Monday, February 28, 2011

HONGERA DADA YANGU, SIO WENGINE WANAUCHUNA TU KAZI KUWAAMBUKIZA WENZAO KWA MAKUSUDI...

Salama: Jasiri aliyetangaza kuishi na virusi vya UkimwiImage
Salama
Maisha tunayoishi hapa duniani, yanahitaji uvumilivu, ujasiri pamoja na busara miongoni mwa jamii inayotuzunguka. Nashawishika kusema hayo baada ya kukutana na Salama Jumanne, ambaye ana ujasiri wa kueleza kitu kinachomsibu pamoja na kupambana na misukosuko kwa jamii ambayo ilimcheka baada ya kuamua kujitangaza kuishi na Virusi vya Ukimwi (VVU). Nilipomwona mara ya kwanza, sikuamini kile alichokieleza kuwa anaishi na VVU, hali iliyonilazimu katika nafasi yangu ya uandishi wa habari, kuandika habari zake na kufuatilia kila tukio analokumbana nalo nami kuliandika ili watu mbalimbali waweze kumsaidia kutokana na matatizo anayokumbana nayo.

Nilihuzunika baada kunieleza historia ya maisha yake, pia nilijiuliza maswali mengi, je, ingekuwa mimi nakumbana na tatizo hili ningekaa kimya au ningewaeleza wenzangu? Je, marafiki, wazazi na jamii kwa ujumla wangelipokeaje tatizo langu ingawa mimi mwenyewe nimeshaamua kulitangaza ili nipate msaada? Binafsi sina uwezo mkubwa wa kumsaidia Salama lakini naamini watu mbalimbali pamoja na wahisani, wataguswa na habari hii na kumsaidia kwa kuwa licha ya kuwa anaishi na VVU, pia ana watoto watatu na mjukuu mmoja.

Salama ni mtu mwenye haiba, huwezi kuamini kuwa anaishi na VVU mpaka alipojitangaza kuwa na hali hiyo, umati uliokusanyika pale Mabibo katika Viwanja vya Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), Siku ya Maadhimisho ya Mwanamke Duniani, inayofanyika Machi 8 kila mwaka. Baada ya kueleza maisha yake, niliamua kuandika makala iliyotoka katika gazeti hili, lakini baada ya hapo watu mbalimbali wanaoishi na Salama eneo la Tandale kwa Pakacha, walimcheka, walimrushia maneno ya kejeli na kumdhihaki.

Naye mama mwenye nyumba aliyopanga, alimtaka kuondoka katika nyumba hiyo kwa madai kuwa atawaambukiza wapangaji wenzake pamoja na watoto kwa kuchangia choo. Ukweli ni kwamba Ukimwi hauambukizwi kwa kushirikiana maliwato, au vyombo vya kulia na anayeishi na VVU, wala kukumbatiana naye, bali asilimia kubwa ya maambukizi yanatokana na kushiriki ngono zembe na anayeishi na VVU. Njia nyingine na ndogo ya maambukizi ya VVU, inatokana na kitendo cha mtu asiyekuwa na maambukizi, kuongezewa damu ya anayeishi ya VVU au kuchangia naye vifaa vyenye ncha kali vikiwamo sindano, miswaki na nyembe.

Njia nyingine ya maambukizi ni kutoka kwa mama mjamzito kwenda kwa matoto, na maambukizi hayo hutokea wakati wa kuzaliwa kwa mtoto. Wataalamu wa mambo ya afya ya mama na mtoto, wanaeleza kuwa mtoto anapokuwa tumboni kwa mama, huwa salama. Ndiyo maana wajawazito hushauriwa kuhudhuria kliniki mara kwa mara na kupimwa afya zao, ili madaktari wajiandae kumsaidia mtoto asipate maambukizi wakati wa kuzaliwa, jambo ambalo linawezekana na limeshaonyesha mafanikio.

