Thursday, April 21, 2011

NAONA KAMA VILE MANENO YA MZEE MSEKWA YANA UKWELI FLANI IVI...


Msekwa: Yafaa spika kuwa mwanasheria, Spika Makinda asema si lazima!




MAKAMU Mwenyekiti wa CCM, Pius Msekwa amesema ni vigumu kwa mtu asiye na taaluma ya sheria kuliongoza Bunge akiwa Spika.Msekwa ambaye aliwahi kuwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tangu mwaka 2000 hadi 2005, aliyasema hayo katika mahojiano na Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC), hivi karibuni akizungumzia utendaji wake akiwa na wadhifa huo. Pia alizungumzia miaka 50 ya Uhuru.

Katika mahojiano hayo, Msekwa alisema alilazimika kurudi shule, kusomea shahada ya sheria ili aweze kuliendesha vyema Bunge.

Kauli hiyo ya Msekwa imekuja wakati Bunge la sasa likishuhudia mivutano ya kisheria baina ya wabunge na Spika wa Bunge hilo la 10, Anne Makinda.

Katika mkutano wa tatu wa Bunge hilo uliomalizika Jumamosi ya wiki iliyopita, Mbunge wa Singida Kusini (Chadema), Tundu Lissu ambaye pia ni Waziri Kivuli wa Sheria na Katiba alionekana kuipa wakati mgumu Serikali alipokuwa akipinga kifungu cha sheria kinachowaruhusu wanasiasa kuingilia uhuru wa mahakama.

Katika mvutano huo ambao pia ulimhusisha, Spika Makinda, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda alimuunga mkono Lissu licha ya muswada huo kupitishwa.

Katika Bunge la 10 pia kumekuwepo malumbano yanayoashiria wabunge wengi kutozijua vyema Kanuni za Bunge na sheria mbalimbali hivyo kujikuta wakivutana wao kwa wao, wakati mwingine na Spika Makinda.

Hata hivyo, baadaye akizungumza na Mwananchi, Msekwa alirejea kauli hiyo akisema: "Bunge ni la kutunga sheria, kwa hiyo ni muhimu kwa Spika kuwa na taaluma ya sheria."

“Ni kweli walinihoji TBC, ilikuwa ni kuhusu miaka 50 ya Uhuru. Ndiyo lile ni Bunge la kutunga sheria, kwa hiyo ni muhimu kwa Spika kuwa na taaluma ya sheria.”

Msekwa ambaye aliwahi pia kuwa Katibu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kati ya mwaka 1962-1970, Katibu Msaidizi wa Bunge kati ya mwaka 1960-1962 na Spika wa Bunge kati ya mwaka 2000-2005 alisema suala la Spika kusoma sheria ni la uamuzi binafsi siyo lazima.

“Huwezi kulilinganisha Bunge la wakati wangu na Bunge la sasa. Ni kweli kazi za Bunge ni zilezile, lakini wabunge wa sasa ni wengine. Siyo lazima kwa Spika kusoma sheria, ni uamuzi wa mtu binafsi," alisema na kufafanua:

"Adam Sapi Mkwawa hakuwa mwanasheria, Chifu Mang’enya hakuwa mwanasheria. Hata mimi nilipoanza sikuwa mwanasheria, lakini baadaye niliona umuhimu wa kusoma sheria.”

Bunge aliloongoza Msekwa lilishuhudia mawaziri wakilazimika kujiuzulu kutokana na kashfa. Hao ni pamoja na Profesa Simon Mbilinyi, Dk Juma Ngasongwa na baadaye Idi Simba wote hao kutokana na nguvu ya Bunge.
Akizungumzia kauli hiyo ya Msemwa, Spika Makinda licha ya kukiri kutosomea sheria moja kwa moja, alisema uzoefu alioupata Bungeni tangu alipotoka shule ndiyo unaomwezesha kuliendesha kwa ufanisi.

“Nimekulia na kuzeekea bungeni, taaluma yangu ni uhasibu, lakini mimi ni kati ya wabunge wakongwe. Tangu nimetoka shule niko bungeni,” alisema.

Alipoulizwa iwapo ana mpango wa kusomea sheria ili kumudu vyema zaidi uendeshaji wa Bunge, Makinda alisema kuwa amesomea sheria katika taaluma yake ya uhasibu ambayo inamsaidia pia kuzielewa Kanuni za Bunge.

“Kwani mimi sijasoma sheria? Mimi ni ‘accountant by professional’, (mhasibu kitaaluma) na huko nimesomea sheria. Ni kweli sina ‘bachelor’ (shahada) ya sheria, lakini, nina uelewa wa sheria," alisema.
Makinda alijigamba: " Nimekuwa mbunge, 'chief whip' (mnadhimu) kwa muda wa miaka minane, nimekuwa mwenyekiti wa Bunge, yote hayo yamenipa uwezo.”

Kuhusu changamoto anazokabiliana nazo katika nafasi hiyo, Spika Makinda alisema kuwa hilo jambo la kawaida kwake, lakini akasema tatizo na jambo kubwa ni wabunge kutokuelewa kanuni.

Hata hivyo, alisema anajitahidi kuwafundisha Kanuni za Bunge ili waendane na mwenendo wake.

“Unajua kipindi hiki wabunge ndiyo wamekuja, wengi wao hawajui Kanuni za Bunge, wanafanya makosa na utundu mwingi. Lakini tutawafundisha kanuni, naamini, Bunge litakuwa ‘smart’ siku zijazo,” alisema na kuongeza:

“Kwa mfano, sasa kuna kitu kinachoitwa ‘adjoin motion’ ambapo mbunge anamtaarifu Spika pale anapokuwa akiahirisha Bunge kuwa ana hoja ya kulitaarifu Bunge, basi Mbunge anapewa dakika 15 za kujieleza. Yote hayo tutawafundisha na wengi wameshaleta maoni ya kufanya hivyo.”

Akizungumzia tukio la hivi karibuni ambalo Mbunge wa Nyamagana (Chadema), Ezekia Wenje alitoa kauli iliyosababisha wabunge kurushiana maneno, Spika Makinda alisema kuwa tukio hilo lilikuwa ni kinyume cha Kanuni za Bunge.

“Kanuni zinakataza wabunge ku-shout hovyo (Kupayuka). Ile ilikuwa ni makosa. Unajua wabunge bado wanajifunza na tutafanya ‘amendments’ (marekebisho) ya kanuni ili kuwawezesha wabunge kuzoea Bunge. Kwa mfano, sasa kuna kitu kinaitwa “Committee of supply,” yaani wakati wa mbunge kutoa shilingi Bungeni. Hilo nalo tutawafundisha ili waelewe,” alisema.

No comments:

Website counter