
Mitambo ya Kuzalisha umeme wa dharura ya Dowans iliyopo Tanesco Ubungo Jijini Dar es salaam.
MITAMBO ya kuzalisha umeme wa dharura ya Dowans iliyoibua mjadala mpana katika jamii kutokana na utata wa mkataba wake, huenda ikawashwa wakati wowote kwa malengo ya kupunguza tatizo la mgawo wa umeme linaloendelea nchini.
Habari zilizopatikana jana mjini Dodoma na kuthibitishwa na baadhi ya wabunge waliohudhuria kikao cha Kamati ya Nishati na Madini walisema kuwa hoja ya kuwashwa kwa mitambo hiyo ilijadiliwa kwa lengo la kupunguza makali ya umeme nchini.
Chanzo chetu cha habari kilisema kwamba wajumbe wa kamati hiyo walikuwa wakijadili ama waitaifishe mitambo hiyo au waingie mkataba wa dharura ili ianze kutoa umeme kwa siku mbili zijazo.
"Suala lililozua mvutano baina ya wabunge ni ama kutaifisha au kuwapo mkataba wa dharura na kampuni inayomiliki mitambo hiyo,"alisema mbunge mmoja aliyekuwapo katika kikao cha kamati hiyo.
Vyanzo hivyo vya habari vilieleza kuwa mpaka jana usiku kikao kilikuwa kikielendea na kwamba baada ya kumaliza kikao hicho wangeshauriana na Spika wa Bunge kueleza msimamo wao.
Alipoulizwa Mwenyekiti wa Kamati ya Nishati na Madini, January Makamba kilichokuwa kikijadiliwa ndani ya kikao, alisema : " Kikao bado kinaendelea. Tutashauriana na Spika baada ya hapa. Tunatarajia kufanya maamuzi yenye maslahi ya kwa nchi nzima."
Awali jana asubuhi wakizungumza katika kipindi cha Jambo Tanzania cha TBC1 , Makamba, Waziri Kivuli wa Nishati na Madini, John Mnyika walipendekeza yafanyike maamuzi magumu ili kuwezesha mitambo ya Dowans kuwashwa ili kupunguza makali ya mgao.
Kwa mujibu wa Makamba, mitambo ya Dowans inazalisha MW 120 na itasaidia kupunguza makali ya mgao kwa asilimia 60 mpaka 70. Wote walitambua uwepo wa suala la Dowans mahakamani.
Hata hivyo, Mnyika alipendekeza sheria ya uhujumu uchumi itumike katka suala la Dowans huku akisema kuwa hawezi kwenda ndani zaidi.
Mniyka alimaanisha kuwa mitambo ya Dowans inapaswa kutaifishwa kwa sababu ya ukweli kuwa mkataba wa Dowans/Richmond ni wa kitapeli na huwezi kuwa na mgawo wakati mitambo iko pale imezimwa.
Wakati huo huo, Makamba alipendekeza kuwa usainiwe mkataba wa muda mfupi wa miezi mitatu na hao wenye mitambo ili kuiwezeshwa kuwashwa. Alipendekeza uangaliwe utaratibu ambao hautaathiri kesi iliyopo Mahakamani.
Spika Makinda azuia Bunge kujadili umeme
SPIKA  wa Bunge, Anne Makinda jana alizuia kufanyika kwa mjadala wa umeme  bungeni baada ya mbunge wa Ubungo na Waziri Kivuli wa Nishati na Madini,  John Mnyika kutoa hoja ya dharura.
Mnyika alitoa hoja ya kutaka  kuahirishwa kwa shughuli za Bunge na kujadili suala la dharura akinukuu  kifungu cha 47(1) na 55 (3) vya Kanuni za Bunge vinayoruhusu mbunge  kutoa hoja ya kujadili jambo la dharura na muhimu kwa jamii baada ya  kipindi cha maswali na majibu.
Kifungu hicho kinasema: "Baada ya  muda wa maswali kwisha, Mbunge yeyote anaweza kutoa hoja kuwa shughuli  za Bunge kama zilivyoonyeshwa  kwenye orodha ya shughuli, ziahirishwe  ili Bunge lijadili jambo halisi la dharura na muhimu kwa umma."
Akitoa  hoja hiyo, Mnyika alisema; " Hoja ya dharura." kauli hiyo ilipokelewa  kwa swali kutoka kwa Spika Makinda aliyeuliza: "Dharura gani tena,  usianze kwa hotuba."
