Mwanamke apigwa kikatili na mume kisa ndama kufariki | Send to a friend |
|
WAKATI wanaharakati wa masuala ya jinsia wakiumiza vichwa jinsi gani wataondoa ukatili wa kijinsia ulioota mizizi barani Afrika, bado vitendo hivyo vinaendelezwa kila kukicha. Sarah Nyamhanga (24) mkazi wa kitongoji cha Tamukeri wilayani Serengeti anasema, mume wake alimfanyia ukatili huo kwa kile alichodai uzembe wa kumuacha ndama anafariki muda mfupi baada ya kuzaliwa. “Ilikuwa ni Januari 15, 2011 nikiwa nyumbani na mume wangu alijua fika kuwa nina wiki tatu toka nijifungue mwanangu wanne lakini, aliniamuru kuchunga ndama aliyezaliwa na yeye akaenda kunywa pombe zake,”anasema Sarah. Anasema kwa kile ambacho hata yeye hakukijua, ndama yule alikufa na alichukulia kuwa ni tukio la kawaida na ndipo alipojikuta akikaribia kupoteza uhai wake. "Aliporudi tu kutoka katika pombe zake kitu cha kwanza kuniuliza ilikuwa ni wapi alipo ng’ombe wake, nikamwambia amekufa, akaanza kutukana na kisha akaenda nje kuleta kamba akanifunga miguu,mikono na shingo na kufunga kwenye tendegu la kitanda na kuanza kunipiga kwa fimbo huku akidai ndama wake,”anasema mama huyo huku amelala na kichanga chake. Sarah anasema, alipigwa na kujeruhiwa vibaya huku mwanaume huyo akisisitiza kuwa atamuua kama alivyokufa ndama wake na hata aliporidhika kuwa amempiga vya kutosha kiasi cha kutoweza kutembea alimfungia ndani ya nyumba na kuondoka. "Baada ya kunipiga alienda kwa wake zake wengine kwani mimi ni mke wa tano, nikabaki ndani na kichanga na wanangu wengine ingawa bado wadogo walikuwa wananisaidia kwa shida," anaeleza Sarah. Mwanamke huyo anasema kuwa aliendelea kutaabika ndani na vidonda vikaanza kuoza na kutoa harufu kwani hakuwa na uwezo hata wa kunyanyuka kwani msaada alioupata ni kutoka kwa watoto wake wadogo. “Nilikata tamaa nikajua ninakufa maana hapakuwa na msaada, maumivu makali yalikuwa yananisumbua, pembeni mwanangu analia anahitaji kunyonyeshwa, wengine nao wanahitaji niwahudumie, nilijiona nakufa kwa kweli,” anasema. Sarah anafafanua kuwa, ukatili aliofanyiwa ulimfikisha wakati akatamani bora ajitoe roho kuliko kuishi akijiona anaoza angali hai “Nikiwa katika hali hiyo, Januari 20 mama yangu alifika akitokea Kenya. aliponiona alilia maana hakuamini, alikuja na furaha ya kuja kubeba mjukuu lakini mimi nilisema Mungu alimleta kunikomboa maana kama si yeye nadhani nisingekuwa hai,” anasema Sarah. Anasema kuwa mama yake alichukua jukumu la kwenda kwa Mwenyekiti wa Kitongoji kutoa taarifa ya unyama huo ambapo kiongozi huyo akiongozana na watu wengine walifika kumwona. “Walistuka sana kuniona niko hivyo, kwanza harufu iliwatisha sana wakamwamuru mwanaume huyo anipeleke hospitali kwa ajili ya matibabu lakini hakufanya hivyo kwani aliogopa angeombwa PF3 hivyo akanipeleka duka la dawa na kununua vidonge kisha akaniacha hapo,” anaeleza Sarah. Kitendo cha kumtelekeza hapo kiliwaudhi watu wengi ndipo mmoja wa maaskari wa wanyama pori Halmashauri ya Wilaya, Wambura Mgemu alipiga simu polisi na ndipo akaweza kufikishwa hospitalini hapo. Hata hivyo, hakukuwa na mtu wa kumuuguza hali ambayo ilipelekea kila anapotakiwa kutoka anasaidiwa na wauguzi ama wanafunzi wa Chuo cha Uganga na Uuguzi cha Kisare kwa kumsukuma kwenye baiskeli maalum. “Tangu nimeingia hapa hajaja mtu zaidi ya mama aliyenifikisha kisha akaondoka kwenda Kenya kuwafuata ndugu zangu, hapa hata kula nasaidiwa na wasamaria wema walioko humu, sijui kama