Salama anakumbuka alizaliwa mwaka 1972 katika Hospitali ya Wilaya ya Bagamoyo, lakini hakumbuki tarehe wala mwezi, alianza Shule ya Msingi Nia Njema mwaka 1988 ingawa aliishia darasa la sita kwa kuwa baada ya kuvunja ungo, wazazi wake walimweka ndani ili afundishwe “unyago”. Baada ya kukaa ndani kwa muda, alitafutiwa mchumba na kulazimishwa kuolewa akiwa na umri mdogo. Alilazimika kuozwa kwa mzee ambaye alikuwa na umri zaidi ya miaka 60 wilayani Bagamoyo na alidumu katika ndoa hiyo kwa muda wa miezi sita. Miezi sita ilipoisha, mume huyo anayemkumbuka kwa jina moja la Jumanne, alifariki. Hawakubahatika kupata watoto na hivyo baada ya msiba wa mume wake, alifukuzwa na ndugu wa mume huyo.

Alianza kuhangaika na maisha, alikosa makazi maalumu. Mwaka 1988, alimpata mume mwingine aitwaye John, ambaye aliishi naye Bagamoyo bila kufunga ndoa na mwaka 1989, alipata mtoto wake wa kwanza aitwaye Zawadi John (20), Godfrey John (14) na mwaka 1999 alibahatika kupata mtoto wa tatu aitwaye Victoria John (10). Baada ya kumpata Victoria, Salama alianza kujisikia kuchanganyikiwa, ndipo mama yake, Asha Athumani (60), aliamua kumuuguza kwa kuuza kiwanja na vitu vyake vya thamani ili mwanawe aweze kupona, lakini kadri siku zilivyozidi kwenda, hali yake ilikuwa inazidi kuwa mbaya ingawa alikuwa akiishi na mumewe.

Baada ya kuumwa kwa muda mrefu, ilipofika Septemba 4, 2000, aliamua kwenda Hospitali ya Wilaya ya Bagamoyo kupima afya yake, ambako aligundulika kuishi na VVU. Baada ya kupata majibu hayo, alikwenda nyumbani kwa mama yake mzazi na kumweleza matokeo ya majibu yake. Salama anasema mama yake mzazi Asha, alichukia sana kutokana na majibu hayo na kuhoji kwa nini auze kiwanja chake na vitu vya thamani alivyokuwanavyo, ili amhudumie wakati akijua kuwa alikuwa akiishi na VVU? Mama huyo alifikia uamuzi wa kumwamuru asiende tena nyumbani hapo na atafute mama mwingine.

Anasema baada ya kauli hiyo kutolewa na mama yake mzazi, alisikitika na kurudi nyumbani kwake ambako alimkuta mume wake John. Alimwelezea majibu aliyopewa hospitalini na kumshauri naye akapime. Salama anasema mara ya kwanza John, alikataa lakini baadaye alienda kupima na kukutwa naye anaishi na VVU. Kutokana na majibu hayo, walifikia uamuzi wa kuwachukua watoto wote watatu kwenda kuwapima hospitalini, lakini majibu yalipotoka, ilibainika kuwa hakuna hata mmoja aliyeambukizwa VVU.

Ingawa hajui ugonjwa huo aliupata lini, Salama anasema mwaka 2007, kulitokea kutokuelewana kati yake na mume wake John kulikosababishwa na tofauti za dini, kwa kuwa mume wake ni Mkristo na yeye Muislam. Baada ya tofauti hiyo, John aliamua kuondoka na kumuachia jukumu la kulea watoto hao peke yake, na ndugu wa mume huyo pia wakaamua kumtenga. Alihangaika kutunza watoto wake kwa kujishughulisha na biashara za vitenge na khanga, ambapo wakati wanaachana na mume wake huyo, mtoto wake wa kwanza, Zawadi John, alikuwa ameshamaliza darasa la saba na alikuwa na mimba.

