Friday, June 3, 2011

LEO KATIKA 'MAHABA; TUACHENI 'WIVU' WA KIJINGA JAMANII...


Zipo hisia zinazowaongoza wanaume wengi kuhusu wanawake. Hawataki wafanye kazi, ikibidi wakae tu nyumbani kwa hoja kuwa wanapokuwa maofisini wataanzisha uhusiano mpya.


Wale wanaoruhusu wake zao wafanye kazi, kila siku roho juu. Macho pima kwenye simu za wenzi wao. Hawana imani ya asilimia 100 kwamba siku hupita bila kusalitiwa. Wanateswa na sononeko la moyo.

Haipendezi kumfikiria mwenzako kwa ubaya. Inashauriwa umuamini na ujiamini. Mawazo chakavu kuhusu mwenzi wako ni sumu. Ukiyaendekeza yanaweza kukufanya ushindwe kutekeleza mambo ya msingi.

Mwanamuziki Stara Thomas amelifafanua hilo vizuri kwenye wimbo wake “Wasiwasi wa Mapenzi”. Kwamba mtu anaweza kujawa na hofu ya kusalitiwa na mwenzi wake mpaka roho ikawa juu juu.
Unaweza kumvaa mtu asiye na hatia na kugombana naye kwa sababu tu ya mawazo kwamba anakuchukulia mali yako. Siku zinasogea, baadaye unakuja kugundua kuwa hisia ndizo zilikupeleka ndivyo sivyo.

Busara za kisaikolojia zinakutaka uwe huru, kwa maana unatakiwa ujiepushe na mawazo mabaya. Mtu akipiga simu ya mwenzi wako, si ukurupuke na kuanzisha songombingo, hebu vaa utulivu na usuluhishe kwa nidhamu.

Kushika simu ya mwenzi wako na kukagua simu zinazoingia na kutoka ni alama ya kutoamuamini. Ingekuwa humtilii shaka yoyote, usingethubutu kukiganda ‘kiselula’ chake.
Unataka kuona SMS zinazoingia na kutoka. Hulali mpaka uone simu alizopiga na alizopigiwa. Presha hiyo yote ya nini? Jaribu kumuamini na umuoneshe jinsi usivyo na shaka naye. Mwache yeye mwenyewe atumie vibaya imani yako kwake.

Kuna mtu kwa wasiwasi alikuwa anashindwa kutimiza majukumu yake ya kila siku, badala yake anakwenda kujificha nje ya ofisi ya mke wake, anashinda pale, lengo ni kuona wakati wa ‘lunch’ mkewe anaongozana na nani.

Ikiwa siku hiyo mkewe kaongozana na mfanyakazi mwenzake wa kiume kwenda lunch, jioni nyumbani ni kesi. “Nimepata taarifa zako, leo ulikwenda lunch na mwanaume, yule ni nani?” Hana lolote, hajaambiwa na yeyote, yeye mwenyewe na upeku peku wake.

UNAMKOSEA HESHIMA MWENZI WAKO
Iwe hutaki mwenzi wako afanye kazi au unamsumbua kwa namna yoyote ile, jawabu ni moja tu kwamba humheshimu. Kutokuwa na imani na yeye, maana yake ndani yako kuna hisia kuwa hajatulia.

Je, unadhani ni vema kumuona mwenzi wako hajatulia? Kama ndivyo, unaendelea kuwa naye kwa sababu gani? Asipoheshimiwa na wewe, unataka nani mwingine ampe heshima?
Mwenzi wako anapogundua kuwa humheshimu, taratibu naye atakushusha thamani. Akigundua huna imani naye, atakosa raha. Hata kama anakustahi leo, ipo siku ataona hana sababu ya kuendelea na wewe.

Mwingine anahaha kuulizia nyenendo za mwenzi wake kwa marafiki. Hilo ni kosa kubwa kwa sababu huyo unayemuuliza, mwisho anaondoka na kitu kikubwa kwamba hakuna uaminifu kwenye uhusiano wako.

Kuna mtu ambaye huweka mabodigadi wa kufuatilia nyenendo za mke wake kila anapokwenda. Anayedhani kufanya hivyo ni dawa, ameula wa chuya kwa uvivu wa kuchagua. Anakosea kupita kiasi.

No comments:

Website counter