JK aunga mkono Dowans isilipwe | Send to a friend |
|
RAIS Jakaya Kikwete jana alitumia maadhimisho ya miaka 34 ya CCM kuvunja ukimya na kuzungumzia sakata la malipo kwa Kampuni ya kufua umeme ya Dowans kiasi cha Sh94 bilioni akisema amaunga mkoTanesco isilipe deni la Dowans. "..Nataka kuwahakikishia kuwa na mie ni miongoni mwa wale wasiotaka Tanesco ilipe..," alisema Rais Kikwete akizungumzia sakata hilo. Kauli hiyo ya Rais Kikwete kuhusu Dowans ilikuwa ikisubiriwa kwa hamu na Watanzania, ambao kwa kipindi kirefu wamekuwa wakitoa maoni mbalimbali,huku baadhi yao wakienda mahakamani kupinga kampuni hiyo isilipwe. Akihutubia wananchi katika kilele cha Sikukuu ya kuzaliwa kwa CCM, ambazo kitaifa zilifanyika mkoani Dodoma jana Kikwete alisema ameamua kusema wazi baada ya kupata shinikizo kutoka kwa watu mbalimbali waliosema kuwa amekuwa kimya juu ya Dowans. “Wapo wanaosema niko kimya au nashindwa kuchukua hatua, kwa sababu marafiki zangu wamehusika. Nawalinda. Kwa sababu hiyo, nikaona nami nisema angalau watu wanisikie, lakini sina la ziada ni yale yale yaliyokwishasemwa. “Msemo wa wahenga wa akutukanae hakuchagulii tusi hapa umetimia. Napenda kuwahakikishia wana-CCM na wananchi wenzangu kuwa, sina uhusiano wowote wa kimaslahi, kwa namna yoyote ile na kampuni ya Dowans,” alisema Kikwete. Rais Kikwete alisema hakutaka kuzungumza kuhusu Dowans kwa kuwa tayari lilikuwa limeshatolewa ufafanuzi na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda pamoja na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, John Chiligati . “Sikuona umuhimu wa kufanya hivyo kwa sababu viongozi wenzangu wameelezea kwa ufasaha uamuzi wa Kamati Kuu na ule wa kikao cha pamoja cha Wabunge wa CCM,” alisema Rais Kikwete. Alisema kuwa taarifa ya kutaka Tanesco iilipe Dowans Sh94 bilioni imeshtua wengi na kwamba yeye baada ya kupata taarifa hiyo aliuliza na kupewa ushauri mbalimbali. “ Wapo waliosema lazima tulipe, wapo waliosema tusilipe, wapo waliosema tusiharakishe kulipa kwani kuna uwezekano wa kutokulipa kwa kutumia sheria,” alisema na kuongeza “ Uamuzi wangu ukawa tusiharakishe kulipa, tutafute njia za kuepuka katika kulipa. Ndiyo maana ya taarifa ya Chiligati na ile ya Waziri Mkuu,” alisema Kikwete. Alisema kuwa ni mzigo mkubwa kwa Tanesco kuilipa Dowans, hivyo ifanyike kila njia ili kuepuka kulipa deni hilo. “ Tumewataka wanasheria wetu wasaidiane na wale wa Tanesco kuhakikisha hilo halitokei. Nataka kuwahakikishia kuwa na mie ni miongoni mwa wale wasiotaka Tanesco ilipe," alisema na kusisitiza: "Kauli za mimi kuhusika na Dowans inanishangaza, maana nisingeamua hivyo katika Kamati Kuu(CC) na Kamati ya Wabunge wa CCM. Ama kweli akutukanae hakuchagulii tusi”alisema Kikwete." Alisema kutokana na ukimya wake maneno mengi yalisemwa ikiwa ni pamoja na kuhusishwa na kampuni hiyo Dowans na kufafanua kwamba jambo jingine lililomfanya kuzungumza kuhusu Dowans ni kauli kwamba hawezi kuzungumza kwa kuwa kampuni hiyo inahusishwa na marafiki zake. “ Sina hisa zozote wala manufaa yoyote yale, Pia sina ajizi wala kigugumizi cha kuchukua hatua kwa sababu ya rafiki yangu au hata kama angekuwa ndugu yangu kahusika. Maamuzi yaliyofanywa na Kamati Kuu na Kamati ya Chama ya Wabunge wa CCM yalifanywa chini ya uogozi wangu,”alisema