Tido Mhando atemwa TBC | Send to a friend |
|
BAADA ya kufanya kazi nzuri ya kuboresha matangazo na uendeshaji wa Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC), serikali imeamua kuachana na mkurugenzi wa chombo hicho, Tido Mhando baada ya mkataba wake kuisha, lakini mtangazaji huyo maarufu ameielezea uamuzi huo kuwa kuwa ni wa utata. Kuenguliwa kwake kumefanyika takriban miezi miwili baada ya kumalizika kwa uchaguzi mkuu ambao TBC iliripoti kwa kina na bila kupendelea chama chochote na hivyo kujivunia sifa kemkem kutoka kwa watazamaji wa TBC1 na wasikilizaji wa redio hiyo ya umma. “Barua ya kutakiwa kuondoka niliipata mara baada ya kukutana na kuzungumza na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Michezo, Utamaduni na Vijana , Seti Kamwanda.’’ "Kimsingi (barua) hukumbusha kwamba mkataba unamalizika na kama serikali inakusudia kuuendeleza au la. Sasa hilo halikufanyika kwangu," alisema. Kwa mujibu wa Tido, hatua hiyo inaweza kutafsiriwa tofauti na wananchi hasa ikizingatiwa kwamba imefikiwa miezi miwili tu tangu kumalizika kwa uchaguzi mkuu. Wafanyakazi walipata taarifa ya kuondolewa kwa Mhando jana baada ya mkurugenzi huyo kubandika tangazo la kuwataarifu kuwa anaondoka na kwamba ametakiwa akabidhi ofisi kwa Joe Rugabaramu. Mfanyakazi mwingine alisema kuwa walitarajia kuwa Mhando angetimuliwa mapema kabla ya uchaguzi kwa kuwa wanadai kuja kwake nchini kulitokana na uhusiano wake na kigogo mmoja wa CCM ambaye kwa sasa hayuko madarakani. "Angetimuliwa hata kabla ya Desemba 15, lakini ikaonekana kuwa isingekuwa sahihi," alisema mfanyakazi huyo ambaye alieleza kuwa Mhando aliwasiliana pia kwa simu na mfanyakazi mmoja mmoja kumuelezea uamuzi huo wa serikali. Habari za Tido kuondoka TBC zilianza kuvuma wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu wakati iliposemekana kuwa alikuwa akipigana vijembe vya chinichini na vigogo wa CCM kutokana na vyombo hivyo vya umma kutangaza habari bila ya upendeleo. Baadhi ya mambo yaliyoibua hisia kuwa mtendaji huyo wa shirika la umma angeondolewa ni msimamo wake wa kuendelea kurusha hewani kipindi cha "Jimbo kwa Jimbo" ambacho kilikutanisha wagombea ubunge wa vyama mbalimbali vya siasa kwenye mdahalo kuhusu maendeleo ya eneo lao. Pamoja na CCM kujitoa, TBC iliendelea kurusha vipindi hivyo hadi kumalizika kwa uchaguzi ambao uliisha kwa CCM kupoteza viti vingi Tanzania Bara, ikiwa ni mara ya kwanza tangu serikali iruhusu mfumo wa vyama vingi. Chanzo kingine alisema: "Kuna watu wanaajiriwa pale TBC ambao malipo yao yanayotokana na Saccos ya shirika hilo, kitu ambacho ni kinyume na taratibu za serikali zinazotaka mwajiriwa alipwe na Hazina." Alipoulizwa endapo atakubali kurejee kwenye wadhifa huo ikitokea serikali ikamwita tena, Mhando alijibu: "Nitalazimika kuchukua muda zaidi kutafakari hilo kwa kina. Kuhusu utendaji wa shirika hilo, Tido alisema amefarijika kwa kiasi kikubwa na mafanikio ya kiutendaji yaliyofikiwa. Mbali na kurusha taarifa za kampeni katika njia iliyoonekana kuwa si ya upendeleo hata kwa chama tawala, TBC ilifanikiwa sana katika urushaji wa moja kwa moja wa matangazo ya mechi za mpira wa miguu na matukio makubwa ya kisiasa na kijamii. Mechi za michuano mbalimbali ya kimataifa na ya ndani, urushaji wa matangazo ya moja kwa moja ya vikao vya Bunge, urushaji wa moja kwa moja wa matukio makubwa na staili ya utangazaji ulilifanya shirika hilo kuwa na mvuto mpya na hivyo kuweza kupambana na vituo vingine vya redio na televisheni vya kampuni binafsi. |
No comments:
Post a Comment