Tuesday, September 27, 2011

HUYU NDIE MCHEZAJI WA KWANZA AFRIKA MASHARIKI KUCHEZA SOKA ULAYA...


Huyo bwana anaitwa SUNDAY RAMADHANI MANARA aka 'Computer' aliyezaliwa miaka 54 iliyopita mjini Kigoma mahali ambapo palikuja kuwa chimbuko la wachezaji wengi nyota kama akina Hamis Askari, Aloo Mwitu, Athuman Juma, Juma Kampala, Abeid Mziba, Makumbi Juma na wengineo.
Mkongwe huyo, ambaye ndugu zake wawili nao walikuwa wanapiga soka yaani Kitwana Manara kaka yake na mdogo wake Kasimu Manara kwa sasa anapatikana maeneo ya Temeke, jijini Dar es Salaam.


MAISHA YA UTOTONI KATIKA SOKA
Sunday anakumbuka maisha yake ya utotoni alianza kuchezea Young Kinya ambayo ilikuwa kama timu ya watoto wa Yanga ingawa ilikuwa kama inajitegemea zaidi na ilikuwa inafanya mazoezi nje ya viwanja vya Kaunda na ilikuwa ukitoka pale unasogea kidogo unakwenda Afrikan Boys ambayo ilikuwa ni timu ya pili ya Yanga na mwanzoni mwa miaka ya 1970 Sunday na wenzie akina Awadhi Kessy, Douglas, Shabaan Ufunguo, Mohamedy Ugando walipandishwa kuichezea Yanga ya wakubwa chini ya kocha Profesa Victor Stanculescu na huko waliwakuta kina Elias Michael, Mohammed Msomali, Hassan Goboss, Boi Iddy, Athuman Kilambo, Maulidi Dilunga, Badi Salehe, Leonard Chitete na wengineo.

MALEZI YAKE KWA STANCULESCU
Sunday, ambaye binafsi anakiri kuwa hajui jina la mashine hiyo yenye kufanya kazi vizuri alipewa na nani zaidi ya kukumbuka tu ni mwaka 1975 alipotoka Zanzibar baada ya kuwapiga Simba mabao 2-0 ila anakubali kuwa maisha waliyokuwa wanalelewa na Mzungu huyo yalimfanya aipende sana Yanga kuliko timu nyingine yeyote ikiwamo Taifa Stars, ambayo walikuwa wachezaji takribani saba, ambao ni kipa Elia Michael, Athuman Kilambo, Hassan Gobboss, Abdulhaman Juma, Kitwana Manara, Gibson Sembuli na yeye mwenyewe.
Ushirikiano ulikuwa mkubwa na ulisababisha kuwa mara zote ni furaha tupu ndani ya mitaa ile ya Jangwani hadi mwaka 1973 ambapo Simba ilifuta uteja kwa kuwafunga bao 1-0 lililowekwa kimiani na nahodha wa Simba wakati huo, Haidar Abeid �Muchacho�.

SUNDAY MANARA NA SIMBA
Sunday anasema mara zote alizokuwa akikutana na Simba alikuwa anawaua tu bila masihara, mwaka 1971 Simba ilifungwa mabao 2-0 na moja alifunga yeye na jingine alifunga Maulid Dilunga, mwaka 1974 mechi ya kihistoria ambayo ilipigwa mjini Mwanza katika Uwanja wa Nyamagana, Simba ilifungwa mabao 2-1, yaliyofungwa na Adam Sabu kwa upande wa Simba kabla ya Gibson Sembuli kufunga dakika ya 87 na Sunday Manara kushindilia msumali wa mwisho dakika 30 za nyongeza.
Mechi nyingine ilikuwa ni fainali ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki iliyopigwa mjini Zanzibar katika Uwanja wa Amaan na Yanga kuibuka na ushindi wa mabao 2-0, huku goli la kwanza likifungwa na Sunday Manara la umbali wa zaidi ya mita 25 na kusababisha utata mkubwa kwa manazi wa Simba wakimtuhumu kipa wao Athuman Mambosasa kuwa aliachia makusudi au alipewa kitu kidogo na bao la pili lilifungwa na Gibson Sembuli kama kawaida yake kwa shuti kali sana.
Mbali na kuifunga Simba mara zote hizo, Sunday pia alikuwa ni rafiki mkubwa sana wa kipenzi cha Simba, Abdallah King Kibaden Mputa ambaye kwa sasa ni meneja wa Simba.
Sunday pia alioa binti wa aliyekuwa Mwenyekiti wa Simba, mzee Hassan Haji ambaye ni baba mkubwa wa Mohammed Mkweche aliyekuwa beki maarufu wa Pan African.
Simba pia ndio waliofanikisha mpango mzima wa Sunday Manara kwenda kucheza soka la kulipwa nje ili atoe balaa la wenyewe kufungwa na mtu huyo, huo ndio uhusiano wake na Simba maarufu kama Lunyasi

