|  
  Andrew ChengeTUHUMA  zilizotolewa na mbunge mteule wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge,  dhidi ya uongozi wa Bunge la Tisa uliokuwa chini ya Spika Samuel Sitta,  zimewachefua wasomi, wanasiasa na wananchi wa kawaida ambao kwa nyakati  tofauti wamesema mwanasheria huyo wa zamani wa serikali hakustahili  kutoa shutuma hizo kwa madai kuwa si msafi.
 
 Juzi, Chenge  aliitisha mkutano na waandishi wa habari kueleza sababu zilizomsukuma  kuwania kiti cha Spika wa Bunge la Muungano na "makandokando"  yanayozunguka jina lake na akatumia nafasi hiyo kumshambulia Sitta kuwa  aliongoza Bunge kinafiki, kizandiki na kwa lengo la kupakana matope na  kutaka mbunge huyo wa Urambo Mashariki aogopewe kama ugonjwa wa Ukimwi.
 Chenge,  ambaye amekuwa akihusishwa kwenye tuhuma kadhaa za ufisadi, ikiwa ni  pamoja na sakata la ununuzi wa rada, alisema akipewa kiti cha ubunge  atahakikisha anarejesha dhana ya wengi wape kwa kuwapa nafasi zaidi  wabunge wa chama tawala chenye wabunge wengi, lakini bila ya kuathiri  haki za wachache kutoa maoni yao.Lakini, badala ya ufafanuzi wake  kusafisha picha yake mbele ya jamii, kitendo hicho kimewachafua watu  wengi waliosoma taarifa za vyombo vya habari vikimkariri Chenge ambaye  alilazimika kujiuzulu uwaziri wa Miundombinu baada ya kutajwa kwenye  kashfa ya ununuzi wa rada.
 
 Katika kashfa hiyo, kitengo cha  uchunguzi wa makosa makubwa cha Uingereza, SFO kilibaini akaunti moja ya  Chenge iliyo nje ya nchi ikiwa na takriban Sh1.2 bilioni wakati  kikichunguza mzunguko wa fedha ambazo serikali ya Tanzania ilitoa  kununua rada. Uchunguzi huo ulikamilika Februari mwaka huu kwa kampuni  ya BAE System kukiri makosa ya kutotunza rekodi zake na kukubali kulipa  fidia.
 Chenge pia anatuhumiwa kuuingiza nchi kwenye mikataba mibovu  na makamapuni ya madini wakati akiwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali na  ununuzi wa ndege ya kifahari ya rais, mambo ambayo yamewafanya wananchi  wengi walioongea na gazeti hili kumshambulia mbunge huyo mteule wa  Bariadi Magharibi.
 
 Wakizungumza na Mwananchi kwa nyakati tofauti  jana na wengine kuandika maoni yao kwenye tovuti, watu wengi  walionyeshwa kuchukizwa na kauli hizo za Chenge wakisema kuwa bado ana  madoa mengi ya tuhuma za ufisadi ambayo anapaswa kujisafisha kabla ya  kushambulia wengine.
 Mwanasheria maarufu nchini, Profesa Abdallah  Safari aliizungumzia mashambulizi ya Chenge dhidi ya Sitta kuwa ni  ukosefu wa ustaarabu."Madai ya Chenge kwamba atatoa fursa zaidi kwa  wabunge wa CCM kwa sababu ni chama tawala, yanaashiria kuwa atakuwa na  upendeleo na hilo linamwondolea sifa kuu ambayo spika anatakiwa kuwa  nayo," alisema Prof Safari alipozungumza na Mwananchi kuhusu tamko la  Chenge.
 Harod Tairo, mhadhiri wa sheria kwenye Chuo Kikuu cha  Tumaini, alienda mbali zaidi na kuielezea mashambulizi ya Chenge kuwa  yanatoa taswira kwamba waziri huyo wa zamani wa miundombinu anataka kiti  hicho ili akalipize kisasi bungeni.Tairo alisema uongozi wa Sitta,  ambaye uongozi wake ulilifanya Bunge lake kuingia kwenye historia kama  chombo kilichotekeleza wajibu wake wa kuiwajibisha serikali, ulifanya  kazi kama ilivyostahili.
 “Pamoja na dhamira yake, anatumiwa na  wanaodhani hawakutendewa haki kwenye bunge lililopita; anatumiwa kulinda  maslahi ya wabunge mafisadi… angekuwa na nia ya kuutumikia umma,  angeeleza hoja zinazokubalika tofauti na alivyofanya,” alieleza Tairo.
 Mbunge  mteule wa Jimbo la Kilindi mkoani Tanga, Beatrice Shelukindo alisema  haungi mkono uamuzi wa Chenge kuingia kwenye kinyang’anyiro cha uspika  kwa kuwa anakabiliwa na kesi mahakamani. Hadi sasa Chenge anakabiliwa na  kesi ya kuendesha gari kizembe na kusababisha vifo vya watu wawili  jijini Dar es salaam na pia kuendesha gari akiwa na bima iliyoisha muda.
 Shelukindo,  mmoja wa wabunge waliojipambanua katika Bunge la Tisa kama mpambanaji  wa ufisadi, alisema pamoja na kuwa ni haki ya kila mbunge kuwania nafasi  hiyo, kuna mambo ya msingi ambayo hayana budi kuangaliwa kabla ya  kufikia maamuzi kama huo ili Tanzania isionekane kutofuata sheria katika  kutekeleza mambo yake.
 Kwa mujibu wa Shelukindo, Watanzania wa  leo ni watu wenye uwezo mkubwa wa kuelewa mambo na hawatawaelewa wabunge  iwapo watampitisha Chenge kuwa spika wakati anazungukwa na tuhuma za  ufisadi.
 “Watanzania wa leo sio wale wa juzi. Wanao uelewa mkubwa na  wanajua misingi ya sheria na wajibu wa vyombo kama Bunge. Sasa sisi  tukijifanya kumchagua eti kwa sababu ni wa wabunge, wananchi watavunjika  moyo na hawatatuelewa,” alisisitiza Shelukindo.
 Kuhusu madai ya  Chenge kuwa kulikuwa na ombwe la uongozi kwenye Bunge lililopita,  Shelukindo alisema mwanasheria huyo mkuu wa zamani hakustahili  kuzungumza maneno mengi kiasi kile kwa kuwa hakuna asiyefahamu kwamba  Bunge lililopita lilikuwa la vyama vingi hivyo lilipaswa kuendeshwa kwa  kanuni za kibunge na siyo kupendelea vyama.Mwanasiasa mkongwe  nchini, Peter Kisumo alieleza kukasirishwa na malumbano aliyoyaibua  Chenge hata kabla ya kuingia bungeni, akisema hiyo inatoa taswira mbaya  kuwa huenda akawa ni mtu wa kulipiza visasi.
 
