Saturday, July 23, 2011

JAMANI WENYE MAHOTELI MSAIDIENI DADA HUYU....


NI binti mrembo kweli ambaye hakuna shaka kwamba kila amwonaye atampenda. Hakuna shaka pia kwamba kama wasichana wengine wengi, naye ana mipango yake mingi ya maishakwa siku za usoni.

Lakini, si hivyo kwa Renata Leonard, ambaye kwa miaka saba iliyopita hakuwa kama alivyo leo sasa, kwani mipango yake ya maisha imetibuka.“Ni ajali iliyotibua mipango yangu kiasi cha kunisababishia kupoteza kumbukumbu mara kwa mara,” anaeleza binti huyo .

“Siku sintoisahau maishani kwani ilikuwa mchana nilipomuaga mama na kumwambia kwamba naelekea kwenye mkutano wa Injili muda mfupi baada ya kutoka Shule ya Sekondari ya Dar es Salaam nilikokuwa nasoma wakati ule,” anaeleza Renata.Renata anasema kuwa alikuwa akisoma kidato cha tano akichukua masomo ya Historia, Jiografia na Kiingereza (HGL) , akiwa mwezi mmoja na nusu tokea wafungue shule.

Anaeleza kuwa muda wa masomo ulipoisha alirudi nyumbani kwao Mbagala Kuu, Manispaa ya Temeke na kumkuta mama yake na kumwomba ruhusa ya kwenda kwenye viwanja vya Jangwani, Dar es Salaam ambako ulikuwa ukifanyika mkutano wa Injili.

“Tangu nijiunge na kidato cha tano nilikuwa nimesoma kwa mwezi mmoja na nusu ambapo siku hiyo nilirudi nyumbani mapema nikaweka madaftari yangu chumbani mwangu na nilimfuata mama na kumuaga, nikimweleza kuwa nilikuwa naelekea Jangwani kwenye mkutano wa Injili.

Anasema siku hiyo ya Juni 29, 2004 alipokuwa anaelekea kwenye mkutano huo wa Jangwani akiwa anavuka Barabara ya Morogoro anakumbuka kuona gari likija kwa kasi na aliposhtuka gari lilimgonga na tangu hapo ndipo alipoteza fahamu.

“Ninachokumbuka nilimuaga mama kwamba naelekea kwenye mkutano wa Injili kule Jangwani na nilipojaribu kuvuka barabara niende upande vilipo viwanja hivyo niligongwa na gari sijakumbuka kitu kilichotokea na kile kilichoendelea.” Kwa shida, Renata anajaribu kueleza, lakini hawezi, anapoteza kumbukumbu na ndipo anaingilia kati mdogo wake aitwaye Revina Leonard akieleza kilichoendelea.

Atakueleza mdogo wangu huyo, mimi sikumbuki vizuri, ”anasema Renata.
Revina ndiye anayemsaidia na kueleza kuwa siku hiyo dada yake (Renata) hakuonekana nyumbani kwa hiyo iliwabidi wazazi na ndugu zao wakisaidiwa na majirani waanze kumtafuta kwa kutoa taarifa hadi misikitini na vituo vya polisi.
“Tulimtafuta kwa siku mbili mfululizo bila mafanikio na ndipo tuliamua kumtafuta hata kwenye wodi kule Muhimbili na mochwari ya Hospitali ya Amana, lakini bila mafanikio.

Kisha tulikaa wanandugu na kukubaliana twende Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH),”anaeleza Revina.
Anasema kipindi chote walichokuwa wakimtafuta dada yake kumbe alikuwa amegongwa na gari na hali yake ilikuwa mahututi na alichukuliwa na wasamaria wema na kukimbizwa Muhimbili.

Revina anaongeza kuwa walipofika hospitalini hapo waliambiwa kuwa kuna mgonjwa wa kike ambaye aligongwa na gari na alifikishwa hapo siku mbili zilizopita na alikuwa amelazwa kwenye chumba cha wagonjwa mahututi.
“Baada ya kuelezwa hayo mama na baba waliruhusiwa kuingia ili wamwone na kweli ndiye dada ( Renata) au la, lakini ilikuwa ni vigumu kwao kumtambua kwa haraka kutokana na majeraha makubwa kichwani mwake.

“Kwa bahati nzuri mama aligundua kwa macho yake, lakini miguu yake ilikuwa na alama aliyozaliwa nayo ingawa mguu wake wa kushoto ulivunjika mara mbili na wa ule wa kulia ulikuwa umevunjika mara tatu,”anasimulia Revina .
Revina anaongeza kuwa dada yake pia alipasuka kichwa na kushonwa nyuzi tano.

Katika simulizi lake, Revina anaongeza kuwa dada yake alilazwa kwenye chumba hicho cha wagonjwa mahututi kwa siku 11 huku akiwa amepoteza fahamu na alikuwa amewekewa hewa ya oksijeni ili kumsaidia kupumua na aliweza kuongezewa chupa sita za damu .“Baada ya siku 11 kupita ndipo Renata alipohamishiwa kwenye wodi ya Mwaisela na alilazwa huko kwa miezi tisa huku akiendelea na matibabu,” anasema Revina.