Ndipo Mnyika alipotoa maelezo ya hoja yake  ya dharura ambapo hata hivyo, Spika Makinda aliipangua na kuizima akitoa  sababu za kutoikubali.
"Kwanza tusubiri, kamati hii ndio kwanza  imeanza kazi, wamefanya kiako chao kimoja, juzi walienda kuangalia Bwawa  la Mtera, wamepanga kukutana Dar es Salaam, tusubiri," alisema Makinda  akimuuliza katibu wa shughuli za Bunge kuashiria waendelee na shughuli  nyingine.
Hata hivyo, jana mchana Kamati ya Nishati na Madini  jana ilikutana kwa dharura kujadili suala hilo huku Mwenyekiti wake  akiahidi kukutana na wanahabari, lakini alishindwa kueleza kuwa walikuwa  wakipumzika kabla ya kuendelea tena na kikao na kuahidi kutoa taarifa  kesho Alhamisi.
Hatua za kuzuia mgawo
Wakati  huohuo, Serikali imetolea tamko tatizo la mgawo wa umeme nchini na  kutaja hatua sita za dharura ilizochukua katika kukabiliana na tatizo  hilo sugu.
Akizungumza bungeni jana, Waziri wa Nishati na Madini,  William Ngeleja alitaja utekelezaji wa miradi ya umeme katika kipindi  kifupi na cha kati kuwa moja ya hatua hizo zilizochukuliwa kumaliza  tatizo hilo.
Waziri Ngeleja alitoa tamko hilo baada ya Spika wa  Bunge, Anne Makinda, kumtaka afanye hivyo ili kumaliza kiu ya wabunge wa  upinzani walioitaka Serikali itolee kauli suala hilo ili wananchi wajue  hatima yake.
Februari 11 mwaka huu Kiongozi wa Kambi ya Upinzani  bungeni, Freeman Mbowe katika swali la nyongeza, alimtaka Waziri  Ngeleja kutolea kauli tatizo la umeme, lakini Spika Makinda aliizima  hoja hiyo akisema haingekuwa rahisi kwa Waziri huyo kuzungumzia suala  hilo muhimu katika kipindi cha maswali ya papo kwa hapo.
Na jana  baada ya kupata fursa ya kuzungumzia tatizo hilo la mgawo wa umeme  Ngeleja alisema Serikali kwa kushirikiana na Tanesco imechukua hatua  sita tofauti.
Ataja hatua hizo za dharura kuwa ni pamoja na  kuhakikisha fedha za kununulia mafuta ya kuendeshea kituo cha kuzalisha  umeme cha IPTL zinaendelea kupatikana kwa wakati ili kizalishe kiwango  cha Megawati 80 ambacho ni cha juu.
Pia kuharakisha mchakato wa  kukodi mitambo ya dharura yenye uwezo wa kuzalisha zaidi ya megawati 260  endapo mvua za kutosha hazitanyesha kuwezesha ongezeko la umeme
unaotokana  na maji  na kutekeleza mpango wa kupanua miundombinu ya kusafuisha na  kusafirisha gesi asilia kutoka visima vya Songosongo hadi Dar es Salaam.
Nyingine  ni kuhakikisha miradi ya kudumu ya kuzalisha umeme ya Megawati 100  itakayofungwa Ubungo, Dar es Salaam kwa kutumia gesi asilia na mitambo  ya megawati 60 itakayofungwa Mwanza kutumia mafuta mazito inakamilishwa  kama ilivyopangwa Desemba 2011 na Januari 2012.
Ngeleja alitaja  hatua nyingine kuwa ni kuendelea kutekeleza miradi ya kupunguza upotevu  wa umeme kutoka asilimia 21 ya sasa hadi asilimia 15 kati ya mwaka 2011  na 2015, pamoja na Tanesco kusimamia mgawo wa umeme kwa umakini zaidi na  kuhakikisha upatikanaji wa umeme katika shughuli za uzalishaji, sehemu  nyeti za huduma za jamii, ulinzi na usalama.
Alisema kuwa wizara  yake kwa kushirikiana na Tanesco inaendelea kusimamia utekelezaji wa  programu ya kuongeza uwezo wa kuzalisha umeme katika kipindi kifupi cha  2011 hadi 2015 ili kuepusha tatizo la mgawo wa umeme siku za usoni  ambapo alitaja miradi tofauti saba.
 
No comments:
Post a Comment