Saturday, November 6, 2010

JAMANI SIKIENI KILIO CHA DADA YETU HUYU....

Habiba: Saratani ya jicho imenikatisha tamaa ya kuishi Send to a friend


Habiba Hamis MkumbaNAMKUTA akiwa amejiinamia huku ameshikilia kichwa chake, anahangaika, anakaa kila mkao, mara alale mara achuchumae.
Wakati mwingine anapiga magoti huku akilia na kulalamikia maumivu makali ya kichwa ambayo anadai hayasimuliki.

Jicho lake la kushoto limefungwa bandeji lakini bado uvimbe mkubwa umejitokeza pembeni huku maji maji yakimwagika.
Kwa tabu anajitambulisha jina lake, anasema anaitwa Habiba Hamis Mkumba, aliyezaliwa miaka 35 iliyopita jijini Dar es Salaam akiwa ni mtoto wa nne kati ya saba wa familia yao.

Anaeleza kuwa, hakuwahi kufikiria kupata matatizo kama haya katika maisha yake kwani mateso anayoyapata, anadai hayaelezeki. Kifupi, amekata tamaa ya kuishi.

Kwa nini akate tamaa?, Habiba anasema amechoshwa na maradhi yanayomkabili ambayo yamemfanya akose raha maishani. Maradhi haya si mengine bali ni Saratani ya jicho.

Akieleza namna alivyoanza kuugua, Habiba anasema dalili za maradhi yake zilianza baada ya kupata uvimbe mdogo juu ya jicho lake la kushoto ambao aliuchukulia ni wa kawaida kabla ya kushauriwa kwenda hospitali.
“Kinyama kidogo tu kiliniota sehemu ya juu ya jicho, ambacho hakikuwa kikiniuma sana, lakini kilipozidi kukua nilishauriwa niende hospitali ya CCBRT nikafanyiwe uchunguzi.

Nikafika pale nikapata vipimo, wakanipangia tarehe ya kurudi kwa ajili ya upasuaji mdogo wa kuondoa kinyama hicho,” anasimulia safari ya mateso ilivyoanza mwilini mwake.
Mwanzoni hakujua kilichoisibu sehemu ile ya jicho na hata madaktari hawakuweza kumweleza mara moja nini hasa ilikuwa sababu ya uvimbe aliotakiwa kuutoa kwa kufanyiwa upasuaji.

Alifanikiwa kufanyiwa upasuaji na kupewa dawa. Maisha yakaendelea huku akiuguza jeraha la upasuaji kabla ya kupatwa na mshangao mwingine. Safari hii uvimbe mwingine mdogo ukajitokeza ila sasa ukawa chini ya jicho.Akalazimika kurudi hospitali kwa mara nyingine.
“Nilipomweleza daktari kuwa tatizo limejirudia tena safari hii chini ya jicho, nikachukuliwa vipimo na kuambiwa kuwa jicho langu halifai, inabidi ling’olewe mara moja kwani linaoza ndani kwa ndani, ” anaeleza na kuongeza kuwa majibu hayo yalimpa woga kiasi cha kumfanya akimbilie Hospitali Kuu ya Muhimbili kwa vipimo zaidi.

Majibu ya Muhimbili yakafanana na yale ya CCBRT, na bila ajizi mtaalamu wa Muhimbili akamweleza kuwa jicho lake lilikuwa limeoza, halifai tena kuwa jicho baada ya kuathiriwa na Saratani.

Habiba hakuwa na namna ila kukubali ushauri wa kitabibu wa kulitoa jicho lake.Hapa ndipo alipopoteza jicho lake, kiungo cha thamani kubwa katika mwili wa mwanadamu.
Jicho lilipotolewa aliambiwa aende hospitali ya Ocean Road kulikopelekwa vipimo vyake kwa uchunguzi zaidi. Hali ikawa bado tete kwake, jicho liliendelea kumsumbua na hatimaye akaamua kwenda Ocean Road kutafuta dawa.
“Nilipofika Ocean Road nikaambiwa nitaanzishiwa tiba ya mionzi ambayo kwa sasa nitapigwa kumi na tangu juzi nimeshaanza tiba hiyo lakini kichwa kinaniuma kupita maelezo siwezi hata kula na ninajisikia kutapika kila mara kwa sababu ya mionzi hiyo.”anasema.

