
AG frederick Werema
MSIMAMO wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Frederick Werema alioutoa juzi kwamba serikali inatakiwa kuilipa kampuni ya kufua umeme ya Dowans Tanzania Ltd fidia ya Sh 185 bilioni umepingwa vikali na baadhi ya wasomi, wanazuoni na wanasaisa nchini.
Kadhalika baadhi ya watu  wa makundi hayo tofauti waliozungumza na Mwananchi jana walisema Jaji  Werema hana mamlaka ya kutangaza kufungwa kwa mjadala, huku wakihoji ni  nani aliyempa mamlaka hayo na kwamba ana maslahi gani katika kampuni ya  Dowans.
Ulipaji wa fidia hiyo unafuatia uamuzi uliotolewa na  Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Migogoro ya Biashara (ICC Court),  Novemba 15, mwaka huu chini ya Mwenyekiti Gerald Aksen na wasuluhishi  Swithin Munyantwali, Jonathan Parker ukiamuru Tanesco iilipe Dowans  kiasi hicho cha fedha.
Akizungumza juzi katika  viwanja vya Ikulu jijini Dar es Salaam mara baada ya kuapishwa kwa Jaji  Mkuu mpya, Mohamed Chande Othman, Werema alisema mjadala kuhusu Dowans  umefungwa rasmi na kwamba hakuna mpango wa serikali kukata rufaa. Kauli  hiyo ya Jaji Werema ni kama imefuta ndoto za Shirika la Umeme Tanzania  (Tanesco) ambalo lilionyesha nia kwamba lingechukua hatua za kukata  rufaa baada ya uamuzi wa ICC kusajiliwa rasmi katika Mahakama Kuu  nchini.
Kadhalika kauli hiyo ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali  ina uelekeo wa kupinga na na ile iliyotolewa na Waziri Mkuu, Mizengo  Pinda aliyewaambia wahariri wiki moja iliyopita kwamba kulikuwa na  mchakato wa kuangalia uwezekano wa serikali kukata rufaa dhidi ya uamuzi  huo wa ICC.
Jaji Werema katika maelezo yake alikwenda mbali  zaidi akiwabeza wale waliowahi kutoa kauli za kupinga kulipwa kwa Dowans  kwa kusema kuwa “Kwa hukumu hii siwezi kusema tutalivalia njuga suala  la Dowans maana kwa hukumu hii hata ukiivalia hiyo njuga itafikia mahala  njuga hizo zitakatika tu”.
Ni kutokana na kauli hizo tata na  nyingine, baadhi ya wananchi wamehoji kile walichokiita utetezi wa  Mwanasheria Mkuu kwa kampuni ya Dowans, huku wengine weakidai kwamba  huenda ana maslahi katika kampuni hiyo.
Katibu Mkuu Chama cha  Chadema, Dr Willbroad Slaa amemtaka Jaji Werema kujiuzulu kutokana na  kuweka wazi kwamba serikali itailipa fidia kampuni ya Dowans Tanzania  Ltd.  Dk Slaa ambaye aliibua mjadala mzito kuhusu kampuni hiyo katika  vikao vya bunge mjini Dodoma wakati akiwa mbunge wa Karatu , jana  aliliambia gazeti hili kwamba kauli ya Jaji Werema inaonyesha jinsi  Tanzania ilivyo kichwa cha mwendawazimu.  "Dowans wameingia nchini kwa  utaratibu ambao mpaka leo haujajulikana na kurithi mitambo ya Richmond,  mitambo ambayo tulizungumza sana kwamba imeingia kwa njia za kifisadi,"  alisema Dk Slaa,  Aliongeza, " Tuhuma za kampuni hii zilikuwa nzito,  zimewekwa wazi lakini serikali haijachukua hatua yoyote, kesi hii mpaka  imekwenda mahakamani hakuna lolote la kueleweka,".
Alisema kuwa  kitendo cha serikali kukubali kuilipa Kampuni ya Dowans kina maana  kwamba fedha zitakazolipwa kwa Kampuni hiyo ni za Watanzania na  kufafanua kwamba serikali inalipa deni lisilowahusu.  "Kauli ya Jaji  Werema inaonyesha kwamba yeye na serikali ni wazembe, utatoaje idhini  bila kuchunguza jambo husika, kuliko kutoa kauli hii alitakiwa kujiuzulu  tu," alisema Dk Slaa.  "Nchi hii inaendeshwa vibaya, serikali haiko  makini inaipeleka Tanzania sehemu mbaya,".  Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha  Dar es Salaam, Profesa Abdallah Safari alisema umefikiwa wakati serikali  ikaweka wazi nani ni mmiliki wa Dowans na kuacha kuwaadaa Watanzania.
"  Jaji Werema anashindwa nini kuwataja wamiliki wa Dowans, hapa tatizo  liko wapi......., mikataba hii iliyojaa rushwa imeibua mijadala mikubwa  nchini, sasa ili kuweka mambo sawa watueleze nani mmiliki wa Dowans na  serikali inamlipa nani,' alisema Profesa Safari  Kwa upande wake Mbunge  wa Kigoma Kusini kupitia NCCR Mageuzi, David Kafulila ambaye hivi  karibuni alitangaza kusudio lake la kupeleka hoja binafsi katika Mkutano  wa Pili wa Bunge, Februari mwakani kutaka serikali iwajibike kwa  kuliingiza taifa hasara kwenye sekta ya umeme, kutokana na hukumu ya  kesi ya Dowans alisema Jaji Werema “hana ubavu wa kufunga hoja ya  Dowans”.
