Sunday, February 20, 2011

NI UAMUZI WA BUSARA ILA WALIPWE WAHUSIKA HALISI NA SIO 'MAMLUKI' ...WATAKAOJITOKEZA


Rais Jakaya Mrisho Kikwete


SERIKALI imesema itagharimia mazishi ya watu waliofariki dunia kutokana na milipuko ya mabomu iliyotokea usiku wa kuamkia juzi katika kambi ya JWTZ, Gongo la Mboto jijini Dar es Salaam na kuwalipa kifuta jasho wafiwa na majeruhi wote.

Mbali na malipo hayo, serikali pia imeiagiza kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa wa Dar es Salaam na kutengo cha maafa cha Taifa kufanya tathimini ya nyumba na mali zilizoharibiwa kisha kuwatambua wamiliki wake ili walipwe fidia.

Tamko hilo la Serikali limetolewa na Rais Jakaya Kikwete jana baada ya kumalizika kwa mkutano wa dharura wa Baraza la Usalama la Taifa uliofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam, juzi.

"Tumeamua kuwa, Serikali igharamie mazishi ya marehemu wetu hao popote ndugu watakapoamua wakazikwe. Baadae ndugu wa marehemu wapewe kifuta machozi," alisema Rais Kikwete katika taarifa hiyo na kuongeza:

"Baraza la Usalama la Taifa, limeagiza Kamati ya Maafa ya Mkoa wa Dar es Salaam na Kitengo cha Maafa cha Taifa wazitambue mapema iwezekanavyo nyumba zilizoharibiwa, wenye nyumba na kuhakikisha kuwa matayarisho husika yanafanyika ikiwa ni pamoja na uthamini ili walipwe fidia wanayostahili bila kuchelewa."

Kuhusu waliojeruhiwa alisema "Tumeamua kuwa Serikali igharamie matibabu yao. Baadaye watakapotoka hospitali walipwe kifuta machozi kwa ulemavu walioupata."

Mbali na hatua hiyo, Rais Kikwete alisema Baraza limeiagiza Kamati ya Maafa ya mkoa kushirikiana na Kitengo cha Maafa cha Taifa kilichopo Ofisi ya Waziri Mkuu kuwahudumia wananchi waliopoteza makazi yao au waliolazimika kuyakimbia makazi yao kwa nia ya kuokoa maisha yao.

"Ihakikishwe kuwa wanapatiwa makazi ya muda pamoja na huduma za malazi, chakula, maji, afya na usafi wa mazingira haraka iwezekanavyo," amesema Rais Kikwete ambaye juzi aliwatembelea hospitalini waliojeruhiwa.

Rais Kikwete alisema alilazimika kuitisha mkutano huo ulioanza alasiri na kumalizika usiku, baada ya kutafakari kwa kina na kuona uzito na unyeti wa tukio hilo.

Kwa mujibu wa Rais Kikwete, Baraza hilo ambalo ndio chombo cha juu cha kumshauri rais kuhusu masuala yahusuyo usalama wa taifa, limesikitishwa sana na tukio hili na hasa vifo vilivyotokea na majeraha waliopata watu na hivyo baraza limetoa pole kwa majeruhi wote.

Alisema kuwa baraza limelipongeza Jeshi la Ulinzi kwa uamuzi wake wa haraka wa kuwatuma wahandisi kufanya kazi ya kutafuta, kutambua na kuyakusanya mabomu yote yaliyoangukia katika maeneo ya raia.

"Tunawaomba wananchi watoe ushirikiano wa hali ya juu kwa Jeshi kwa kuwapa taarifa wanapoyaona mabomu katika maeneo yo yote," alisema Rais Kikwete.

Rais Kikwete alisema baraza hilo pia limeagiza Jeshi kufanya uchunguzi wake wa ndani wa chanzo cha tukio hili kama Sheria ya Ulinzi wa Taifa inavyoagiza. Aidha, imetaka vyombo vingine vya ulinzi na usalama visaidie katika uchunguzi huo.

"Baraza limeamua pia kuwa, Serikali ya Tanzania iombe nchi rafiki zisaidie katika uchunguzi wa chanzo cha tukio hili na kushauri namna bora zaidi ya kuimarisha usalama na uhifadhi wa mabomu na risasi katika maghala ya Jeshi letu kote nchini," alisema rais Kikwete katika taarifa hiyo iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu.

Rais ameliagiza pia jeshi la Polisi kushirikiana na ndugu waliopotelewa na watoto na kuhakikisha wanapatikana haraka na kuunganishwa na familia zao.

Rais Kikwete alisema tukio hilo limemsikitisha na kumpa uchungu mwingi, hasa kwa kuzingatia ni miaka miwili tu imepita tangu mabomu mengine yalipuke kwenye kambi ya jeshi ya Mbagala Kizuiani jijini Dar es Salaam.

Kwa sababu hiyo akawaomba wananchi wawe watulivu katika wakati huu mgumu na kuahidi kwamba uchunguzi utafanywa na vyombo vya ndani na nje ya nchi ili kujua kiini cha tatizo hilo.

No comments:

Website counter