Tuesday, July 19, 2011

LEO KWENYE KONA YA MAHABA...


KUNA tabia siku hizi, vijana wanakutana klabu usiku, wanapendana, halafu wanakwenda kulala pamoja hotelini. Baada ya wiki tatu wanafanya ‘pati’ kubwa ya kuvalishana pete, tayari wameshakuwa wachumba.

Miezi miwili ya uhusiano wao, wanatangaza ndoa. Kwa madai yao, wameshachunguzana vya kutosha, wamepimana tabia na wanataka kujenga familia pamoja. Wataweza? Ni ndoto!
Mambo vipi wapenzi wa safu hii? Nilianza moja kwa moja na utangulizi wa mada hii baada ya kuzidiwa na mzuka...naona kama vile nachelewa. Mimi ni mzima bukheri wa afya, karibuni uwanjani.

Kikubwa ninachotaka kuzungumza leo ni umuhimu wa mwanamke kumchunguza mwanaume wake kama ni sahihi, kama anafaa kuwa wake wa maisha. Ni kweli si rahisi kugundua kila kitu kwa usahihi kutoka kwa mwenzi wako mtarajiwa lakini kuna yale mambo ya muhimu zaidi ya kuzingatia ambayo angalau yanampa asilimia nyingi za kuwa mume.

Ndoa ni muhimu na ngumu kwa wakati mwingine hasa linapokuja suala la kuchagua mwenzi wa kuishi naye maishani. Wanawake wengi wamekuwa wakigombana na wenzi wao wa ndoa, ama ndoa zao kuvunjika kabisa kutokana na kutoelewana.

Hata hivyo, unapowauliza baadhi ya wanawake ambao tayari wamekwishaachana na waume zao au wapo katika migogoro mikali katika ndoa, watakupa sababu za msingi ambazo huenda ikawa ni manyanyaso na mateso makali katika ndoa zao.

Kimsingi matatizo hayo kwenye ndoa, yanatokea kwa vile mwanamke hakupata muda wa kumchunguza vya kutosha mwenzake. Amekurupukia ndoa. Kama angepata muda wa kumchunguza mwenzake kabla ya kuingia kwenye ndoa, pengine angemjua zaidi na kumuepuka.

Katika makala haya, japo kwa uchache, nitakupa sifa za mwanaume ambaye anafaa kuwa mume kwa asilimia sabini. Yapo mengi ambayo unatakiwa kuyachunguza kwa mwanaume wako, lakini hapa nitakuainishia yale ya muhimu zaidi.

NI MKWELI?
Katika hili hekima na busara nyingi huhitajika kutumika. Ngao kubwa ya utambuzi juu ya mpenzi uliyenaye kuwa ni mume mwema linategemea sana hili. Ukweli ni silaha muhimu sana katika uhusiano.

Japokuwa natambua kwamba, kuna wengine watajiuliza utajuaje kama huyu ni mkweli au siyo. Kitendo cha kukutamkia kuwa anakupenda ni cha ukweli sana hasa kama atakuwa anakupenda kwa dhati na ataonesha kwa vile anavyokupenda.

Kikubwa cha kuzingatia hapa, anayawekaje bayana maisha yake yaliyotangulia, anakueleza kwa uwazi upi hasa. Inawezekana alishawahi kuishi na mwanamke kabla yako au kuwa na uhusiano na mwanamke mwingine kabla yako, amekufahamisha vipi. Chunguza kila akuambialo ili kuhakikisha ukweli wake.

Baadhi ya wanaume wanafikia hatua ya kuazima magari na kujifanya yao ili wawanase wanawake lakini kumbuka wahenga walisema, ‘Njia ya muongo ni fupi’, hivyo baada ya muda utachambua pumba na nafaka!

ANAKUJALI?
Kuna msemo wa Kiswahili usemao, ‘Nyota njema huonekana alfajiri’. Msemo huu una maana kubwa sana. Kama mwanaume huyu ambaye kwa sasa ni mchumba wako (wazazi wawe wanatambua) anakupenda, lazima atakujali, atakuwazia wewe katika maisha yake yote, atakuona wewe ni mwenye thamani kubwa katika maisha yake.

Hatakusumbua kwa kutaka ngono kabla ya muda muafaka wa kufanya hivyo kufika. Anayejali afya yako; Kwanza hatathubutu kushiriki tendo la ndoa ukiwa katika mazingira yasiyo salama. atakupeleka hospitali unapokuwa mgonjwa (haijalishi kama una wazazi au wasaidizi wengine). Hiki ni kipimo cha juu ya upendo wake kwako.

Kama katika uchumba atashindwa kukupeleka hospitali, vipi mkiwa ndani ya ndoa? Si atakuacha ukilia ndani huku yeye akiendelea na starehe zake?

ANA MSIMAMO?
Huu huonekana mapema sana, asiyetingishika wala kushawishiwa na marafiki zake katika mambo yasiyofaa.

atashikilia msimamo wake katika kutekeleza yale yote aliyokuahidi na aliyopanga kuyafanya kwa ajili yenu.
Mathalani ameambiwa na watu kuwa una uhusiano wa kimapenzi na mwanaume mwingine. Huyu mwenye msimamo huchukua muda mwingi kufanya uchunguzi juu ya aliyoyasikia kabla hajakuuliza chochote.

Nasema hivyo kwa sababu kuna baadhi ya wanaume wana kasumba mbaya, wanaposikia kitu kuhusu wachumba zao au wapenzi wao, kabla ya kufanya uchunguzi huwajia juu wenzi wao na wakati mwingine hufikia hatua ya kuwapiga.
Hii ni hulka mbaya ambayo baadhi ya wanaume wanayo, lakini jaribu kujiuliza, kama hamjaoana anadiriki kukupiga kama ngoma, akikuoa itakuwaje?

No comments:

Website counter