Monday, March 21, 2011

MMMH HII SASA 'KALI' JAMANI LOOH...

Wavamia msitu Loliondo kusaka dawa Send to a friend

Mchungaji Ambilikile Mwasapile akiweka dawa katika vikombe ambavyo husambazwa kwenye magari kwa wagonjwa na wananchi walifika upata tiba katika kijiji cha Samunge, Loliondo, mkoani Arusha. Picha na Mussa Juma


WAKATI dawa aliyoigundua Mchungaji Ambilikile Mwasapile ikionekana kuwavuta watu karibu nchi nzima kutaka kuinywa, baadhi ya wakazi wa Arusha wameamua kwenda maporini kusaka dawa hiyo.
Taarifa ambazo pia zimemfikia mchungaji huyo mstaafu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), zimeeleza kuwa watu hao tayari wamevamia pori la mlima Sonjo kuchimba dawa anayotumia kutibu.Hata hivyo, Mchungaji Mwasapile alisema haitawasaidia kwa vyovyote kwa sababu ni yeye pekee aliyepewa uwezo na Mungu ili awaponye watu.


Hata hivyo, Mchungaji Mwasapile, ameiomba Serikali kuingilia kati kwa kuwadhibiti watu hao, aliowaita kuwa ni matapeli ambao tayari wamevamia pori hilo kwa sababu watasababishawatasababisha watu wengine kuikosa kwa vile uchimbaji utakuwa ni wa vurugu na pia utasababisha uharibifu wa mazingira.

Akizungumza na waandishi wa habari, mchungaji huyo alisema watu hao, wamekuwa wakiwatumia baadhi ya vijana wa kijiji cha Samunge ambao wanaujua mti wa Mugariga, au Mungamuryogo na wameanza kuchimba mizizi na kusafirisha nje ya kijiji hicho.

"Naomba nitoe angalizo, hii dawa ni mimi pekee ndiye Mungu ameniotesha kuitoa na inakwenda pamoja na maombi sasa hawa wanachimba mizizi na kwenda kutengeneza haitawasaidia ni utapeli," alisema Mchungaji Mwasapile.

Mchungaji huyo aliiendelea kuiomba Serikali kukarabati miundombinu ya kufika katika kijiji cha Samunge kwa sababu sasa mvua zimeanza kunyesha na kwamba siku si nyingi barabara za kumfikia zitakuwa hazipitiki.
Kutokana na ubovu wa barabara hiyo, gari lililokuwa limembeba Waziri Mkuu Mstaafu lilikwama juzi jirani tu na kwa mchungaji huyo sambamba na magari mengine kadhaa.

Kukwama kwa magari hayo, kulitokana na mvua ambazo zimeanza kunyesha na kuharibu barabara ya kwenda katika kijiji hicho, inayotokea eneo la Kigongoni Mto wa Mbu, kupitia kata za Selela, Engaruka na Ngaresero.
Magari mengi yalikuwa yameharibika na kukwama kati kati ya miti juzi, hali ambayo inatishia usalama wa barabara hiyo ambayo ni ya vumbi.

Akizungumzia barabara hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro, Elias Wawa Lali, aliwataka madereva kuwa makini ili kuzuia mfululizo wa ajali.

Katika hatua nyingine, Mchungaji Mwasapile alirudia tena onyo lake la kuwataka watu kuacha kuwapeleka kwake wagonjwa waliotoroshwa hospitali huku wengine wakiwa na chupa za kuongezewa maji mwilini.

"Wanakuja huku wakiwa na Dripu za maji. Sasa hapa sio hospitali ya rufani. Wagonjwa waletwe hapa kwa tahadhari kubwa kwanza barabara zetu sio nzuri," alisema Mwasapile.
Idadi ya magari na watu toka ndani na nje ya nchi inaongezeka katika kijiji hicho na sasa kupata dawa mgonjwa inachukuwa kati ya siku mbili hadi tatu.

Mwandishi wa habari hizi juzi alishuhudia wagonjwa toka nchi za Kenya, Zambia, Malawi, Uganda na Afrika Kusini wakiwa wamepanga foleni ya kupata dawa.

