchini uliofanyika ofisi kwake jana, baada ya kuulizwa kwamba, akiwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM analichukulia vipi suala la malumbano yanayoendelea ndani ya chama hicho, kati ya viongozi chama, UVCCM na Waziri Mkuu Mstaafu wa Serikali Awamu ya Tatu, Frederick Sumaye?

Pinda alisema mvutano huo siyo mzuri na kwamba hata viongozi wanaotoa ushauri kuhusu mwenendo wa chama, wanatakiwa kufuata utaratibu wa kutoa dukuduku zao kupitia vikao halali vya CCM tofauti na wanavyofanya sasa.
“Kwa jumla, malumbano yanayoendelea sasa siyo mazuri, ila pia wanaotoa ushauri ni vizuri wakatumia vikao, halali vya chama ili yapatiwe ufumbuzi ndani ya chama,” alisema Pinda.

Alisema viongozi wana haki na nafasi ya kutoa maoni yao katika vikao lakini, baadhi yao hawafanyi hivyo na huenda wanaogopa, badala yake wanaeleza nje ya vikao na kusababisha malumbano yasiyo na msingi.

Wiki iliyopita, Sumaye alijibu shutuma mbalimbali ambazo zimekuwa zikielekezwa kwake na Katibu Mkuu wa CCM, Yusuf Makamba, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi, akisema kauli za hivi karibuni za viongozi wa UVCCM dhidi yake ni matusi, kejeli na hatari kwa taifa.

Sumaye aliwaambia waandishi wa habari Dar es Salaam kwamba CCM bado ni chama kinachotegemewa kuleta maendeleo kwa Watanzania siku zijazo, lakini kauli za makada wake hao ni kali na zinaashiria kuwa hakina budi kusafishwa ili kirudi kwenye mstari.

Hivi karibuni, Baraza Kuu la UVCCM Taifa likitanguliwa na lile la Mkoa wa Pwani, walitoa kauli kali za kuwatisha viongozi wanaokikosoa chama hicho nje ya vikao, wakisema lengo lake ni kuharibu mustakabali wa CCM.
Umoja huo uliapa kuwa utafanya kampeni za kuhakikisha viongozi hao, uliodai kuwa wana malengo ya kuwania urais mwaka 2015, hawapati nafasi yoyote ya uongozi.

Mbali na Sumaye, viongozi wengine walioshambuliwa ni pamoja na Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta ambaye amekuwa mstari wa mbele kukitaka CCM kijibu hoja za Chadema badala ya vitisho.
Sumaye pia alianza kushambuliwa baada kukitaka CCM kijibu hoja za Chadema ambazo alisema badala ya kuiachia Serikali lazima chama hicho kizijibu kwa sababu ni za kisiasa.

Tiba ya Loliondo
Kuhusu tiba ya magonjwa sugu inayotolewa na Mchungaji Ambilikile Masapila katika Kijiji cha Samunge, wilayani Ngorongoro, Pinda aliitaka Halmashauri ya Wilaya hiyo, kutumia fedha ilizokusanya kwa kutoza fedha magari yanayokwenda huko kuboresha mazingira na miundombinu katika eneo la kutolea tiba hiyo.

"Halmashauri ya wilaya hiyo imekusanya fedha nyingi kutokana na ushuru wa magari ya kwenda katika Kijiji cha Samunge. Hivyo tumeiagiza itumie fedha hizo kuboresha mazingira na miundombinu katika eneo la Mchungaji inapotolewa tiba hiyo," alisema Pinda.

Alisema Serikali imeuagiza uongozi wa Mkoa wa Arusha kuratibu safari za kwenda katika kijiji hicho kwa kuweka vizuizi katika barabara zote zinazokwenda huko kuanzia Arusha Mjini, Babati na Bunda ambako wagonjwa watachukuliwa kwenda Samunge kwa zamu kupitia eneo la Mto wa Mbu.

Pia aliitaka Halmashauri ya Ngorongoro kutafuta eneo karibu na kijiji hicho kwa ajili ya kuzika wagonjwa wanaofariki dunia wakiwa huko.

No comments:

Website counter