Wednesday, January 26, 2011

KWA MTAJI HUU SOKA LA 'BONGO' HALIWEZI KUENDELEA KAMWE!

Yanga yamwaga Ugali Papic amwaga mboga Jangwani Send to a friend


KOCHA wa Yanga, Kostadin Papic


KOCHA wa Yanga, Kostadin Papic jana alitangaza rasmi kukatiza mkataba wake wa kuifundisha klabu hiyo kwa kukabidhi barua kwa uongozi akiwa amebakiza miezi kabla ya kumalizika mkataba wake Aprili mwaka huu.

Hatua ya Papic kutangaza kujiondoa rasmi kuinoa Yanga inafuatia wiki kadhaa za marumbano kati yake na uongozi wa klabu hiyo hasa baada ya viongozi wao kutangaza kumwajiri aliyekuwa kocha mkuu wa Ruvu Shooting, Fredy Felix Minziro.

Awali kabla ya Papic kuiambia Blogu hii juu ya uamuzi wake huo kulikuwa na kikao baina yake na uongozi wa Yanga uliofanyika jana kwenye hoteli ya Movenpick jijini Dar es Salaam kuanzia majira ya saa 4 asubuhi hadi saa 6 mchana.

Mapema kabla ya kufikia uamuzi huo Papic aliiambia Blog hii ya KINYAIYA muda mchache kabla kuikabili Polisi Dodoma katika mechi ya ligi kuwa kitendo cha uongozi wa Yanga kumwajiri Minziro kuwa msaidizi wake bila ridhaa yake ni dharau kubwa hivyo hataweza tena kuifundisha timu hiyo.

Akizungumza na baada ya kumalizika kikao kati yake na uongozi wa Yanga, Papic alisema,"Kama nilivyosema awali kuwa nitaondoka hivyo natangaza rasmi mkataba wangu na Yanga umekwisha.

"Sitaweza kuongea mengi zaidi muda huu kwani nimechoka isipokuwa jambo la msingi na ambalo ninaweza kueleweka ni kwamba nimejiuzuru.

"Kuna vitu vichache tu vya kumalizana nao pamoja na kushughulikia tiketi na Jumatatu nitaondoka kurudi Serbia,"alisema Papic.

Wakati huo huo, Uongozi wa Yanga umezidi kukaliwa kooni kwa kutakiwa kufanya ukaguzi wa mahesabu baada ya kugundulika kuwa kuna baadhi ya wachezaji wamesaini mikataba miwili.

Habari ambazo Blogu hii imezipata zinasema kuwa mfadhili wa klabu hiyo Yusuf Manji ameendelea kuusisitiza uongozi chini ya Lloyd Nchunga kutaka ukagazi wa mahesabu ufanyike haraka ikiwa ni pamoja na kuwepo wa uwazi wa mapato na matumizi ndani ya klabu hiyo.

Chanzo hicho kimesema hatua hiyo imekuja baada ya kugundulika kuwa kuna baadhi ya mikataba ya wachezaji wa Yanga imechakachuliwa kwa kuandikwa miwili miwili huku ile inayopelekwa kwa mfadhili wao ikiwa na fedha nyingi.

"Unakuta mkataba aliopewa mchezaji una fedha ndogo, mfano ni Omega Seme mkataba wake ni milioni 5, lakini uliopelekwa kwa mfadhili wetu ni milioni 13, sio yeye tu wapo wachezaji wengi wamefanyiwa hivyo,"kilisema chanzo hicho.

"Nchunga (mwenyekiti) amekuwa mstari wa mbele kutaka mahesabu yakaguliwe, lakini kuna baadhi ya viongozi hawataki na ndio maana wamekuwa wakitofautiana kwenye vikao vyao vya kamati ya utendaji."

Mwaka 2008 wanachama wa klabu ya Yanga walitaka ufanyike ukaguzi wa mahesabu kufuatia shilingi milioni 150 za kadi za wanachama kutafunwa na pia shilingi bilioni 1 kutumika ndani ya siku 100 hivi karibuni kitu ambacho kinazidisha mashaka kwa viongozi wa klabu hiyo na kutakiwa kufanya ukaguzi wa mahesabu.

Katika hatua nyingine Yanga jana ilitangaza viingilio vya mpambano wao wa kimataifa wa kombe la Shirikisho kati yao na Dedebit ya Ethiopia utakaopigwa Januari 29 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Afisa habari wa Yanga, Louis Sendeu alivitaja viingilio hivyo kuwa ni Sh 3,000 kwa jukwaa la viti vya rangi ya bluu na kijani, Sh 5,000 kwa jukwaa la viti vya rangi ya machungwa huku wale watakaokaa Jukwaa la viti maalumu A watalipa Sh 20,000 na viti maalum B ni Sh 10,000.

Aidha alisema kuwa kikosi cha timu ya Dedebit kitawasili nchini kesho huku akiwataja waamuzi wa mpambano huo kuwa ni Abd Elgdir (kati) na wasaidizi wake ni Mohamed El Tour na Al Saeed Salim wakati kamisaa ni Line Kila Hafen.

No comments:

Website counter