Thursday, March 17, 2011

KAMA ULIKUWA NA MPANGO WA KUFUNGUA BAR KULE 'ZENJ' BASI FUTA ILO WAZO...

Wimbi la kuchoma moto baa laongezeka Zanzibar




Wimbi la ulipuaji moto wa baa limeendelea kuikumba Zanzibar baada ya baa nyingine tatu kuchomwa moto katika Mkoa wa Mjini Magharibi na Mkoa wa Kusini Unguja.

Matukio hayo yamefanya idadi ya baa zilizochomwa moto kufikia sita katika kipindi cha mwezi mmoja hapa Zanzibar na kusababisha hali ya wasiwasi mkubwa kwa wenye biashara ya kuuza pombe.

Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Ahmada Abdallah, alithibitisha kutokea kwa matukio hayo na kusema Polisi imeanza kufanya uchunguzi.

Alizitaja baa zilizochomwa moto katika Mkoa wa Mjini Magharibi kuwa ni Festa Baa ya eneo la Bububu Kitosani na Lukenge iliyopo katika eneo la Jang’ombe Urusi.

Alisema watu wasiojuilikana walichoma moto baa ya Festa saa 8:00 usiku na kusababisha hasara kubwa kabla ya kikosi cha kuzima moto kufika katika eneo hilo na kuuzima moto huo.

Kamanda Ahmada alisema tukio lingine lilitokea saa 9:00 usiku baada ya watu wasiofahamika kuichoma moto baa ya Lukenge eneo la Jang’ombe na kusababisha hasara ya zaidi ya Shilingi milioni moja baada ya upande mmoja wa paa la baa hiyo kuteketea kabisa kwa moto huo.

Alisema baa zote zilikuwa zimeezekwa kwa makuti na matukio hayo yalitokea usiku wa Machi 12, mwaka huu.

Alieleza baa ya Lukenge inamilikiwa na Simon Kunambi, wakati baa ya Festa inamilikiwa Mussa Paulo, wakazi wa Zanzibar.

Alisema idadi ya matukio ya baa kuchomwa moto katika mkoa wake imefikia matano na hakuna mtu aliyekamatwa na kufikishwa mahakamani. Baa nyingine zilizochomwa moto ni Peace and Love iliyopo mtaa wa Chumbuni, Migombani Bar iliyokuwa kati kati ya Mji Mkongwe Zanzibar na baa moja iliyopo eneo la Mwanyanya, nje kidogo ya mji wa Zanzibar.

“Polisi tunachukia vitendo vya baa kuchomwa moto kwa vile tabia ya kujichukulia sheria mkononi ni kinyume na utawala wa sheria na tutaendelea kuwasaka wahusika na kuwafikisha mbele ya sheria,” alisema.

Wakati huohuo, baa marufu ya MK iliyopo Fuoni Meli Tano, imeteketezwa kabisa kwa moto na watu wasiojuilikana mwishoni mwa wiki iliyopita.

Habari zilizopatikana kutoka kwa baadhi ya majirani katika eneo hilo zlisema moto huo ulianza kuwaka usiku na kusababisha baa hiyo kuteketea yote, lakini juhudi za kumpata Mkuu wa Upepelezi katika mkoa huo hazikufanikiwa baada ya Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kusini Unguja, Augostine Olomy, kuwa nje ya Zanzibar.

No comments:

Website counter