|  Mchungaji Ambilikile MwasapileMCHUNGAJI  Ambilikile Mwasapile amesema hivi karibu atahamisha utoaji wa tiba  katika eneo analoishi sasa na kwenda sehemu ambayo itakuwa na nafasi  kubwa zaidi, kwa lengo la kupanua huduma na kubadilisha mazingira  anayoishi.
 Akizungumza juzi mchana kijini hapo, mchungaji huyo  alisema yeye si mganga wa kienyeji, bali anatibu kwa miujiza ya Mungu na  kusisitiza kwamba ili mgonjwa apone anatakiwa kuwa na imani katika  huduma hiyo.
 "Nataka nieleze kidogo kuwa mimi si mganga wa  kienyeji. Tiba yangu ni miujiza ya Mungu ambaye ameamua kuliweka neno  lake katika mti huu ili lilete uponyaji.
 Ameamua kuukomesha ugonjwa wa Ukimwi duniani kabisa," alisema mchungaji huyo na kuongeza:“Kwa  wale wanaoumwa Ukimwi wanapokunywa dawa hii wanapona kabisa. Tiba  itaanza kujidhihirisha ndani ya siku saba. Lakini wadudu hata kama bado  watakuwapo, hawatakuwa na nguvu na katika kipindi cha miezi mitatu,  wadudu wote watakufa kabisa.
 
 Kwa wale wenye kansa, dawa  inamaliza kabisa tatizo hilo, dawa hii inaponya kichaa, kifafa na  magonjwa mengine ambayo mgonjwa atataka apone."Idadi ya wagonjwa  wanaomiminika kwa Mchungaji Mwasapile inazidi kuongezeka siku hadi siku.  Hivi sasa wanakaa foleni kati ya siku tatu na tano kabla ya kupata tiba  hiyo.
 Wengi wanailalamikia Serikali kwa kushindwa kumsaidia  mchungaji huyo kuboresha mazingira ya utendaji kazi wake. Mmoja wa  wagonjwa waliokuwa wakisubiri tiba hiyo, Sara Ibrahim alisema: "Huduma  ni nzuri lakini hakuna ulinzi wa maana. Hakuna 'ambulance' (gari la  wagonjwa), watu wanafia kwenye magari kwa kukosa msaada wa karibu  kuwafikisha kwa mchungaji. Tunaiomba Serikali isaidie huduma hiyo pia  kwa kujenga vyoo, kusambaza maji na kutoa jenereta."
 Licha ya  malalamiko hayo, barabara ya kufika huko inazidi kuharibika na  kusababisha mamia ya wagonjwa na jamaa zao kukwama porini. Zaidi ya  abiria 600 waliokuwa wanatoka Arusha kwenda huko wamekwama umbali wa  kilometa 306 kutokana na ubovu huo.
 
 Mwishoni mwa wiki iliyopita,  Mwananchi ilishuhudia magari 68 yenye uwezo wa kubeba zaidi ya abiria 10  kila moja, yakiwa ama yamepasuka magurudumu au yamepata pancha katika  barabara hiyo iliyojaa mashimo baada ya mvua kubwa kunyesha Jumamosi  iliyopita.
 
 Mmoja wa madereva wa magari hayo ya kitalii, Aman  Mshanga alieleza moja ya sababu za magari hayo kukwama njiani kuwa, ni  pamoja na mengi kutofanyiwa matengenezo kabla ya kuanza safari. Alisema  kutokana na umuhimu wa barabara hiyo katika siku za hivi karibuni,  Serikali inapaswa kuifanyia matengenezo.
 
 Alisema Barabara ya  Arusha kwenda Loliondo, hasa katika Kijiji cha Samunge anakofanyia  matibabu mchungaji huyo itaendelea kuwa mbaya kiasi cha kukosa  mawasiliano kabisa katika siku za hivi karibuni kama hakutakuwa na  jitihada za kuitengeneza.
 
 Hata hivyo, wakati dereva huyo akisema  kwamba sababu za magari hayo kukwama njiani ni kutokana na ukosefu wa  matengenezo kabla ya safari, polisi mkoani Arusha imekuwa ikieleza kuwa  chanzo cha ajali hizo ni mwendokasi wa madereva.
 Mmoja wa  wagonjwa, Anna Ibrahim alisema: "Kila gari linalofika Samunge linatozwa  Sh2,000 lakini barabara bado ni mbovu na hatujui fedha hizo zinakwenda  wapi? Serikali inatakiwa itumie kodi yetu kutuletea maendeleo,” alisema.  Hadi kufikia juzi, idadi ya magari yanayopeleka wagonjwa kwa Mchungaji  Mwasapile yanakadiriwa kufikia 40,000.
 Akizungumzia ongezeko hilo  la wagonjwa wanaokwenda kwake kupata tiba, Mchungaji Mwasapile alisema  hiyo ni sehemu tu ya watu watakaotoka maeneo mbalimbali duniani kuifuata  huduma hiyo kwake... "Watu wataendelea kufurika hapa kutoka kila pembe  ya dunia na maajabu ya Mungu yataendelea kujionyesha."
 
 
 | 
1 comment:
I wish mtu angenipa jibu kwa swali langu moja tu. Tangia lini jamani Mungu anatoa tiba kwa malipo? Suala la uponyaji mimi naliamini kabisa ila hili la kulipisha watu..NEVER!!!
Post a Comment