Kikwete. Kuhusu suala la Katiba, Rais Kikwete alisema siyo sera ya wapinzani bali ni mali ya CCM ambayo tangu mtangulizi wake Benjamini Mkapa alishaianzisha, hivyo akasema na yeye ni muumini mzuri wa kutaka mabadiliko. Alisema kuwa atawaambia wasaidizi wake waharakishe kupeleka muswada bungeni ili uweze kujadiliwa na wabunge ambao wataona ni namna gani mchakato huo utakavyotekelezwa ili kupata katiba mpya. Kuhusu matatizo ndani ya CCM, alisema bila ya chama hicho kufanya mageuzi makubwa katika kubadili muundo na uongozi, kitakufa kifo cha mende. Kikwete pia aliwaeleza mamia ya watu waliohudhuria kilele cha sherehe hizo za miaka 34 ya CCM, kuwa chama hicho kimeishiwa fedha na kwamba yako maeneo yanayosababishwa na viongozi wasiokuwa wabunifu. Mwoshoni mwa mwaka jana gazeti hili liliwahi kuchapisha kichwa cha habari kuwa CCM hoi kifedha baada ya kupata habari kutoka ndani yua chama hicho. Alisema katika mabadiliko makubwa yanayotarajia kuja ndani ya chama hicho kikongwe nchini, yataanza mara moja mwishoni mwa mwezi ujao wakati Kamati Kuu itakapokutana kupokea tathmini ya uchaguzi. Akitumia maneno ya ukali Kikwete alisema: “Mabadiliko hayo yanatakiwa kuanza mara moja bila kuchelewa kwani ukongwe wa chama chetu pamoja na baadhi ya viongozi wanaweza kuwa ni mzigo unaokisumbua chama”. Mwenyekiti huyo alisema mabadiliko hayo yanatakiwa kuendana sambambana matakwa ya watu wakiwemo kundi kubwa la vijana, ili wasije kiona chama hicho kuwa ni mzigo usiobebeka. “Lazima chama kianze mchakato wa mageuzi kwani kuwepo kwa muda mrefu ndio hatari ya chama chetu, lakini pia tabia za baadhi ya viongozi zinaweza kuwa ni sehemu nyingine ya hatari hiyo hivyo. Nasema lazima chama kiwe kama nyoka anayeweza kujivua magamba yake na kuwa mpya wakati wote hilo litajadiliwa katika vikao vya kamati na utekelezaji wake utaanza mara moja ili kuongeza mvuto ndani ya chama chetu”. Alisema chama kinatakiwa kukimbia kutokana na hali halisi ya namna walivyoiona katika mchakato wa uchaguzi ulipita hivyo wale ambao wanakwenda mwendo wa kinyonga lazima watabwagwa kuanzia Machi mwaka, huku akisisitiza kuwa mvuto huo uwapendezeshe vijana. Kuhusu suala la mapato, alisema kwa sehemu kubwa CCM imeacha kusimamia vyanzo vyake na badala yake imekuwa ikitegemea zaidi fedha za ruzuku ambazo mara baada ya kupungua kwa viti bungeni, sasa ruzuku hiyo inaishia kulipa mishahara ya wafanya kazi tu. Katika hatua nyingine, Rais Kikwete alisema hata kwa miujiza hawezi kutimiza matakwa ya Watanzania wote katika kipindi cha uongozi wake wa miaka 10. Alitolea mfano kuwa hata hayati Mwalimu julius Nyerere alishindwa kumaliza mambo yote ingawa alikaa kwa muda mrefu Ikulu kuliko marais wengine, hali kadharika pamoja na watangulizi wake akiwemo Benjamini Mkapa pamoja na Ali Hassan Mwinyi. “Watanzania wasitegemee kuwa nitafanya mageuzi makubwa hata Mungu mwenyewe hakumaliza kuiumba dunia kwa siku moja, lakini pia hata Mwalimu aliyekaa muda mrefu hakumaliza matatizo ya Watanzania kwa kipindi chake”. Kwa upande wa wananchi wa Dodoma ambao walimpa Kikwete zaidi ya asilimia 81 ya kura za urais , alisema mji huo utaboreshwa pamoja na kufikiria kuipanua Ikulu ya Chamwino iliyo nje kidogo ya mji, ikiwa ni pamoja na kujenga nyumba ya rais. |
No comments:
Post a Comment