Thursday, March 3, 2011

OOOH POLE SANA DADA YANGU...


Frida Mgimwa



“Sijui nitakuwa mgeni wa nani, kwa sababu maisha yangu na wanangu watano yanategemea biashara yangu ya kukopesha ambayo naifanya kwa kuzunguka mitaani, siwezi tena kuzunguka kwa sababu ya risasi niliyopigwa mguuni mwangu, sijui nitawalisha nini wanangu,”

Ndivyo mkazi wa Donbosco kata ya Mkwawa, Manispaa ya Iringa, Frida Mgimwa (33), alivyoanza kuzungumza, siku chache baada ya kudai kuwa alipigwa risasi na askari polisi wa kike, mjini Iringa.

Anasema hakuwahi kudhani kama siku moja atajeruhiwa bila hatia na kukosa mtu wa kumsikiliza baada ya kila mmoja kumgeuka huku taarifa za jeshi la polisi zikieleza kwamba, alipigwa na kitu chenye ncha kali.

“Nilipigwa bila hatia yoyote na sijui kama niliwahi kuwa na ugomvi na mtu yeyote, aliyenipiga nilimuona na hata nikiambiwa nikamuonyeshe naweza kwa sababu, namfahamu kwani nilimuona kwa macho yangu,” anasema Mgimwa.

Siku ya tukio
Akielezea tukio hilo, Mgimwa anasema awali, mtoto wake aliugua na kuamua kumpeleka hospitali kwa ajili ya matibabu, lakini wakati akisubiri vipimo, mtoto huyo alilalamika kuwa na njaa jambo ambalo lilimlazimu kukodi gari hadi Miami, ili aweze kumnunulia mtoto wake, chakula aina ya chipsi.

“Mtoto wangu alikuwa akiumwa, nikaamua kumchukua hadi hospitali ambako walimpima, lakini kabla hawajanipa majibu mtoto alikuwa akililalamika njaa, hivyo nikaamua kumpelea kwenye bar ya Miami, ili niweze kumnunulia chipsi,” anasema.

Anasema siku hiyo ilikuwa February, 4 saa tatu usiku mwaka huu, na kwamba, aliamua kuchukua tax hadi eneo la Miami ambako mara nyingi amekuwa akipendelea kwenda.

Anasema wakati akishuka kwenye tax aliyokuwa akiitumia, alistuka kusikia kishindo mguuni mwake, na mara damu zikaanza kumtiririka.

Alisema kuwa wakati akishuka kwenye gari hiyo, alipigwa risasi kwenye mguu wake wa kushoto na baadaye alimuona askari wa kike ambaye bado alikuwa ameshikilia bunduki jambo ambalo lilimshangaza.

“Niliposhusha mguu wa kushoto, nilisikia kishindo na maumizu makali sana yakitokea mguuni, sikujua ni nini lakini nilipoinua macho yangu nilikutana na uso wa askari wa kike akiwa ameshika bunduki kuielekezea kwangu, nililia sana na maumivu sikujua kosalangu,” anasema na kuongeza...

“Nilipigwa risasi mbele ya mtoto wangu ambaye wakati huo alikuwa akiumwa pia, sijawahi kukosa jambo lolote nashangaa kwanini nimeadhibiwa kiasi hiki,” aliongea mama huyo huku akibubujikwa na machozi.

Anasema baada ya kujeruhiwa, dereva wa taxi aliyekuwa amemkodi, alimpeleka kituo cha polisi, Iringa mjini ambako alitoa maelezo juu ya tukio hilo akidai askari wa kike ndiye muhusika.

Anasema wakati akitoa maelezo yake, ghafla gari ya polisi , gari hiyo ya polisi ambayo askari aliyempiga alikuwa ameipanda, iliwasili eneo la kituo jambo lililomfanya aweze kumuona tena askari aliyempiga, ambaye alimtambua.
Anasema alipaza sauti kwa uchungu akimuuliza askari huyo sababu za kumpiga na kwamba, kama angekuwa na kosa kwanini asingemchukulia hatua za kisheria tofauti, lakini askari huyo alitabasamu na kuendelea na shughuli zake.

“Nilipofika kituoni nilitoa maelezo yangu na kwa bahati nikamuona polisi aliyenipiga risasi, nililia kwa uchungu na kumuuliza kwanini amenifanyia unyama ule, kwa kweli alicheka tu na kuingia ndani, ndipo nilipopelekwa hospitali ya mkoa wa ajili ya matibabu,” anasema.