Madaktari wa Moshi
Kutoka Moshi, madaktari mbalimbali wameitaka Serikali kuandaa kongamano la wanasayansi kujadili tiba inayotolewa na Mchungaji Mwasapile, ikiwamo kutolewa kwa ripoti za kisayansi za wagonjwa waliopona. Wakizungumza na Mwananchi, madaktari hao wamedai kisayansi haiwezekani kupima dawa inayotokana na imani ya dini, lakini ni vyema wakapatikana wagonjwa wanaodai kupona wakiwa na kumbukumbu za matibabu ya siku za nyuma.

Mmoja wa madaktari bingwa, Profesa Waitoki Nkya, ambaye sasa amestaafu serikalini alisema Taifa bado liko gizani kuhusu ukweli wa nguvu ya dawa hiyo katika kutibu magonjwa sugu ukiwamo Ukimwi, kisukari na saratani.

Binafsi siamini katika jambo hilo lakini, naishangaa Serikali na vyombo vyake kwamba kweli vimeshindwa kutuambia mgonjwa X wa Ukimwi alikuwa na CD4 200, baada ya kunywa zimeongezeka hadi 1,000?” alijoji.

Profesa Nkya ambaye aliwahi kufanya kazi Hospitali ya Rufaa ya KCMC na kuhamishiwa Hospitali ya Rufaa ya Mbeya kabla ya kustaafu, alisema taifa linaweza kuondokana na giza hilo kwa wataalamu kuthibitisha nguvu ya dawa hiyo.

Profesa Nkya alisema Tanzania kama Taifa haliwezi kuruhusu watu waliokunywa dawa hiyo kujisemea wenyewe kuwa wamepona wakati hakuna hata mmoja anayethubutu kutoa vipimo vya awali na vya sasa kuthibitisha amepona.

Hata hivyo, daktari mmoja ambaye ni mratibu wa Ukimwi kwa zaidi ya miaka 10 sasa, alisema katika suala la Ukimwi bado hajathibitisha nguvu ya dawa hiyo isipokuwa kwa magonjwa ya kisukari na shinikizo la damu (BP).

Kwa kisukari na BP naweza kusema kuna mafanikio kidogo kwa sababu kuna wagonjwa wetu wa kisukari walikuwa katika hatua ya kudungwa sindano kila siku lakini, sasa wana wiki hawajachoma sindano na wako vizuri,” alidai.

Daktari mwandamizi katika Hospitali ya Mkoa Kilimanjaro ya Mawenzi, Dk Issa Mbaga, ambaye alisema anatoa maoni binafsi na sio ya Taasisi yake, alisema tatizo ni waliokunywa dawa kutopima upya kuthibitisha kupona.
Unajua ni vigumu kupima jambo kiimani kama ilivyo kunywa dawa ya Babu kule Loliondo lakini, hawa waliorudi na kutuambia wanaendelea vizuri kwa nini wasipime upya wakatupa ripoti?” alihoji Dk. Issa.

Wazidi kwenda Loliondo
Wakati huo huo, kitimutimu cha wananchi kutaka kwenda huko kimesikika karibu kila mkoa hapa nchini ila tatizo kubwa ni gharama za usafiri pamoja na chakula.Katika Manispaa ya Shinyanga watu wengi wamejitokeza kwenda kujiandikisha ili waende Loliondo baada ya kupata taarifa kuwa Mbunge wao, Steven Masele amekusudia kuwagharimia usafiri.

Wananchi hao walikusanyika jana kwenye ofsi ya mbunge kujiandikisha na awamu ya kwanza ya kundi la watu hao ilitarajia kuondoaka jana.Akizungumza na Mwananchi kwa njia ya simu mbunge huyo alisema kuwa amegharimia safari hiyo bila kujali wanaoenda ni wagonjwa au la.

Hata hivyo, alisema wale wenye uwezo washiriki watapaswa kuchangia kiasi kidogo cha fedha ili kutoa nafasi ya watu wengi wanaomiminika katika ofisi yake ili kujiandikisha kwa safari.

Mwanza nako
Jijini Mwanza nako watu wengi wamesikika wakitaka kupata tiba hiyo miongoni mwao ni wafanyakazi Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza ambao tayari wameanza kuchangishana ili kugharimia safari.

