Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe MBUNGE wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe ambaye jana aliruhusiwa kutoka katika Hospitali ya Aga Khan ya jijini Dar es Salaam alikolazwa kwa matibabu ya tumbo amedai kuwa matatizo hayo aliyapata baada ya kula chakula chenye sumu.“Namshukuru Mungu naendelea vizuri na nimesharuhusiwa kutoka hospitali, madaktari wameniambia ilikuwa food poisoning (chakula chenye sumu),” alisema Zitto.
Zitto ambaye hakuweza kueleza chakula hicho alikuwa wapi na kina sumu ya aina gani, alisema kuwa baada ya kugundua tatizo hilo, madaktari walimtaka kuwa makini na vyakula anavyokula.
“Sumu gani nimekula na ni wapi, mimi nadhani sio story (habari). Cha msingi kwa sasa naendelea vizuri na nimetakiwa kuwa makini na vyakula ninavyokula,” alisema Zitto.
Hata hivyo, kauli hiyo ya Zitto inapingana na madaktari wake waliosema kuwa mbunge huyo kupitia tiketi ya Chadema, alikuwa anasumbuliwa na mchafuko wa kawaida wa tumbo.
“Alikuwa anasumbuliwa na Gastro enteritis (mchafuko wa tumbo), tatizo hili linaweza kusababishwa na bacteria, virusi katika chakula, au kama chakula hakijapikwa vizuri,” alisema Dk Mustafa Bapumia.
Zitto alilazwa hospitalini hapo tangu Disemba 9 mwaka huu saa 3:00 usiku, baada ya kutoka kwenye mkutano wa ndani wa chama chake uliofanyika Bagamoyo mkoani Pwani ambako alivuliwa cheo cha Naibu Kiongozi wa Kambi ya upinzani bungeni.
Kuhusu hatua ya chama hicho kumvua Zitto wadhifa wake wa unaibu kiongozi wa upinzani bungeni, alisema kwa sasa bado hawezi kuzungumzia suala hilo kwa sababu hajapata taarifa rasmi kutoka chama chake mbali na kusoma suala hilo kwenye vyombo vya habari.
Hata hivyo, alieleza hakuwahi kuomba kupewa wadhifa huo, kwa hiyo endapo watu waliomwona anafaa kufanya kazi na kumpa wadhifa huo, wakiamua kumnyang’anya siyo tatizo kubwa kwake.
“Kwa sasa nadhani suala la afya yangu ndiyo muhimu zaidi. Ngoja kwanza nitoke hapa na afya yangu iimarike na kama kutakuwa kuna sababu ya mimi kuzungumza nitazungumza,” alisema Zitto:
“Lakini ikumbukwe kuwa mimi sikuwahi kuomba wadhifa huu…, kwa hiyo kama watu walionipa wameamua kunibadilishia, mimi sidhani kama kuna tatizo.”
Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe aliupolizwa na Mwananchi Jumapili juu ya Zitto kuvuliwa uongozi bungeni alisema kuwa chama kitatoa taarifa baadaye.
Katika hatua nyingine Mbunge wa Mpanda Mjini, Said Amur Arfi aliyekuwa amelazwa katika Hospitali ya Aga Khan ya jijini Dar es Salaam, amesafirishwa kwenda India kwa matibabu zaidi.
Arfi aliliambia Mwananchi Jumapili kuwa madaktari waliokuwa wakimtibu wamemwambia kuwa mfuko wake wa nyongo una mawe hivyo anahitaji kufanyiwa upasuaji.
“Nilikuja hapa kwa sababu nilikuwa nasumbuliwa na maumivu makali ya tumbo, nilitoka Mpanda Disemba 2, mwaka huu kuja kwenye semina lakini kutokana na maumivu ya tumbo nilienda Hospitali ya Regency na baada ya kupigwa ultrasound nilielezwa kuwa nina tatizo la uvimbe kwenye maini,” alisema Arfi.
Alisema alivyokwenda katika Hospitali ya Aga Khan alielezwa kuwa ana tatizo jingine la mawe kwenye mfuko wa nyongo na kuwa inabidi afanyiwe upasuaji.
“Naishukuru serikali kupitia ofisi ya Bunge kunipeleka India kwa matitabu zaidi,” alisema Arfi.
Hata hivyo, alisema bado hajaelezwa hospitali anayokwenda kutibiwa na kuwa, taarifa zote hizo anazo muuguzi wa serikali atakayesafiri naye. Wakati huohuo, Mtangazaji wa Televisheni ya Channel Ten, Cyprian Musiba, anadaiwa kuwekewa sumu kwenye chakula na kufanya alazwe hospitalini kwa matibabu.
Musiba alilazwa katika kituo cha Afya cha Ebrahim Haji kilichopo jijini Dar es Salaam juzi mchana akiwa hajitambui.
Mmoja wa madaktari wa hospitali hiyo, Dk Ramadhani Ali aliliambia Mwananchi Jumapili kuwa Musiba alifikishwa katika hospitali hiyo akiwa anasumbuliwa na tumbo lakini, baada ya kupata matibabu, afya yake iliimarika na jana mchana aliruhusiwa kutoka hospitalini.
“Anaendelea vizuri kwa kweli na amesharuhusiwa” alisema Dk Ali huku akisita kueleza tatizo la lililokuwa linamsumbua Musiba.
Mke wa Musiba ambaye hakujitambulisha alisema kuwa kabla ya Musiba kuruhusiwa mmoja wa madaktari wa HospitaliI hiyo waliwaeleza kuwa Musiba alikula sumu iliyokuwa katika chakula.
“Tumeruhusiwa muda si mrefu ila daktari amesema Musiba alijisikia vibaya kwa kuwa alikuwa amekula sumu iliyokuwa katika chakula,”alisema mke wa Musiba.
Musiba ambaye mara nyingi hutangaza habari za michezo na burudani aliliambia Mwananchi Jumapili kuwa juzi hali yake ilikuwa mbaya na kuongeza kuwa alipelekwa katika hospitali hiyo kwa ajili ya matibabu.
“Hali yangu ilikuwa mbaya sana nilikuwa wa kufa tu ndugu yangu, ila namshukuru mungu naendelea vizuri, ila daktari hapa hospitali amenieleza kuwa nilikula sum,” alisema Musiba.
Habari zaidi zilidai kuwa Musiba alianza kupata matatizo ya tumbo saa kadhaa baada ya kula chakula katika hoteli moja iliyopo karibu na ofisi za Channel Ten.
|
No comments:
Post a Comment