Anasema alipelekwa hospitali, na kwamba kutokana na kuwa ilikuwa usiku, ilimlazimu kulala na mtoto wake hospitalini hapo, hadi asubuhi.

Anadai kuwa siku ya pili, askari walikwenda hospitalini hapo na kumchukua ili akawaonyeshe eneo la tukio, alikubali kutoka akiamini wauguzi wanafahamu, na badala yake walimrudisha nyumbani kwake, huku wakimwambia kuwa, hana sababu ya kurudi hospitali tena.

Anasema siku ya pili baada ya kuona hali yake inazidi kuwa mbaya kutokana na risasi kuwa bado mwilini mwake, aliamua kukodi gari hadi hospitali ambako alipokelewa na manesi waliomshangaa kwanini aliondoka bila kuaga.

Anasema alipofika hospitali alipokelewa vyema, akavalishwa shuka jeupe na kuingizwa chumba cha upasuaji ambako alitolewa risasi iliyokuwa bado mwilini mwake.

Anasema kuwa siku iliyofuata walienda askari wawili na ambao walimuuliza kama anamfahamu aliyenipiga risasi, alipowajibu kuwa amfahamu walimuambia haina haja ya kuandika maelezo badala yake waliondoka.

Anasema ilipofika saa 11 jioni, nesi alimpa ruhusa ya kwenda nyumbani eti hali yake imetengemaa, japo bado yeye mwenyewe alikuwa akisikia maumivu makali mguuni kwake.

Hospitali
Kutokana na maelezo ya mwanamke huyo, Mwananchi ilikwenda hospitali ya Mkoa na kukutana na Kaimu Mganga Mfawidhi Dk Oscar Gabone na kuuliza kama Feb 4, hospitali hiyo ilimpokea mwanamke aliyepigwa risasi.
Dk Gabone aliamua kuwaita wauguzi wawili ambao walifika ofisini kwake, na kueleza kwamba ni kweli walimpokea mgonjwa aliyepigwa risasi na kwamba, aliruhusiwa baada ya hali yake kuanza kutengemaa.
“Alikuja hapa akiwa na jeraha la risasi mguuni mwake, tulimpokea kama wagonjwa wengine, alilazwa, akatibiwa na akaruhusiwa baada ya hali yake kutengemaa na si vinginevyo. Tulishangaa siku moja aliondoka bila kuaga, alipokuja asubuhi tulimuuliza kwanini aliondoka?
Alituomba radhi akitusihi tumhudumie, tulimuhudumia vizuri tu,” anasema mmoja wa wauguzi.

Maelezo ya jeshi la polisi
Kwa mujibu wa maelezo ya jeshi la polisi si kweli kwamba mwanamke huyo alipigwa risasi isipokuwa ni kitu chenye ncha kali.
Kaimu Kamanda wa polisi Claus Mwasyeba anasema kuwa uchunguzi wa polisi umebaini kuwa siku hiyo hakukuwa na tukio lolote la mtu kupigwa risasi.
“Tulipata taarifa toka kwenye magazeti na baadaye tukasikia radioni, tulifanya uchunguzi na kubaini kuwa hakukuwapo na tukio lolote la mtu kupigwa risasi,” anasema Mwasyeba.

Kwa mujibu wa Mwasyeba, mlinzi wa Miami, alimchukua mama huyo na dereva na kuwapeleka kituoni ambako alipewa PF 3 na kwenda kutibiwa na kwamba, alikuwa amejeruhiwa na kitu chenye ncha kali nakwamba, suala la kumtambua aliyehusika, mwanamke huyo amekuwa akijikanganya katika maelezo yake.

Mkanganyiko

Upo mkanganyiko wa maelezo na Polisi wametoa tamko lao kwamba, hakukuwa na tukio la kupigwa risasi siku hiyo isipokuwa mama huyo alijeruhiwa mguu wake na kitu chenye ncha kali.

Bado kuna maswali mengi ambayo jamii inajiuliza. Inakuwaje mwanamke aeleze kwamba alipigwa risasi na kumsingizia askari wa kike huku akisisitiza kuwa anamtambua?

Ikiwa alipigwa na kitu chenye ncha kali nani alikuwa muhusika wa tukio hilo? Lakini pia nilipokwenda hospitali niliuliza kama kuna tukio la risasi na nikapewa maelezo kwamba mama huyo alienda kutibuwa na je alipelekwa chumba cha upasuaji kufanya nini?

No comments:

Website counter