Aliyekuwa ofisa habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Florian Kaijage
ALIYEKUWA ofisa habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Florian Kaijage ametajwa kuhusika na uzembe uliosababisha fadhaa kwa uongozi wa kitaifa akiwamo Rais Jakaya Kikwete kwa kutoimbwa nyimbo za mataifa wakati wa mechi ya kimataifa ya Taifa Stars na Morocco mwaka jana.
Akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam jana, mwenyekiti wa kamati maalum ya kuchunguza tukio la kutopigwa nyimbo hizo wakati wa mchezo huo wa Oktoba 8 mwaka jana, ambaye pia ni Mwanasheria Mkuu wa zamani wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), Hamidu Mbwezeleni alisema wamebaini kuwa Kaijage alishindwa kutekeleza wajibu wake na hasa baada ya kupuuza maagizo ya kikao cha maandalizi ya mechi hiyo.
"Kwanza kabisa tumebaini siku moja kabla ya mechi kulikuwa na kikao cha maandalizi ya mchezo kati ya serikali na TFF."Kimsingi, Rais wa TFF, Leodegar Tenga alimwagiza Kaijage kuhakikisha CD za nyimbo za taifa zinaandaliwa mapema na kufanyiwa majaribio ili kama kuna upungufu uweze kurekebishwa mapema na ikiwezekana hata bendi ya brass ya polisi itumike, lakini hakutekeleza maagizo hayo.
"Pia, mwenyekiti wa kikao cha matayarisho ya mechi hiyo, Leonard Thadeo (Mkurugenzi wa Michezo, Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo) aliagiza uongozi wa Uwanja wa Taifa ufungue mapema milango mapema kumwezesha Kaijage na timu yake kufanya majaribio mapema ya vifaa vyote, lakini Kaijage hakufanya hivyo licha ya milango hiyo kufunguliwa kama walivyoagizwa," alieleza Mbwezeleni.
Mbwezeleni alilitaja kosa jingine lililofanywa na Kaijage kuwa ni kumkabidhi mtaalamu wa Kichina kwenye studio za uwanja huo CD ya aina ya MP3 ambayo ilikuwa haioani na mashine zinazotumika kwenye uwanja huo hali ambayo ilileta mtafaruku mkubwa.
Mbwezeleni alisema Kaijage baada ya kumpa Mchina CD hizo aliondoka na kuendelea na shughuli zake nyingine alizokuwa nazo kwenye Uwanja wa Taifa, lakini Mchina alipojaribu kupiga wimbo huo wa Morocco CD iligoma kwa sababu ni MP3.
Mtaalamu huyo wa Kichina alipoona CD aliyopewa haioani na mashine za pale uwanjani aliamua kutoka kwenye studio na kuanza kumtafuta Kaijage ambaye hakukumwona.
Mbwezeleni alisema Kaijage alipomaliza shughuli zake alirudi studio ili kuonana na mtaalamu huyo wa Kichina ili kujua mambo yanakwendaje, lakini Mchina hakuwepo kwa sababu alikuwa tayari amekutwa na zahama ya CD kukataa kupiga na alikuwa akimtafuta Kaijage.
" Msimamo wa kamati ni kwamba Kaijage, ama alikuwa mzembe au hakuwa mwangalifu katika utendaji wake wa kazi hiyo,"alisema mwenyekiti wa kamati hiyo.
"Tumebaini kuwa Kaijage hakwenda kufanya majaribio ya CD kama alivyoelekezwa, alimkabidhi mtaalamu wa Kichina CD za MP3 wakati mashine iliyoko uwakanjani hapo haitumii mfumo huo, hivyo ni dhahiri ulikuwa uzembe kwa sababu kama angefanya majaribio mapema zipo studio ambazo zimeweza kutengeneza CD nyingine,"alisema Mbwezeleni.
Aidha, mwenyekiti huyo alisema kuwa kamati yake imetoa mapendekezo ya kuwepo kwa mtaalamu wa Kitanzania au Kichina, lakini awepo studio saa moja kabla ya mchezo kuanza, tena bila kuondoka.
Pia, imependekezwa kuwa watu wa itifaki (protocol) wapatiwe nyimbo za taifa siku moja kabla ya mchezo ili kuzifanyia mazoezi.
Kamati hiyo, pia imeshauri kwamba suala la mazoezi ya vyombo na mashine za sauti liwe la lazima na wahusika waandikiwe) na kutaarifiwa kuhusu kazi hiyo ili kuondoa fadhaa kama ilivyojitokeza.
Katika mchezo huo wa kufuzu kwa fainali za Afrika mwaka 2012, Stars ilifungwa kwa bao 1-0 huku nyimbo hizo zikilazimika kuimbwa wakati wa mapumziko ya mchezo huo, jambo ambalo lilisababisha aibu na fadhaa, kiasi cha TFF kuunda kamati hiyo.
Katika utetezi wake, Kaijage aliiambia kamati hiyo kuwa alizidiwa na kazi kubwa mbili, zikiwamo za kushughulikia vitambulisho vya ziada kwa ajili ya waandishi wa habari pamoja na watangazaji wa kituo cha Supersports cha Afrika Kusini kilichorusha laivu mechi hiyo.
Jukumu jingine likiwa la kuandaa orodha ya wachezaji wqa timu zote mbili zilizotakiwa kucheza siku hiyo kwa muda kabla ya kuanza kwa mchezo huo.Pia, aliieleza kamati kwamba alichelewa kupata CD yenye wimbo wa taifa wa Morocco hadi Oktoba 8 saa 11.00 jioni.
Kesho yake, yaani Oktoba 9, Kaijage aliieleza kamati hiyo kuwa alipata CD nyingine ya wimbo huo kutoka kwa maofisa wa diplomasia wa Morocco waliotokea Nairobi, Kenya, majira ya saa 4 asubuhi, hivyo kutopata muda wa kutosha wa kuzifanyia mazoezi ya kutosha.
Kamati hiyo, hata hivyo haipendekezi hatua zozote za kinidhamu dhidi ya Kaijage, ambaye hata hivyo ameondoka TFF na nafasi yake tayari imejazwa na Boniface Wambura.
|
No comments:
Post a Comment