wasingenisaidia ingekuwaje maana hata maziwa kifuani yanafikia wakati yanakauka maana sili vizuri na mwanangu sijui kama atakuja kuwa na afya nzuri,” analalamika. Alipotakiwa kueleza madai yaliyotolewa na mumewe mara baada ya kukamatwa na polisi kuwa alimshika ugoni, alidai ni uongo wa hali ya juu kwani yeye hajafanya hivyo. “Huyo anataka kupotosha ukweli wa mambo maana mimi kwanza nina wiki tatu tangu nimejifungua ,nina tamaa gani hiyo ya kufanya ngono, anashindwa kuwa mkweli tu, kama ni ugoni alinishika na mwanamme gani mbona hamtaji?” Alipododoswa kama yuko tayari kumsamehe mumewe baada ya kukiri kosa ili waweze kuishi tena, alikataa na kudai kuwa yuko tayari kwenda mahakamani kumtolea ushahidi ili afungwe kwa kuwa alikusudia kumuua. Baadhi ya wagonjwa waliolazwa wodi hiyo ya wanawake wamesema kuwa hata kama ni mapenzi kwa mume, kwa hali kama hiyo haitakiwi kuvumilia na kuwa ukatili wanaofanyiwa ni kutokana na mfumo dume na kiasi kikubwa cha mahari kilichotolewa. “Ukiolewa inakuwa kama sasa unakwenda kusulubiwa na kukitokea umetendewa unyama kama huo ukirudi nyumbani nako unarudishwa kwa madai kuwa ng’ombe za kurudisha hawana na maisha ndivyo yalivyo,” wanaeleza wanawake hao. Hata hivyo, walimtaka Sarah kuangalia maisha yake kwa kuwa yeye alipotoka Kenya na kuingia kijijini humo aliolewa na mwanamke maarufu kama Nyumba Ntobhu na kuwa mwanamme huyo alimtoa huko alikokuwa ameolewa na mwanamke mwenzake. “Kwanza huyu alikuwa ameolewa na Nyumba Ntobhu, mwanamme kamtoa huko halafu anakuja kumtesa namna hiyo, vipi angekuwa amemtolea mahari si angemuua kabisa? Wanahoji wagonjwa wenzake. Mganga wa zamu Tanu Warioba anakiri kuwa Sarah kaumizwa sana na haijajulikana kama ataweza kupona hiyo miguu hasa mmoja kwa kuwa inaonekana alimpiga kwa lengo la kuivunja vunja. "Tunaendelea na vipimo zaidi kubaini mfupa umepasuka kwa kiasi gani, ingawa tunajitahidi lakini bado hajaweza kutembea, inaelekea kipigo kilikuwa kikali sana," anasema mganga huyo. Naye Mratibu Msaidizi wa Mpango wa Kukomesha Vitendo vya Ukatili wa Jinsia na Ukeketaji Wilaya ya Serengeti kupitia Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) Sophia Mchonvu, anasema, ukatili aliofanyiwa Sarah hautakiwi kuvumiliwa na mhusika anatakiwa kuchukuliwa hatua kali. “Vitendo vya ukatili wa kijinsia vinazidi kuongezeka kila kukicha, madhara yake ni makubwa kwa wanawake na hata watoto, Sarah alipigwa akiwa na kichanga, mwanaume bila kujali kuwa alikuwa anahatarisha maisha ya watu wawili,” anasema. Anasema wanawake wanatakiwa kuvunja ukimya dhidi ya vitendo vya kikatili ili hatua kali zichukuliwe dhidi ya wahusika. "Hata suala la ukeketaji, wanawake wamekuwa hawavunji ukimya, ndiyo maana mfumo dume unaendelea." anabainisha. Kutokana na kukithiri kwa vitendo vya ukatili kwa Wilaya za Serengeti na Tarime mkoani Mara, maadhimisho ya siku ya kupinga ukatili wa kijinsia na ukeketaji duniani yatafanyika wilayani humo kitaifa Februari 6, lengo likiwa ni kuwezesha jamii kutambua na kubadilika. Wakati huo huo mtuhumiwa aliyefanya ukatili huo anatarajiwa kufikishwa mahakamani wakati wowote ili kujibu tuhuma zinazomkabili. Habari zilizotufikia zinadai kuwa Sarah amepelekwa Nchini Kenya kwa ajili ya matibabu zaidi baada ya ndugu zake kubaini kuwa huenda akapata madhara makubwa zaidi. Habari zaidi zilibaini kuwa kuna uwezekano wa Sarah kukatwa mguu mmoja baada ya kuonekana kujeruhiwa vibaya. |
No comments:
Post a Comment