Habari zilizopatikana toka ofisi ya mkuu wa mkoa huo na kuthibitishwa na Ofisa Usafirishaji wa Mkoa, William James zilieleza kwamba wafanyakazi hao wamekusudia kwenda kabla ya kufika mwishoni mwa mwezi huu.

James alisema hadi jana wafanyakazi 26 walikuwa wamejiorodhesha kwenda na kila mmoja tayari amelipa Sh80,000.Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Abbasi Kandoro, alielezea kuwa hahusiki katika mpango huo kwa sababu hiyo ni safari binafsi.“Hii siyo suala la ofisi ni wafanyakazi binafsi, ndiyo maana uliponiuliza nilishangaa na kwa vile mimi sikuwepo nilikuwa sijui lolote," alisema Kandoro.

Morogoro nao wamo
Kutoka mkoani Morogoro, inaripotiwa kuwa Watu Wanaoishi na Virusi vya Ukimwi (Wavumo) wamemwomba mbunge wa jimbo la Morogoro Mjini, Aziz Abood kuwapa msaada wa kuweza kufika Loliondo ili kupata dawa ya 'Babu'.Akizungumza na waandishi wa habari jana katika ofisi za Wavumo, katibu wa kikundihicho, Said Shija alisema kuwa wao nao wamehamasika na dawa hiyo.

Alisema kuwa wao wana imani na dawa hiyo na kwamba kinachowashinda hadi sasa kufika huko Loliondo ni kwamba hawana uwezo na kumudu gharama za usafiri.

Askofu Kakobe
Jijini Dar es Salaam, Askofu wa Kanisa la Full Gospel Fellowship, Zacharia Kakobe, ameendelea kutoa maneno ya shutuma dhidi ya mchungaji Mwasapile.

Hii ni baada ya Mwasapile kusema kwamba anawakaribisha ili kunywa dawa hiyo licha ya kumdharau pamoja na tiba anayoitoa. Kakobe amerusha kombora lingine akidai haendi ng’o na yeye sio nyasi zinazotikiswa na upepo kama watu wengine wanaokwenda huko.

Mwasapile maarufu kwa jina la ‘Babualiwajibu viongozi hao waliomtuhumu kuwa tiba anayoitoa ni ya nguvu za giza, akisema kuwa waliotoa tuhuma hizo wana mtazamo wa kifedha zaidi na sio imani.

Akizungumza na gazeti hili jana kwa simu, Askofu Kakobe alisema kwanza anawahurumia wanaoendelea kwenda huko kwa sababu tayari wameshatekwa na huduma hiyo ya 'kitapeli.'

Siwezi kwenda kunywa dawa hata kidogo, kwa sababu mimi sio nyasi zinazotikiswa na upepo kama wengine waliokwenda huko,” alisema Askofu Kakobe.

Ajali Loliondo
Kwa upande mwingine, ajali za magari yanayoenda, au kutoka kwa 'Babu' nazo zinaendelea kuongezeka.
Jumatano iliyopita mtu mmoja alikufa na wengine watano kujeruhiwa baada ya gari lililokuwa njiani kwenda Loliondo kupasuka tairi na kupinduka eneo la Makuyuni, wilayani Monduli.

Ajali hiyo inafanya idadi ya watu waliokufa tokea msururu wa watu toka pembe zote za nchi walipoanza kumimika katika kijiji cha Samunge, Wilayani Ngorongoro kufiki saba.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Akili Mpwapwa alithibitisha kutokea kwa ajali hiyo. Alisema ajali hiyo ilitokea saa nane mchana kufuatia kupasuka kwa gurudumu la nyuma la gari hilo, kisha kupinduka.
Alimtaja aliyefariki dunia kuwa ni Fatuma Badru (34), mkazi wa Soweto mjini Moshi.

Aliwataja majeruhi kuwa ni Ruth Lyimo, Mary Sembugao na Salma Badru na mmoja aliyefahamika kwa jina moja la Omary.

Habari hii imeandikwa na Mussa Juma-Loliondo, Daniel Mjema-Moshi, Suzy Butondo-Shinyanga, Frederick Katulanda-Mwanza, Filbert Rweyemamu-Arusha, Lilian Lucas-Morogoro na Elizabeth Suleyman - Dar.


No comments:

Website counter