|  
  Wafuasi  wa CUFwakiandamana Buguruni  jiji la Dar es Salaam jana kuelekea ofisi  ya Waziri wa Katiba na Sheria kuwasilisha Rasimu yao ya Katiba mpya.  Picha na Michael Jamson CHAMA  Cha Wananchi (CUF) jana kiliwazidi ujanja polisi waliokuwa wakidhibiti  maandamano yao baada ya kufanikiwa kuyafanya na kuwasilisha rasimu yao  sifuri ya katiba kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria.  Polisi  hao walikuwa wanazuia maandamano hayo kutekeleza agizo la Kamanda wa  Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam Suleiman Kova aliyolitoa juzi  kuzuia maandamano hayo kwa kile alichoeleza kuwa ni batili.
 
 Katika  maandamano hayo yaliyosimamisha kwa muda shughuli za kiuchumi na  kijamii, wafuasi na wapenzi wa chama hicho wakiongozwa na Kaimu Naibu  Katibu Mkuu wa CUF, Julius Mtatiro, walifanikiwa kuingia barabarani na  kuwasilisha rasimu yao ya katiba kama walivyopanga.  Hata hivyo  maandamano hayo yaliyoanzia Buguruni Sheli hayakuanza saa 2:00 asubuhi  kama yalivyopangwa kutokana na mvutano ulioibuka baina ya waandamanaji  hao na polisi wenye silaha ambao walifika ofisini hapo kuwadhibiti.
 
 Kabla  ya kuanza maandamano hayo, polisi waliwatangazia wananchi hali ya  hatari na kuwataka wajifungie majumbani mwao huku wakifyatua risasi za  moto na kurusha mabomo kuwatawanya.  Gazeti hili lilifika Buguruni Sheli  saa 2:00 asubuhi na kukuta eneo hilo limetapakaa askari wa kikosi cha  Kuzuia Ghasia (FFU) huku wengi wakiwa wamejipanga katika maeneo  mbalimbali ya barabara ya Uhuru kuwazuia waandamanaji.
 Ilipofika  saa 3:30 asubuhi lilipita gari la matangazo la CUF lenye  vipaza sauti  na ndani yake kulikuwa na mtu aliyekuwa akitangaza kuwa maandamano yapo  palepale na yataanzia Makao Makuu ya Chama, saa 4:30 asubuhi badala ya  Buguruni Sheli.
 Mara baada ya tangazo hilo, wananchi walianza  kukusanyika kwa wingi nje ya makao makuu ya chama hicho wakiwa na  mabango mikononi na vitambaa vilivyoandikwa ujumbe mbalimbali wa kudai  katiba mpya.  Baada ya mabadiliko hayo ya ghafla polisi waliamua  kuwafuata kwenye na kuwaonya, “Wanachama wa CUF, maandamano yenu ni  batili.
 
 Tafadhali fuateni sheria kuwasilisha madai yenu.”  Kauli  hiyo ya Dereva wa gari la Polisi aina ya Defenda aliyevalia sare za FFU  ilirudiwa mara tatu lakini, wanachama hao hawakusikia badala yake  wakaendelea na azma ya kutaka kuandamana huku wakiimba, “Chinja ua,  Katiba Lazima.”
 Tangazo hilo lilifuatiwa na tangazo la hali ya  hatari lililotangazwa na Dereva huyo ambaye alisema “Naomba wenye magari  ya kiraia mwende mbele, waandishi wa habari mwende mbele, wananchi  ingieni majumbani mwenu na wafanyabiashara fungeni biashara zenu,  tunataka kufanya kazi.”  Lakini licha ya tangazo hilo la hatari,  waandamanaji waliendelea kuimba na kusogelea magari hayo ya FFU zaidi ya  matano yaliyokuwa mbele yao.
 “Mara ya mwisho, narudia wananchi  wa CUF maandamano yenu si halali, fuateni sheria kuwasilisha madai  yenu,” alisema dereva huyo ambaye jina wala nambari yake haikujukana  huku wanachamahao hao wakimjibu, “Hamtufanyi lolote ninyi.
 
