Monday, March 21, 2011

HAKI YA MUNGU SIMBA 'MKIJIPANGA' MTAWATOA HAWA WACONGO...
Image
Kikosi cha TP Mazembe


Habari zinazosomwa zaidi:

SIMBA sasa inahitaji ushindi wa mabao 2-0 itakaporudiana na TP Mazembe wiki mbili zijazo ili isonge mbele katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Hatua hiyo inatokana na kipigo cha mabao 3-1 ilichokipata jana kutoka kwa TP Mazembe katika mchezo wa kwanza raundi ya kwanza Ligi ya Mabingwa Afrika uliofanyika Uwanja uitwao Stade de La Kenya wenye uwezo wa kuchukua watazamaji 35,000, ambao ulijaa, huku wenyeji wakiwa na vikundi karibu tisa vya ushangiliaji.

Ni matokeo ambayo yalipokewa kwa furaha na wachezaji wa Simba akiwemo Kocha Mkuu, Mzambia Patrick Phiri, ambaye alisema amekubali matokeo na watajipanga kuhakikisha wanapata ushindi zitakaporudiana Dar es Salaam na kusahihisha makosa.

Katika mchezo huo, Patou Kabangu aliipatia TP Mazembe bao la kuongoza dakika ya 11 kutokana na mpira wa adhabu walioanzia na wachezaji wa Mazembe na kupiga shuti lililomshinda kipa Juma Kaseja.

Dakika ya 24, Narlise Ekanga alifunga bao la pili baada ya kugongeana pasi na Alain Kaluyitika mbele ya mabeki wa Simba waliojichanganya na kuukwamisha mpira wavuni.

Simba ingeweza kuwa ya kwanza kupata bao baada ya kuanza mchezo, lakini ilikosa umakini katika umaliziaji, kwa washambuliaji wake Emmanuel Okwi, Patrick Ochan, Mbwana Samatta na Mussa Mgosi kushikwa na vigugumizi vya miguu kila walipokaribia lango la TP Mazembe lililokuwa linalindwa na kipa Kidiaba Muteba.

TP Mazembe ambao ni mabingwa watetezi wa ligi hiyo, ambapo Desemba mwaka jana ilikuwa timu ya kwanza Afrika kucheza fainali ya klabu bingwa ya dunia na kufungwa mabao 3-0 na Inter Milan, ilifunga bao la tatu dakika ya 66 mfungaji akiwa Narlise Ekanga akiunganisha mpira wa kona.

Dakika 10 baadaye Simba iliyofikia hatua ya kuvaana na Mazembe baada ya kuiondoa Elan de Mitsoudje ya Comoro katika mchezo wa hatua ya awali kwa jumla ya mabao 4-2, ilipata bao kwa mkwaju wa penalti iliyofungwa na Emmanuel Okwi.

Penalti hiyo ilitolewa na mwamuzi Younis Yassek wa Misri baada ya kipa Kidiaba Muteba kumuangusha Okwi eneo la hatari katika harakati za kuokoa.

Simba ilizinduka zaidi kipindi cha pili baada ya kufunga bao, huku kipa wake Kaseja akiokoa michomo kadhaa tofauti na hali ilivyokuwa kipindi cha kwanza.

Simba: Juma Kaseja, Haruna Shamte, Amir Maftah, Juma Nyoso, Kelvin Yondani, Jerry Santo, Amri Kiemba, Patrick Ochan, Emmanuel Okwi, Mbwana Samatta/Nico Nyagawa na Mussa Mgosi/Ali Mohammed.

Mazembe: Robert Kidiaba, Pamhile Mihayo, Janivier Besala, Jean Kasusula, Joel Kihwaki, Benza Bedi, Patou Kabangu/Given Singuluma, Narlise Ekanga, Alain Kaluyituka, Rainford Kalaba na Deo Kanda.

No comments:

Website counter