 
TUNAKUTANA tena kupitia safu hii nikiamini umzima na unaendelea vyema na  majukumu yako ya kila siku kama kawaida. Kwa Waislam najua swaumu kama  kawa, Mungu awajaalie afya njema na mmalize salama salmini.  Ndugu  zangu, huko nyuma niliwahi kuandika namna simu za mkononi zinavyovuruga  uhusiano. Tatizo la wapenzi na wanandoa kukorofishana mara kwa mara  kutokana na kushutumiana juu ya utumiaji mbaya wa simu zao za mkononi si  geni kwa walio wengi.  Walioachana kwa sababu ya chombo hicho cha  mawasiliano ni wengi lakini pia wale ambao ‘wanatifuana’ kila kukicha  kila mmoja akimfikiria mwenzake tofauti kuhusiana na matumizi mabaya ya  simu yake idadi ni kubwa kuliko maelezo.    Kwa maana hiyo basi,  leo nataka kuzungumzia kitu ambacho naweza kutofautiana na wengi lakini  ndiyo ukweli hasa katika kipindi hiki, lengo ni kuleta amani na  kuwafanya wapenzi na wanandoa kudumu muda mrefu bila migogoro isiyokuwa  na lazima.  Juzi nilipata simu kutoka kwa msomaji wangu mmoja  aliyejitambulisha kwa jina la Suzan wa Arusha. Katika maelezo yake  anadai ameachwa na mume wake baada ya mwanaume ambaye alikuwa mpenzi  wake wa zamani kuanza tabia ya kumpigia simu usiku na wakati mwingine  kumtumia sms kuonesha bado wanaendelea kupeana mambo.  “Inaonekana  ni tabia ya baadhi ya watu kufanya makusudi ya kugombanisha wanandoa au  wapenzi ili waachane, sijui wanapata faida gani. Nilimpa uhuru mume  wangu kuishika simu yangu wakati wowote, kilichonipata ni kuachika.  “Kuna  mwanaume siku moja alinitumia sms akinipongeza kwa penzi nililompa jana  yake, kitu ambacho hakina ukweli. Kwa bahati mbaya siku hiyo nilimuaga  mume wangu kuwa naenda kumtembelea shangazi huko Moshi. Sikumjali lakini  kosa nililofanya sikuifuta ile sms.  “Mume wangu akaiona na  kunipa kibano cha hali ya juu. Nilijaribu kumwambia ukweli wa mwanaume  huyo lakini sijaeleweka na mbaya zaidi tukiipiga ile simu haipatikani.  Tukawa hatuaminiani kabisa, mume wangu akawa anahisi namsaliti.  “Hivi ninavyoongea na wewe sina ndoa. Mume wangu kaniacha kwa sababu ya kumpa uhuru kushika simu yangu,” alisema Suzan.   Tunajifunza  nini kwa ushuhuda huu? Wewe haijawahi kukutokea hii? Jitu linakutumia  sms hulijui lakini linakuambia linakupenda sana kuliko hata mumeo  anavyokupenda, mumeo akiiona hii atakufikiriaje? Ni sawa unaweza  kumuelewesha lakini je, kama huyo mpenzi wako ni mgumu wa kuelewa  unadhani nini kinaweza kutokea hapo?  Nilishawahi kusema kwamba,  ili kumjengea mpenzi wako mazingira ya kukuamini, mpe uhuru wa simu yako  lakini ukweli ni kwamba uhuru huo huo niliouzungumzia ndiyo  unaosababisha matatizo kwa walio wengi leo hii.  Ndiyo maana  baadhi ya watu wanasema kama ni kutokuaminiwa na wenza wao bora iwe  hivyo lakini hawawezi kuwapa uhuru wa kushika simu zao, kwa nini? Kwa  kuwa wanajua watatibuana kila mara.  Unaweza kumfikiria mpenzi  wako tofauti kwamba anaficha madhambi yake kwa kukukataza kugusa simu  yake lakini wakati mwingine yawezekana ni katika kuepusha matatizto na  wala hakuna uovu wowote unaofichwa! 
 
No comments:
Post a Comment