Monday, February 28, 2011

DUUH KAZI 'KWEELI KWEELI' LOOH...

Slaa alipua mabomu Send to a friend


Katibu mkuu wa Chadema Dk Willibroad Slaa akihutubia umati wa watu waliofurika katika uwanja wa Mkendo mjini msoma jana katika muendelezo wa maandamano ya chama hicho nchi nzima yalioanzia mkoani Mwanza alhamisi wiki hii.

MAANDAMANO ya Chadema yameingia mkoani Mara na kuuteka mji wa Musoma huku Katibu mkuu wa chama hicho, Dk Wilibroad Slaa, akitoboa siri ya kulipuka kwa mabomu ya Gongo la Mboto na Mbagala.

Naye Mwenyekiti Chadema taifa, Freeman Mbowe aliitahadharisha Serikali kuwa taifa litaingia kubaya iwapo mchakato wa mabadiliko ya katiba utachakachuliwa kwa maslai ya mafisadi.

Akizingumza jana katika Uwanjwa wa Mukendo mjini Musoma baada ya maandamano ya kilomita 15 kutoka Bweri hadi mjini, Dk Slaa alisema kulipuka kwa mabomu hayo kumetokana na Serikali ya CCM chini ya Rais Jakaya Kikwete kupuuza ombi la Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kuwapa fedha kwa ajili ya kuteketeza mabomu yaliyokwisha muda wake.

Alisema kazi ya jeshi ni kulinda uhai wa watu wake nchini, lakini kupitia jeshi taifa limeweza kupoteza watu zaidi ya 40 kutokana na serikali kugoma kutoa fedha hizo ambazo ziliombwa na JWTZ.

“Tunataka Kikwete atueleze kwa kina kama ni kweli, maana tunaambiwa kabla ya mabomu kulipuka mwaka 2009 JWTZ (Mbagala) waliomba fedha kwa ajili ya kuteketeza mabomu, lakini kutokana na serikali kutothamini maisha ya watu wake ilikataa kuwa hakuna fedha.

"Tunaambiwa tena kuwa kabla ya mabomu haya ya mwisho kulipuka wanajeshi waliomba fedha serikalini kwa ajili ya kuteketeza mabomu hayo, lakini pia serikali hiyohiyo haikutoa kwa madai kuwa hakuna fedha,” alieleza Dk. Slaa.

Kwa sababu hiyo akamtaka
Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Hussein Mwinyi alijiuzulu.

Dk Slaa alisema kuwa Watanzania wanataka Waziri Mwinyi afuate nyayo za baba yake kama ambavyo alijiuzulu kwa mauaji ya polisi mkoani Shinyanga na kwamba asipofanya hivyo baada ya siku tisa kuisha Chadema watatangaza hatua ya pili kwa ajili ya kumshinikiza ajiuzulu.

Onyo kuhusu Katiba

Akizungumza katika mkutano huo uliokuwa umefurika watu, Mweyekiti wa chama hicho, Mbowe alitahadharisha kuwa serikali ya CCM itaingilia na kuvuruga mchakato wa katiba kwa maslai yake binafisi, basi "Tanzania patachimbika kama Tunisia na Misri."

Hata hivyo, Mbowe alisema kwa muda sasa amekuwa akishangazwa na kauli za Rais Kikwete ambazo zimekuwa zikidai kuwa nchini kuna udini akisema hizo ni propaganda zake.

Alisema kama kweli Kikwete anauhakika juu ua jambo hilo basi anapaswa kuwachukulia hatua wahusika.

Kabla ya mkutano huo viongozi hao waliwaongoza wananchi wa Musoma kuandamana umbali wa kilomita 15 wakitembea kupinga ugumu wa maisha na kulipwa kwa Dowans.


“Tutaendelea kuandamana mpaka maskini wa Tanzania asikilizwe. Tutaandamana mpaka vijana wa kitanzania wapate ajira na hatutalala mpaka kieleweke,” alisema Mbunge wa Ilemela, Highness Kiwia.

Mbunge wa Nyamagana, Ezekiel Wenje alisema vijana wengi wanafanya kazi za umachinga kwa sababu ya mfumo mbovu uliowekwa na serikali unaowafanya wakose ajira.

“Musoma kulikuwa na kiwanda kizuri sana cha Mutex kilichokuwa kinatoa ajira kwa vijana, lakini kwa uzembe na ujanja wakawapa watu kwa madai ya kubinafsisha. Sasa kimefungwa hakuna ajira kwa vijana na matokeo yake ndiyo wamachinga ambao wanapigwa mabomu kila wakati,” alisema Wenje na kuongeza.

“Kuna kila sababu ya kutafuta haki kwa njia mbalimbali. Andamaneni mpaka haki yenu ipatikane."


Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi alisema Wamarekani wana msemo kuwa anayehifadhi magaidi naye ni gaidi, hivyo wasanii wanazunguka na CCM na kuimba kuwa nchi hii ina amani nao ni wasaliti.

Mbunge wa Kawe, Halima Mdee alisema pamoja na kuwa jimbo lake linakaliwa na vigogo wote wa nchi hii, lakini mwaka jana walifikia hatua ya kuikataa CCM.

“Kama Kawe wamesema CCM baibai inakuwaje ninyi watu wa Mara. Nawaambieni kuwa mwaka 2015 majimbo yote saba yanatakiwa yachukuliwe na Chadema na kuingia Ikulu, maana sisi tumewaahidi kupambana na ufisadi mpaka mwisho," alisema.

Utetezi wa Mbunge Lema

Dk Slaa alizungumzia pia kitendo cha Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema kutakiwa kuwasilisha ushahidi kwa madai yakuwa kuwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda alidanganya bungeni hivi karibuni.

Dk Salaa alisema kuwa tayari amewasilisha ushahidi na kwamba unaonyesha wazi kuwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda alidanganya mara 23 bungeni kuhusiana na suala la mauaji ya Arusha.

“Spika aliomba ushahidi Lema kapeleka, lakini kwa sababu alitaka kumlinda Pinda akasema kuwa ushahidi huo upelekwe kwake.

"Lema ameitwa muongo hadharani na ushahidi aliowasilisha umebainisha Pinda ndiye alidanganya mara 23, sasa tunataka apewe nafasi hadharani bungeni auseme ushahidi wake katika kikao cha bunge lijalo Aprili,” alidai Slaa.

No comments:

Website counter