www.kinyaiyas.blogspot.com: Kwa habari za Kijamii, Michezo na Burudani kwa wakati...
Sunday, September 11, 2011
KUTANA NA MWANAMKE WA SHOKA...
BIASHARA ya usafiri wa pikipiki maarufu kama ‘bodaboda’ imeshamiri nchini kote. Hata hivyo, kwa kiasi kikubwa biashara hii hufanywa na wanaume. Lakini hali ni kwa Maria Chacha (25). Huyu ni mwanamke pekee anayetoa huduma ya usafiri wa bodaboda katika eneo hilo. Pamoja na changamoto kubwa anazopata katika kazi hiyo, Maria ameweza kusimama imara na kujipatia riziki yake ya kila siku kupitia kazi hiyo na kuweza kutunza familia yake ya watoto wanne. Maria anasema haikuwa rahisi kwake kupata kazi nzuri baada ya kuachana na mume wake, hivyo akalazimika kutafuta kazi itakayoendana na elimu yake. Kutafuta kazi Anasema awali, alipata kazi hiyo ndani lakini aliacha baada ya siku mbili tu tangu kuanza kutokana na kile anachosema ni ukorofi wa mwajiri wake. Baada ya hapo alianza kazi ya kubeba zege katika jengo lililokuwa likijengwa katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando anadai kwamba, alikuwa akilipwa ujira wa Sh3, 000 kwa siku. Hata hivyo ugumu wa kazi hiyo ulimfanya aanze kufikiria kazi nyingine na alipata kazi ya ulinzi katika Kampuni ya Ulinzi ya Mara Security na kudumu kwa miezi mitano. “Kazi ya ulinzi ilikuwa ngumu sana kwangu, sikuweza kukesha usiku, tena nje, niliugua sana malaria kutokana na mbu na baridi kali la usiku,” anasema Maria. “Pia gharama za maisha zilikuwa kubwa kwani wakati huo nilikuwa nikiishi na wanangu wawili, hivyo ilinilazimu kuanza kufanya kazi ya umachinga ambapo mchana nilikuwa nikiuza nguo mitaani na usiku nikienda kwenye lindo,” anasema Maria na kuongeza kuwa baadaye aliamua kuachana na kazi hiyo ya ulinzi. Anasema pia kukatwa mishahara bila utaratibu na kuchelewa kulipwa ni sababu nyingine zilizomfanya aacha kazi hiyo ya ulinzi. Udereva wa Bodaboda Baada ya kuzunguka kwa muda mrefu aliamua kuingia kwenye kazi ya udereva wa Bodaboda. Anasema haikuwa rahisi kama alivyokuwa akifikiria kupata kazi hiyo na alikumbana na vikwazo vingi kimoja wapo ni kubaguliwa kutokana na jinsia yake. “Nilikuwa natembelea vijiwe vya waendesha pikipiki nikawaeleza kuwa nataka kuwa dereva wa bodaboda. Wengi walikuwa hawaniamini kama naweza, hakuna aliyekuwa tayari kunipa pikipiki yake nijaribu kazi hiyo” anasema Maria. Lakini kwa bahati nzuri siku moja alitoke jamaa aliyemtaja kwa jina la Marwa Mgaya na kumpatia pikipiki yake ili aone kama ana uwezo wa kuendesha na kuongeza: “Ilikuwa ni bahati kwangu, sikufanya kosa, kila mtu alistaajabu na huo ndio ukawa mwanzo wa kuaminika.” Hata hivyo anasema awali alikuwa na wasiwasi kwani bado hakuwa na uzoefu wa kutosha wa kuendesha pikipiki, lakini baada ya wiki mbili aliweza kuwa mzoefu wa kutosha kujua mitaa ya jiji na kuanza kuona mafanikio yake baada ya mwaka mmoja. Anakiri kuwa kwa kipindi chote alichokuwa akiendesha bodaboda, hakuwa na leseni, hivyo aliona umuhimu wa kuongeza ujuzi wa kazi yake ambapo alisema alienda kusomea udereva kwa muda wa mwezi mmoja. “Niliingia darasani kwa muda wa mwezi mmoja na nusu ambapo niliugawa muda wangu wa kazi na shule, mafunzo haya niliyapata katika chuo cha udereva cha Lake, na sasa nina leseni ya udereva wa pikipiki na gari” anasema. Changamoto kazini Kuna matatizo mengi ambayo Maria anakumbana nayo akiwa kazini, kubwa ni kutoaminika na baadhi ya wateja kuwa anaweza kuendesha pikipiki, hivyo wakati mwingine wanamkwepa na kwenda kwa madereva wakiume. Mazingira magumu hasa wakati wa mvua, pia jua kali la mchana na kudhulumiwa na wateja wakorofi wakati wa malipo ni changamoto nyingine anazokabiliana nazo. Matarajio ya baadaye Maria anasema hajaridhika kuishia kuwa dereva wa pikipiki bali anataka kuwa dereva wa magari makubwa akiamini kuwa kazi hiyo itamuongezea kipato. Aidha Maria aliomba mtu yeyote anayeweza kumpatia kazi ya udereva kwa kipindi hiki tofauti na pikipiki ampatie kwa kuahidi kufanya kazi kwa uaminifu. Historia yake Maria Chacha alizaliwa katika kijiji cha Nyangoto, wilayani Tarime mwaka 1986 akiwa mtoto wa nane katika familia ya watoto tisa wa mzee Samburu Chacha na mkewe Bokhe. Alihitimu darasa la saba mwaka 2001, na mwaka uliofuata aliolewa na Grabriel Chacha aliyeishi naye kwa miaka nane na kuzaa watoto wanne. Mwaka 2009 ndoa yao ilivunjika kutokana na matatizo ya kifamilia baada ya mumewe kumfanyia vitendo vya unyanyasaji, ikiwamo kumpiga na kisha kumfukuza. Baada ya hapo aliamua kuhamia jijini Mwanza na kuanza harakati za maisha.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment