
Viongozi wa Chadema wakiwa katika maandamano jijini Arusha
POLISI mkoani Arusha, jana lilimwaga damu za watu kadhaa, walioshiriki na wasioshiriki maandamano yaliyoandaliwa na Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
Risasi za moto na mabomu ya machozi vilitumika katika jitihada za polisi kuzima maandamano ya Chadema, wakitekeleza amri ya Mkuu wa Jeshi hilo, Ispekta Jenerali Saidi Mwema.
IGP  Mwema alitangaza kuyapiga marufuku maandamano ya Chadema akibainisha  kwamba taarifa za kiintelijensia zimebaini kwamba kungekuwa na vurugu  wakati wa kufanyika kwake.
"Maandamano hayo ni marufuku, lakini  wanaruhusiwa kufanya mkutano wao wa hadhara. Kuna taarifa za  kiintelijensia kwamba kunaweza kutokea fujo na uvunjifu wa amani,”  alisema IGP Mwema alipozungumza na waandishi wa habari juzi jioni.
Awali  Chadema iliruhusiwa kufanya maandamano hayo yaliyoandaliwa kushinikiza  taratibu zifuatwe katika uchaguzi wa wenyeviti au mameya wa halmashauri  nchini.
Maandamano hayo pia yalilenga kuwahamasisha wananchi wa  mkoa wa Arusha na mikoa jirani kushiriki kutoa maoni yao bila woga juu  ya kuandikwa upya katiba ya nchi, pindi kamati itakapoanza kazi.
Maandamano  hayo yalipangwa kuwashirikisha wabunge wote wa Chadema, na yalipangwa  kuanza jana saa 4:00 asubuhi na kuishia kwenye viwanja vya NMB mjini  Arusha ambako mkutano wa hadhara ungefanyika.
Kamanda wa polisi  mkoa wa Arusha, Thobias Andengeye juzi aliruhusu maandamano hayo lakini  akasisitiza kwamba jeshi lake litatoa ulinzi ili kuhakikisha yanakuwa ya  amani.
"Tumekubali maandamano na mkutano wa Chadema lakini  tunaomba wafuate taratibu na wahakikishe  hakuna uvunjifu wa amani ambao  unaweza kutokea," alisema Andengenye.
Hata hivyo baadaye juzi jioni IGP Mwema, aliitisha mkutano na waandishi wa habari jijini  Dar es Salaam na kutangaza kuyafuta.
IGP  Mwema aliwaeleza waandishi wa habari kuwa ameamua kufuta kibali cha  maandamano hayo kutoka na kupata taarifa za kiintelijensia kwamba  “kungetokea vurugu”.

Mchumba wa Katibu mkuu wa Chadema Dk Willibrod Slaa Josephine Mushumbusi akiwa anavuja damu baada ya kupata kipigo kutoka kwa polisi eneo la tanki la maji jijini Arusha akiwa kweye maandamano jana.
Na walipojaribu kufanya maandamano hayo polisi ilianza kutumia risasi za moto na mabomu ya machozi kuwatawanya waandamanaji hao uamuzi ambao ulifanya watu kadhaa wakiwamo wabunge wa Chadema kujeruhiwa vibaya.
Hadi jana jioni zaidi ya watu kumi, akiwepo mke wa Dk Slaa, Josephine Mushumbusi, walijeruhiwa kwa kipigo huku watu wengine watatu, wakiwa wako hoi baada ya kupigwa risasi za moto.
Wakati watu hao wakiumizwa kwa vipigo, mali kadhaa ikiwamo gari la mbunge wa viti maalum mjini moshi, Grace Kiwelu viliharibiwa.
Mwenyekiti wa  Chadema, Freeman Mbowe pia alikumbwa na dhoruba pale alipojikuta  akitumbukia kwenye mtaro wa maji machafu na polisi kumshabulia, wakati  alipokuwa akishiriki maandamano pamoja na wabunge kadhaa wa Chadema.
Wakati  hayo yakiendelea, shughuli zote katika mji wa Arusha zilisimamia huku  barabara kadhaa nazo zikifungwa tangu asubuhi kutokana na vurugu za  polisi na kamatakama ya watu iliyokuwa ikiendeshwa na jeshi hilo.
Vurugu  za polisi pia zilifika katika makazi ya watu na katika hospitali ya  wilaya ya Arusha ya Kaloleni ambako, wagonjwa kadhaa walizimia kutokana  na polisi kurusha mabomu ya machozi jirani na hospitali hiyo.
Daktari  za zamu wa hospiali hiyo, Anna Kimaro alielezea kushangazwa na hatua ya  polisi kurusha ovyo mabomu ya machozi jirani na hospitali.
Baadhi ya wagonjwa, Mwanaidi Mussa na Sabra Khalfani, walisema wamedhurika na hali hiyo kwani walipatwa na mshtuko.
“Mwanangu  alipoteza fahamu kabisa hadi sasa hajisikii vizuri,” alisema Sabra  alipozungumza na Mwananchi hosipitalini hapo, huku akiwa amebeba mtoto  wake Abdul Yusuph, mwenye umri chini ya mwaka mmoja.
Katika  vurugu hizo, pia baadhi ya waandishi wahabari walijeruhiwa kwa kupigwa  na polisi akiwepo mwandishi wa gazeti hili, Moses Mashala,mpiga picha wa  kituo cha televisheni cha Channel ten, Ashraf Bakari, mwandishi wa  kujitegemea wa BBC, Moses Kilinga na wengine kadhaa.
Kamanda  Andengenye hakupatikana jana kuelezea idadi kamili ya majeruhi kwani  polisi, waliwazuia wanahabari kufika kituo kikuu cha polisi huku  wakiwataka kuondoka eneo la kituo hicho katika muda dakika tano.
 
1 comment:
Tunaelekea kwenye true FREEDOM na mwisho wake ni kifo kwa mafisadi.
Post a Comment