 “Yoyote  atakayechaguliwa au hata kama wote hawatachaguliwa, mimi nafikiri si  sahihi kuanza kumsakama Spika aliyepita kwa sababu ukianza hivyo Bunge  linaweza kuwa forum (jukwaa) la kulipiziana visasi,” alisema Kisumo.
 Msomi  wa shahada ya uzamivu (Phd) kwenye Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine  (SUA), Gasper Mpehongwa alilisifia Bunge lililopita kwamba lilikuwa bora  na lenye uhuru wa kutosha kwa maslahi ya taifa.
 “Ninaposema lilikuwa safi namaanisha hata Spika alikuwa safi. Ningepewa nafasi ningemchagua tena (Sitta),” alisema Mpehongwa.
 
 Mwanafunzi  mwingine wa Phd chuoni hapo, akizungumza na Mwananchi kwa sharti la  kutotajwa jina gazetini, alisema Chenge ana nguvu ya fedha inayoweza  kumpatia kiti hicho na kwamba hilo likitokea, wengi wataumia.
 Mkazi  mmoja wa Moshi aliyejitambulisha kwa jina la Hussein Mfinanga alisema:  “CCM na serikali yake wasifikiri Watanzania ni mbumbumbu… tunafahamu  uadilifu. Sasa kabla ya kumpitisha Chenge watuambie sababu zilizomfanya  ajiuzulu ni zipi na kama sasa ametakasika.”
 
 Mfinanga  anayejihusisha na biashara ya huduma ya internet, alisema Chenge  alijiuzulu uwaziri wa miundombinu baada ya kuhusishwa na kashfa ya  ununuzi wa rada, hivyo hakupaswa kujitakasa mwenyewe bali vyombo vya  dola.
 Mfanyabiashara huyo alimsihi Rais Jakaya Kikwete na CCM  kutoingia katika mtego wa kutompitisha mtu mwenye sifa na uadilifu na  kuitaka Taasisi ya Makosa Makubwa Duniani(SFO) kutamka kama change ni  mtuhumiwa wao au la.
 
 Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyabiashara  Wenye Viwanda na Kilimo (TCCIA), Patrick Boisafi alisema Watanzania  wanaufahamu utendaji wa Chenge na wa Sitta hivyo wanaiachia CCM kuwaweka  katika mizani na kuwapatia mtu safi.
 “Tunafahamu Chenge ana haki ya  kikatiba kuwania nafasi hiyo, lakini shaka yetu inaegemea katika maneno  yanayosemwa juu yake… cha kujiuliza ni je sasa amesafishika? na ni  chombo gani kimemsafisha," alihoji Boisafi.
 