 Kama  ni mabomu na maji ya kuwasha tumezoea.”  Baada ya hapo magari hayo ya  polisi yaliyokuwa yamesheheni askari wenye silaha nzito za moto na  mabomu ya kutolea machozi, yaliondoka na kwenda kuegeshwa katika  makutano ya barabara ya Uhuru na barabara ndogo inayoingilia Makao Makuu  ya CUF eneo la Rozana.
 Baadaye waandamanaji walianza maandamano  na walipofika Rozana, magari ya polisi yaliondoka na kwenda kuegeshwa  katika kituo cha mabasi cha Buguruni Malapa, ambako gari maalumu la  kumwaga maji ya kuwasha maarufu kama deraya, lilikuwa limeegeshwa.   Baada ya kuona hivyo waandamanaji walijipa moyo na kuona labda polisi  wanawaogopa na hivyo kuingia moja kwa moja katika barabara kuu ya Uhuru  kuelekea mjini.
 Lakini, walipofika Malapa, walikumbana na  kizuizi cha magari ya polisi zaidi ya sita ya FFU na deraya nyingine.   Hapo ilikuwa kama mchezo wa kuigiza baina ya FFU na waandamanaji, baada  ya kila upande kumtunishia msuli mwingine. Wakati polisi wakiwataka  wanachama hao wasalimu amri na kusitisha maandamano yao, wanachama hao  wanajibu "Kuandamana ni haki yetu kikatiba."
 
 Wakiwa  wanatunishiana misuli katika kituo cha mabasi cha Malapa, gari moja la  FFU lilikaa katikati ya barabara na dereva wake alitangaza tena  “Tafadhali hili gari usilipite, ukilipita hili gari unatafuta shari.”    Lakini pamoja na tangazo hilo, wanachama hao waliendelea kulipita gari  hilo na mkuu wa operesheni ya polisi hao akaruhusu gari la maji ya  kuwasha kuanza kuwarushia maji.
 
 Wakati hayo yakiendelea,  daladala na magari yote yanayotoka na kwenda Buguruni yalikuwa yamezuia  kupita na kupaki pembeni ama kwa amri au kwa hofu yao wenyewe.  Baada ya  kuona kizuizi hicho waandamanaji hao waliamua kuingia mitaani na kwenda  kuibukia katika mitaa ya Amana na Ilala Boma na kuendelea na safari ya  kuelekea Wizarani. Wakati huo polisi walikuwa wameachwa Malapa.  Polisi  hao walisituka kwamba maandamano yanaendelea wakati waandamanaji hao  walipokuwa tayari wamefika eneo la Karume na Mchikichini.
 
 Maandamano  yalipofika kati ya mitaa ya Ilala Boma na Karume, polisi hao ambao  walikuwa tayari wameshajawa na hasira kwa mchezo wa sinema waliokuwa  wakichezewa na waandamanaji, waliamua kufyatua risasi za moto  kuwatawanya.  Pia mabomu kadhaa ya kutoa machozi yalilipuliwa katika  mitaa hiyo jambo ambalo lilisababisha waandamanaji hao kuanza kupoteza  mwelekeo huku baadhi ya viongozi wao, wakifanikiwa kupita kwa gari la  chama lenye bendera.
 
 Baadaye maandamano hayo yalifanikiwa  kufika ofisi za Wizara ya Katiba na Sheria ambako viongozi wa CUF  walikabidhi rasimu yao ya katiba.  Akizungumza baada ya kukabidhi rasimu  hiyo, kiongozi wa maandamano hayo Julius Mtatiro alisema maandamano  yalikuwa halali na kwamba licha ya kupigwa mabomu na kutishwa kwa risasi  za moto, wamefanmikiwa kufikisha ujumbe kwa serikali na wadau wote wa  katiba.
 
 “Tumefanikiwa kufikisha ujumbe wetu ingawa maandamano  yetu yalikatiswa na polisi hali ambayo inaonyesha wazi ubakaji wa  demokrasia nchini kwani maandamano ni haki ya kikatiba ya kila raia,”  alisema Mtatiro.  “Tumekabidhi rasimu yetu sifuri ya katiba wizarani,  ingawa waziri hatukumkuta lakini tunashukuru imepokewa na katibu mkuu wa  wizara hiyo,” aliongeza Mtatiro.  Hata hivyo katika makabidhiano ya  rasimu hiyo, waandishi wa habari hawakuruhusiwa kuingia ndani ya ofisi  na kushuhudia.
 
 Mwisho    Juzi Kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar es  Salaam Al-hajji Suleiman Kova aliwaeleza wanahabari kuwa maandamano  hayo ya Chama Cha Wananchi (CUF), ameyazuia na kwamba ni batili, huku  kwa upandeo wao CUF kupitia Mtatiro wakisisitiza kutimiza azma ya  kuandamana hadi kwa Waziri Kombani na kumkabidhi rasimu hiyo.
 
 | 
1 comment:
Hahaha, wamewaweza kweli, ila siku nyingine msizoee ,mtapigwa mabomu ya moto
Post a Comment