Anaeleza kuwa miezi tisa ilipita, lakini mguu wake wa kushoto ambao ulikuwa umevunjika mfupa mkubwa na kuwekewa chuma ulikuwa umeanza kuoza na kuamuliwa na daktari ukatwe.Revina anasema daktari aliposema mguu wa dada yake ukatwe, mama yao alikataa na kuamua kumhamisha bila ya taarifa na kumpeleka Kibaha kwa Dk. Bake ambapo aliungwa mguu wake.

“Novemba 2004 alipelekwa katika Hospitali ya Dk Bake iliyoko Kibaha Mkoani Pwani na alilazwa kwa ajili ya kufanyiwa upasuaji kwa mara ya pili ambao ulifanywa kwenye mguu wa kushoto ambao ulikuwa umeshaanza kuoza, “anaeleza Revina.

Anasema Renata alifanyiwa upasuaji huo wa mguu kwa mara ya pili ambapo aliwekewa vyuma vipya ili viweze kumsaidia mguu huo kuunga.“Niliambiwa nyama ya goti imeungana na mfupa na kusababisha goti lisikunje, lakini baada ya kufanyiwa upasuaji niliweza kutembea kwa kutumia magongo, ila mguu wangu ulikuwa haukunjiki.

“Kwa kutokunja goti langu niliambiwa na daktari wangu kuwa aliyenifanyia upasuaji nikiwa hospitali ya Muhimbili alinifanyia vibaya na ndio maana hadi leo hii siwezi kukunja goti,”anasema Renata.Renata anaongeza kuwa baada ya kutolewa hospitalini Kibaha aliendelea na matibabu huku akiwa anatumia magongo katika kipindi cha miezi sita.

Mwaka 2005 aliacha kutumia magongo na alikuwa anapelekwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa ajili ya kupatiwa mazoezi maarufu kama ‘mama cheza’ ambapo alikuwa akilipia Sh 8,000 kila siku.

“ Kwa bahati mbaya, Juni 2005 baba yangu ambaye alikuwa msaada mkubwa alifariki na hivyo nikakosa fedha (Sh 8000) za kila siku kwa ajili ya mazoezi. Nikawa siendi tena hospitali kutokana na kutokuwa na fedha,”anasema Renata.
“Mama yangu alisitisha kunipeleka kwenye mazoezi ( kwa Mama Cheza) kutokana na kutokuwa na fedha na aliamua kunifanyia mazoezi nyumbani kuanzia 2005 hadi 2006 ambapo pale nyumbani palikuwa na mlima ambao ulinisaidia katika kufanya mazoezi,”anasema.

Anasema mwaka 2007 alijiunga na English Vision ambayo ipo Ubungo na alikuwa anafundishwa kusoma na kuandika kwa kuwa alikuwa amepoteza kumbukumbu zote.“Nilisoma kwa kipindi cha miezi sita ili nijue kusoma na kuandika kwa kuwa nilikuwa sijui kabisa kusoma kutokana nilikuwa nimepoteza kumbukumbu zangu zote,”anasema Renata.

Anasema baada ya kumaliza kujifunza kusoma na kuandika aliamua kusomea masomo ya hoteli katika Chuo cha Amazon na alisomea usafi wa vyumbani.“Kutokana na hali yangu ya usahaulifu na kupoteza kumbukumbu nilisoma mwaka mmoja na baadaye nilipangiwa kufanya mazoezi ya vitendo kwenye hoteli ya Peacock katika kipindi cha miezi minne.

“ Nilipata ripoti nzuri na katika ripoti yangu nilipata alama C ambapo cheti changu kilikuwa kizuri,”anasena Renata. Anaongeza baada ya kumaliza kozi yake aliweza kutafuta kazi sehemu mbalimbali, lakini hakufanikiwa. Anaeleza kuwa kama ajira itatokea anao uwezo wa kufanya kazi.

Anaeleza kuwa tatizo lake la kupoteza kumbukumbu kwa sasa linatokea mara moja moja, hivyo yeye amechoka kukaa nyumbani hivyo kama kuna kazi katika hoteli yeyote nchini ana uwezo wa kufanya kazi kwa upande wa usafi wa vyumbani.

“Kipindi hiki nipo katika wakati mgumu sana kimaisha kutokana na mama yangu kwa wakati huu hana uwezo wa kifedha, hivyo nimekaa kipindi cha miaka mitatu bila kazi, kwa yeyote atakayejitokeza kunipa ajira kwenye hoteli nitafanya kwa kuwa uwezo wa kufanya ninao,”anasema Renata.

Binti huyo anawaomba wamiliki wa hoteli wajitokeze na kumsaidia kwani uwezo anao, lakini amekosa ajira kutokana na ajali ambayo anasema imemwathiri.

*Anayetaka kumsadia - 0657 003488 (Renata) au 0653 207663 (Pamela

No comments:

Website counter