Hivi ndivyo maisha ya Habiba yalivyo kwa sasa,amekuwa mwathirika wa Saratani ugonjwa ulioshika kasi kwa kiwango kikubwa nchini.
Katika kumbukumbu zake, Habiba haelewi nini hasa kilikuwa chanzo cha udhia aupatao sasa.Hata hivyo anasema, mwaka 2000 aliwahi kupigana na msichana mwenzake katika ugomvi ulioshuhudia akitiwa ngeu jichoni baada ya kuumwa meno na mwenzake.Je hii inaweza kuwa sababu? Habiba anahisi hivyo.

“Sijui kama nitapona, naumwa sana kichwa na nikipigwa hii mionzi inanivuruga tumbo. Sijisikii kula, nasikia saratani haina dawa zaidi ya tiba ya kutuliza tu, nahisi nitakufa tu,” hii ndiyo kauli yake ya mwisho kwangu aliyoitoa huku akibubujikwa na machozi.

Mama yake aitwaye Mwajuma Issa, anasema tangu binti yake akumbwe na maradhi hayo mwaka 2008, amekuwa mtu wa vilio hali inayompa simanzi kila amtazamapo.
“Tunatamani apate nafuu apone kwa sababu anakesha akilia na hataki kula, kila mara anazungumzia kufa, anatutisha mno. Hata hivyo Habiba ana maumivu makali nafikiri hata kuzungumza na wewe amejikaza, hawezi hata kutulia jinsi anavyosumbuliwa na kichwa,” anafafanua.

Akikumbuka zamani, anasema mwanaye alikuwa mrembo na mwenye afya tele ila sasa maradhi yanayomkabili yamempa muonekano tofauti ambapo wanaomjua tangu zamani hushindwa kuzuia machozi yao pale wanapomtia machoni.
Kwa uande wake, mtaalamu wa masuala ya saratani toka Uingereza, Dk James Pahneny anafafanua sababu na aina ya saratani hii ambayo imekuwa maarufu katika miaka ya hivi karibuni.

“Zipo aina tatu na zaidi za Saratani. Kitaalamu zinaitwa Intraocular Melanoma, Intraocular Lyphoma na Retinoblastloma. Aina hizi mara nyingi huanza katika mboni au pembeni ya jicho. Nyama, uvimbe au ukungu hujitokeza katika sehemu hiyo,” anafafanua.

Akieleza sababu za saratani hizi, anasema kwa watu wenye asili ya Uzungu, wengi hupata saratani aina ya Melonama kwa sababu ya kuwa na macho yenye mwanga mkali. Wengine wanaoweza kupatwa na ugonjwa huu ni watu wanaofanya kazi za kuchomea vyuma ambao huathiriwa na mionzi.

Sababu nyingine anazotaja ni mionzi ya jua, maambukizi ya VVU ambayo huharibu kinga ya mwili.
“Saratani inayotokana na VVU huitwa kitaalamu kwa jina la Kaposi Sarcoma.Huku watoto wadogo wakiathiriwa zaidi na aina iitwayo Retinoblastoma,” anaeleza.
Kuhusu hisia za Habiba, Dk Pahneny anakanusha kwa kusema, kung’atwa meno hakuwezi kusababisha saratani katika mwili wa binadamu.

2 comments:

Anonymous said...

kwa kweli story inasikitisha,serikali yetu ni ufisadi kwa kwenda mbele.angalau kungekuwa na vitengi maalum vya kusaidia watu kama hawa.ukiangalia,shida ni nyingi mno hujui umsaidie yupi umuache yupi,saratani nayo ni ugonjwa mbaya sana na wenye maumivu,hasa kwa tz,kupona ni chance ndogo mno.sikatai tz ukimwi upo,lakini kungekuwa na elimu nzuri kuhusu huu ugonjwa wa saratani,kwani saratani nyengine ukiiwahi unapona,wananchi wangepata elimu ya kutosha pengine ingesaidia

Anonymous said...

inasikitisha kweli,naungana na mdau hapo juu kungekuwa na vitengo maalum hasa vya kuhamasisha watu kucheki kabla ukiwahi saratani unapona ila ikishakuenea basi utachomwa mionzi tuu,panachomwa hapa,hapa panaoza mwisho kifo.

Website counter