Wakati alipokuwa akisubiri majibu, alibahatika kujifungua mtoto ambaye alipewa jina la Hafidh John, sasa ana miaka miwili. Hata hivyo, majibu yalipotoka Zawadi alifaulu na kuchaguliwa kujiunga na Shule ya Sekondari Changarikwa, iliyopo Chalinze mkoani Pwani. Anasema mtoto wa pili ambaye ni Godfrey amemaliza darasa la saba mwaka 2008, lakini hakubahatika kujiunga na kidato cha kwanza. Kwa sasa yupo nyumbani na Victoria anasoma darasa la tatu wilayani Bagamoyo. Anasema pato la biashara yake halimtoshi ingawa anasaidiwa na shirika lisilo la kiserikali la Action Aid, linalojishughulisha na mambo mbalimbali ya kusaidia jamii.

Anasema kwa msaada wa shirika hilo na pato lake hilo, amekuwa akiweza kukidhi mahitaji machache ya familia ingawa bado anahitaji msaada. Salama ni mmojawapo kati ya wanachama 253 wakiwamo wanawake na wanaume wanaoishi na VVU, katika chama cha WAMABA, kilichopo Bagamoyo, mkoani Pwani na anatoa mwito kwa jamii na wanawake kwa ujumla kutokata tamaa. Anasema matatizo ni sehemu ya maisha ya mwanadamu na jambo kubwa ni kukabiliana nayo badala ya kujuta.

Anasisitiza kuwa jambo la msingi ni kukabiliana nayo na si kusikitika na kwamba ingawa ametengwa na familia yake, lakini bado anampenda mama yake. Amemsamehe mama yake kwa kuwa alikuwa na hasira na uelewa duni kwani alifikiri anaweza kufa kutokana na kugundulika kuishi na VVU lakini bado anaishi na kulea familia yake pamoja na mjukuu. Baada ya habari zake kuchapishwa kwenye gazeti hili, tabia ya baadhi ya wapangaji wenzake, mama mwenye nyumba na watu anaoishi nao mtaani, zilibadilika na walianza kumdhihaki kwa maneno mbalimbali.

Anasema alifanya juhudi za kuonana na mama mwenye nyumba lakini hakuwa tayari kuzungumzia suala hilo, badala yake alimsihi Salama kutafuta nyumba nyingine ya kuishi. Anasema atalazimika kuondoka hapo kwa sababu mama mwenye nyumba hiyo, amemtaka kuondoka ingawa hana fedha ya kutafuta nyumba nyinyine kwa sasa kwani mtaji wake wa biashara ya khanga na vitenge, hautoshi kumwezesha kupata fedha kwa haraka kiasi hicho. Kwa sasa anatafuta wafadhili mbalimbali kumsaidia katika tatizo hili.

Mwanasheria wa Kampuni ya Tanzania Standard Newspapers (TSN), Emmanuel Tamila, anasema kuna umuhimu kwa wanaharakati, wanasheria pamoja na wadau mbalimbali, kutoa elimu kwa wananchi juu ya unyanyapaa, kwani unyanyapaa si kwa wanaoishi na VVU tu, bali hata watu wenye magonjwa mbalimbali, hunyanyapaliwa. Anasema ipo haja kwa jamii kuelimishwa juu ya Sheria ya Ukimwi ya mwaka 2008, na kuvijua vipengele vyake, ili waelewe kuwa ukimnyanyapaa anayeishi na VVU, ni kuvunja Sheria hiyo.

Kifungu namba 6 kipengele cha 32 cha Sheria hiyo, kinaeleza kuwa mtu yeyote atakayebainika kumdhalilisha au kumnyanyapaa mwenye VVU, akitiwa hatiani, analazimika kulipa faini ya Sh milioni 2 au kifungo cha mwaka mmoja au kutumikia kifungo pamoja na faini. Mkurugenzi wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (TAMWA), Ananilea Nkya, anasema ingawa wanasheria, wanaharakati pamoja na wadau mbalimbali wanazungumzia kuhusu Ukumwi na unyanyapaa, ipo haja kwa wananchi kupewa elimu ya kutosha kuhusu unyanyapaa, ili wasiwatenge watu walioathirika na badala yake waongeze upendo ili nao waishi sawa na binadamu wengine.

No comments:

Website counter