 Wakili mmoja wa  kujitegemea aliyeomba jina lake lihifadhiwe aliilaumu moja kwa moja  Takukuru kwa kulifanya suala la Chenge kuwa siri licha ya kuhojiwa na  kila Mtanzania.
 “(Takukuru) Wanaweza wakajitetea kuwa Chenge  anachunguzwa na SFO, lakini tuhuma nzito kama hiyo ya rada haiwezi  kuachiwa taasisi za kimataifa kana kwamba sisi hatuna uwezo...  tungeshirikiana nao,” alidai.Hata hivyo, Takukuru ilitoa taarifa  jana ikieleza kuwa uchunguzi wa SFO umebaini kuwa Chenge hakuhusika  kwenye sakata hilo. Taarifa hiyo haikufafanua sababu za Takukuru kutoa  ufafanuzi sasa wa jambo ambalo uchunguzi wake ulikamilika Februari mwaka  huu.
 Mwanasiasa mkongwe nchini na muasisi wa Chadema, Edwin Mtei  alishangazwa na hatua ya Chenge kuchukua fomu ya kuwania kiti hicho huku  na kuhoji uadilifu wa kada huyo akisema unatia shaka kutokana na  kukakabiliwa na tuhuma za kashfa mbalimbali za ufisadi. Mtei,  ambaye pia aliwahi kuwa gavana wa Benki kuu ya Tanzania (BoT), alisema  endapo chama chake (CCM) kitadiriki kumpatia wadhifa huo, nchi itakuwa  njia panda. ‘Hata mimi ndio nilikuwa nashangaa na wenzangu hapa na  tunajadili kuwa itawezekanaje mtu kama Chenge achukue fomu ya kuwania  kiti cha uspika na CCM wanamuangali tu. Huyu mtu ana tuhuma nyingi za  ufisadi... hii nchi tutaiweka pabaya sana,” alisema Mtei.Naye Profesa Mwesigwa Baregu alisema amestushwa kusikia CCM imempa fomu Chenge kugombea kiti cha spika.
 “Bunge  letu lina hadhi, haliwezi kuongozwa na Chenge… kwanza amalize tuhuma  zake kwenye mahakama mbalimbali na ile ya rada sijui aliifikisha wapi.  Nadhani anatafuta kujisafisha ila amekosea. Njia pekee ni yeye kukaa  kando,” alisema Prof Baregu ambaye ni mhadhiri wa Chuo Kikuu cha  Mtakatifu Agustino.
 Profesa Baregu alisema Sitta alisimamia Bunge kwa  kuzingatia kanuni na kwamba kama Chenge anamtuhumu kupendelea wabunge  wa upinzani, aeleze wabunge waliokaripiwa bungeni kwa kutozingatia  taratibu na kanuni za Bunge ikiwa ni pamoja na kuzuiwa kuhudhuria vikao  vya bunge, walikuwa wa kambi gani.
 Alisema kumbukumbu zinaonyesha,  John Cheyo (UDP) mwaka 2008 alikaripiwa na Sitta wakati wa kikao cha  Bunge kutokana na kukiuka kanuni na taratibu. Pia Zitto Kabwe (Chadema)  mwaka 2009 aliadhibiwa kwa kuzuiwa kuhudhuria vikao vya Bunge kwa miezi  mitatu kwa kilichoelezwa kukiuka taratibu za bunge.
 
 Kada mmoja wa  CCM aliyezungumza na gazeti hili kwa ombi la kutotajwa jina alisema  kauli ya Chenge ni miongoni mwa mikakati mingi inayolenga kuhakikisha  Bunge lenye msisimko kama lililopita, halitokei tena.
 “Leo ameibuka  Chenge na hizo kauli zake; kesho mtasikia wanaodai spika awe mwanamke.  Sioni sababu ya kampeni kufanywa kwenye vyombo vya habari wakati  mchakato wake ni wa ndani ya vyama, kisha bungeni,” alieleza.
 Kada  huyo alisema wanaotumia vyombo vya habari wangekuwa na dhamira nzuri,  wangeeleza sifa, majukumu na wasifu wao ili wananchi wawajue na kujenga  imani nao.
 
 Kutoka Mtandaoni, Wasomaji wa Mwananchi wamekuwa na  maoni tofauti juu ya kauli hiyo, lakini wengi wamechukizwa na kitendo  cha Chenge kutumia lugha kali  wakimtaka akae kimya kwa kuwa hana sifa.
 "Tunamshauri  huyu mzee 'visenti' asilete utani mbele ya safari kwani ataanguka kwa  aibu mbele ya jamii na amwogope Mungu, mikataba mibovu aliyopitisha  kinyemela inatosha," alisema  Estomihi Lyimo.
 Msomaji mwingine  aliyejitambulisha kwa jina la Mchungu wa Bongo  alisema "kama umetumwa  na hao watuhumiwa wa ufisadi na kama kuna mbunge atapokea pesa ili  awasaliti Watanzania... basi mbunge huyo na afe na watu wote waseme  amen".
 Msomaji aliyejitambulisha kwa jina la Deobern alisema:  "Nilisikitika sana niliposikia kuwa Chenge ambaye sistahili hata kumwita  mheshimiwa, amechukua fomu ya kugombea uspika. Sishangai kwa sababu,  inawezekana nikawa namwonea Chenge ilhali ametolewa sadaka kumfunga paka  kengele.
 
 "Asante Chenge kwa kujitokeza kuwania uspika. Hivi  kweli hujioni umechafuka? Ondoa jina lako haraka utaaibika.Wewe nadhani  uroho wako wa madaraka unataka kuimaliza sisiem na pia kuichafua inji  hii."
 | 
No comments:
Post a Comment