KUVUNJIKA KWA YANGA KUZALIWA PAN
Sunday akizungumza kwa masikitiko makubwa na bila kumung�unya maneno anamtupia lawama kubwa kocha raia wa Zaire wakati huo, Tambwe Leya kuwa baada ya kutolewa na Enugu Rangers ya Nigeria katika mashindano ya Afrika aliwatuhumu wachezaji nyota akina Sunday, Omary Kapera, Sembuli na wengineo kuwa wameihujumu timu hadi kusababisha kufungwa hivyo wanachama kwa hasira wakawafukuza viongozi wote wakiongozwa na mzee Tabu Mangara na Shiraz Sharif na kuwekwa viongozi wengine ambao waliwataka wakiri makosa.
�Kwa kuwa hatukujua kosa letu, tukaondoka na kuelekea Nyota Afrika ya Morogoro na baadaye tukarudi Dar es Salaam na kuunda timu inaitwa Pan mwaka 1976,� anasema.

SUNDAY MANARA NA SOKA LA KULIPWA

Mwaka 1977 Sunday alitimkia Uholanzi kupiga soka la kulipwa na alikuwa mchezaji wa kwanza Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla kwenda kucheza katika ligi kubwa Ulaya katika timu ya Heracles ambayo ipo hadi sasa katika ligi hiyo na huko alikutana na watu kama akina Jaan Rep, Ruud Krol, Johan Neeskens, Johan Cruyff ,Van Hangem na wengineo. Alikaa huko mpaka mwaka 1979 alipotimkia nchini Marekani ambako walikuwa wameanza mipango ya kukuza soka nchini kwao.

TENGA KAJIFUNGIA NA FIKRA ZAKE
Sunday akizungumzia soka la Tanzania anamshushia lawama nzito Mwenyekiti wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) Leodegar Tenga kuwa analipeleka soka kuzimu na kuwa hahitaji ushauri kwa watu ambao anajua kabisa kuwa wamecheza soka kwa upeo mkubwa na soka wanalielewa kama yeye.

�Tenga hapendi kukosolewa sasa mawazo mapya atayapata wapi? Namshauri kama mdogo wangu aitishe mdahalo wa kitaifa tuzungumzie soka, tupo tunaojua matatizo ya soka si hao wenye vyeti na soka hawalijui,� anasema Computer ambaye kwa sasa yuko mbioni kuwa na Academy yake ambayo itakuwa mfano wa kuigwa nchini

SOKA LA ZAMANI NA SASA
Computer anasema viongozi wa zamani walikuwa na mapenzi makubwa na viongozi wenzao wa timu nyingine na wachezaji wa upande mwingine pia wachezaji walikuwa wanapendana nje ya uwanja, upinzani ilikuwa ndani ya uwanja.

Sunday, ambaye ni mpenzi wa Barcelona ya Hispania anawasifia wachezaji kama Mbwana Bushiri, Emil Kondo na John Lyimo kuwa walikuwa na vipaji vya hali ya juu, ingawa anakiri kuwa hata sasa wapo wenye vipaji lakini wameshindwa kuvumbuliwa.


1 comment:

Anonymous said...

SISI HUA NI WA KWANZA KUANZISHA JAMBO ILA NI WA MWISHO KATIKA KULIENDELEZA,ANGALIA NCHI YA KWANZA KUPATA UHURU UKANDA HUU,MAMBO YA MZIKI,. NK

Website counter