"Hili suala mimi nimeshaliwasilisha bungeni bado  kupangiwa siku tu ya mjadala, hapo Werema au serikali haiwezi kuzuia  mjadala uliopo bungeni," alifafanua Kafulila. Aliongeza, kuwa Jaji  Werema hawezi kufunga mjadala wa hasara ya Sh 185 bilioni na kuongeza  kwamba ni lazima aeleze uhalali wa kulipa deni hilo wakati tayari  ilishaelezwa mkatabahuo ulikuwa batili.  "Serikali imeshindwa kusema  hata mmiliki wa Dowans ni nani, sasa inakwenda kumlipa nani, mzimu au,  alihoji Kafulila. Alisema ana imani kwamba Spika wa bunge, Anne Makinda  atairuhusu hoja yake na kusisitiza kuwa ataweka mambo yote hadharani ili  umma wa watanzania ufahamu mbivu na mbichi kwa kuwa hauwezi kuumizwa na  madeni kwa mchezo wa serikali dhaifu.
Naye mhadhiri wa chuo  hicho katika Shule ya Sayansi ya Siasa na Uongozi wa Umma, Dk Bashiru  Ally, alisema inasikitisha kuona mwanasheria mkuu akitoa msimamo kama  huo, wakati ofisi yake inahusika na kuisababishia serikali hasara ya  bilioni ya fedha kutokana mikata mibovu ambayo serikali imekuwa  ikiingia.
Ally alisema takribani kipindi cha miaka 20, ofisi  hiyo imekuwa ikingia mikataba mbalimbali ambayo badala ya kuwa na tija  kwa taifa imekuwa ikisababisha hasara za mabilioni ya fedha. “Werema  amerithi ofisi inayonuka rushwa, kwa kipindi kifupi tangu akae katika  ofisi hiyo, bado hatujaona juhudi zozote za kusafisha uchafu huu, na  vizuri Werema mwenyewe anayajua vema haya kwasababu amekulia katika  ofisi hiyo siyo mtu kutoka nje,” alieleza Ally. Alisema kupitia ofisi  hiyo, kwa muda huo wa miaka 20 sekta ya madini na nishati kupitia  mikataba mibovu inayobarikiwa na ofisi hiyo, imeongoza kwa  kulisababishia taifa hasara kubwa.
Ally alitaja baadhi ya  mikataba hiyo kuwa ni pamoja na ule wa Kaumpuni ya kufua umeme ya IPTL,  Richmond, ununuzi wa Rada na Dowans. “Sasa suala siyo kuangalia kama  tulipe ama tusilipe hizo fedha kwa Dowans, ikumbukwe katika nafasi yake  ofisi ya mwanasheria mkuu lazima nao walihusika kutoa ushauri wakati wa  kesi hii, kwa hiyo jambo la msingi kufahamu Tanzania hatujawahi kuwa na  mwanasheria wa serikali anayeweza kusimamia maslahi ya umma,” alisema  Ally.
Mbunge wa Kigoma Kaskazini kupitia Chadema, Zitto Kabwe  yeye alisema wanasiasa lazima wawajibike katika mjadala wa Kampuni ya  Dowans kwa kuwa siasa ziliingia kuanzia kutolewa kwa zabuni hadi  kuvunjwa kwa mkataba.  Zitto alisema kuwa anaisubiri hoja ya Kafulila  kuhusu umeme ili aweze kuzungumzia Dowans na kutoa maoni yake.  "Suala  la msingi hapa ni kujua je ni sawa kulipa Dowans? Bunge lilisema mkataba  si halali, mahakama imesemaje kuhusu hilo? Bunge lilisema kampuni ni  feki, mahakama imesemaje? Alihoji Zitto.
Alisema kuwa Sh 185  bilioni ni fedha nyingi sana kulipa bila kupata majibu hayo kwani fedha  hizo zina uwezo wa kuweka lami kwenye barabara ya kimometa 200 kama  Manyoni-Tabora.  "Sakata zima lilijaa siasa na ndo maana tuko  hapa,"alisema Zitto.
Kauli ya Zitto inaungwa mkono na ile ya  Mkurugenzi wa Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD), Dk Benson Bana  amesema serikali ikate rufaa,ili kujiridhisha kama kweli kampuni ya  Dowans inastahili kulipwa kiasi hicho cha fedha. "Hizi ni fedha za  walipakodi, tusikurupuke kulipa kabla hatujajiridhisha bila kuwa na  shaka kwamba kampuni ya Dowans inastahili kiasi hicho cha fedha,"  alisema.
Alisema inasikitisha kuona wananchi wanayumbishwa na  viongozi wasiojua madhara ya maamuzi wanayoyachukua. "Baadhi  walishangilia wakati mkataba wa Dowans na Tanesco ulipovunjwa, viongozi  walitumia nafasi ya kuvunjwa kwa mkataba huo ili kukamilisha malengo yao  ya kisiasa, sasa ni zamu ya kodi ya wananchi kulipa deni hilo,"  alisema.
Naye Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa Chadema Makao  Makuu Erasto Tumbo alimshukia Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kueleza  kuwa mjadala wa Dowas umefungwa kilichobaki kulipa deni hilo akihoji ana  maslahi gani na kampuni hiyo. Alisema hoja iliyopombele ya Watanzania  kwa sasa ni kujua nani mmiliki wa kampuni na pia kuona serikali inakata  rufaa kama alivyowahi kubainishwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.
“Huyu  Warema ni nani hata atuambie Watanzaia mjadala huo umefungwa,ana  maslahi gani na kampuni ya Dowans, naomba akae kimya awaache Watanzania  wamjue mmiliki wa Kampuni hiyo inayotaka kuchota mali za  Watanzania”alisema Tumbo.
Imeandaliwa na Fidelis Butahe, Hussein Issa, Boniface Meena, Fredy Azzah, Raymond Kaminyonge  na Geofrey Nyang'oro
 
No comments:
Post a Comment