Friday, January 14, 2011

NA KWELI HII TABIA IMEENEA SANAA APA MJINI...SEHEMU kubwa ya wananchi wanaojenga nyumba hususan mijini, Dar es Salaam ikiongoza, wamekuwa na tabia ya moja inayoshangaza. Wanafunga mlango mkuu wa kuingilia na kutumia zaidi ule wa kuingilia jikoni kwa matumizi yote.

Hili ni jambo ambalo baadhi ya wadadisi wamekuwa wakihoji kulikoni? Kila aliyehojiwa kila amekuwa na maelezo tofauti.

Juma Khamisi (44) na familia yake wanaishi Mbagala Kizuiani, Dar es Salaam licha ya kwamba sehemu ya mbele ya nyumba yake imekamilika tofauti na ile ya upande wa jiko, mlango huo wa jikoni ndiyo anaoutumia.

“Sababu kubwa inayonifanya nitumie mlango wa nyuma ni kuepuka vurugu za watoto wa jirani kuingia ndani kwangu. Lakini pia nikiruhusu mlango wa mbele uwe unatumika, itakuwa ni rahisi hata majirani kuingia ovyo ndani na siku hizi unajua bwana ni vigumu kujua nani mwenye nia nzuri au mbaya. Wengine wanakuja tu kuangalia kuna nini ili baadaye waje kuchukua.”

Anasema mbali ya sababu hizo, kwa kutumia mlango huo wa jikoni unawafanya watu wasiokuwa na nia ya dhati ya kuingia ndani kuishia nje kwani kuna mlolongo mrefu hadi kufika sebuleni.

“Ukitumia mlango wa jikoni kuna-process (hatua) nyingi, kwanza utaona usumbufu wa kupishana pishana na watu wakiwa wanapika, kwa hiyo wakati mwingine utaona bora uishie nje tu usaidiwe shida yako,” anasema.

Anaeleza pia kuwa, mlango wa mbele wa nyumba yake unahitaji nguvu nyingi kuufungua kwani mingi inafungwa kwa kutumia vifaa vingi kulinda usalama wake hali ambayo inawawia vigumu mkewe na watoto wake.

Anasema kuwa mlango huo mbele una mageti mawili ya chuma pamoja na milango miwili ya mbao ambayo yote ni mizito, hivyo inahitajika mtu mwenye nguvu kuifungua jambo ambalo linawatia uvivu mkewe na watoto wake kufungua kila siku.

Kwa upande wake, Tina Mushi (35), mkazi wa Kimara, Dar es Salaam anasema analazimika kutumia mlango wa jikoni kwa kuwa muda mwingi anakuwa sehemu hiyo.

“Mimi muda mwingi nikiwa nyumbani nakaa jikoni, kwa hiyo nalazimika kutumia mlango wa jikoni na kufunga ule wa mbele,” anasema.

Hata hivyo, anasema sababu nyingine inayomfanya atumie mlango huo ni kutokana na udogo wa sebule yake ambao humfanya wakati mwingine kulazima kuweka kiti kwenye mlango huo na hivyo inakuwa si rahisi kuufungua.

“Lakini pia kiusalama siyo vizuri sana kupenda kufungua mlango wa mbele. Kuufunga kunasaidia watu wasizoee kuingia wanavyotaka hata mwizi akija nyumbani kwako kuiba kama hatakuwa mtu anayekufahamu basi huyo mwizi atakuwa ameelezwa jinsi ramani ya nyumba yako ilivyo na mtu anayekufahamu vyema,” anasema.

Anasema licha ya mlango wa sebuleni kuwepo usawa wa lango la nje la kuingilia, lakini kuna varanda iliyopo jikoni ambako hupendelea zaidi kukaa hivyo wageni wakija inakuwa rahisi kwake kukaa nao badala ya kuwakaribisha sebuleni.

Mushi anasema sababu nyingine ya kutumia zaidi varanda badala ya sebule ni kutokana na kukithiri kwa vitendo vya ujambazi katika maeneo mengi ya Dar es Salaam.

Hata hivyo anasema, wageni ambao ni ndugu zake au wale anaowaamini na kuwaheshimu, baadhi yao hupata fursa ya kufika katika sebule yake.

Naye John Mollel, mkazi wa Mbezi Beach, Dar es Salaam anasema licha ya nyumba yake kukamilika, hatumii kabisa mlango wa kuingilia sebuleni labda itokee dharura.

Anasema sababu kubwa ni mazoea au kupendelea kwao kukaa kwenye varanda ya jikoni... “Hata wageni niliowazoea wakija huwa wanatumia mlango wa jikoni kuingia ndani, lakini wengine kama vile baba, wakwe zangu, au hata wengine tu ambao hawajazoeleka sana pale nyumbani, wakija hata kama watakuwa uani watarudishwa wakatumie mlango wa sebuleni kuingia ndani.”

Lakini kwa Aminieli Kisali (36) wa Tabata sababu kubwa ya kutumia mlango wa jikoni ni kwa kuwa ule wa sebuleni unaangaliana moja kwa moja na barabara.

Kutokana na hali hiyo, anasema endapo mlango huo ukitumika, kuna wakati unaweza ukisahaulika kufungwa na hivyo kuwafanya wapitanjia kuona moja kwa moja kila kitu kilichopo ndani na hiyo ni hatari kwa usalama wake.

“Kutokana na eneo la kiwanja changu, ilikuwa lazima mlango wa mbele ukae eneo la barabarani,” anasema Kisali na kuongeza: “Kwa kawaida watoto wakifungua milango mara nyingi huiacha wazi, sasa pale kwangu kama mlango ukiachwa wazi watu wanapita barabarani wataona kila kilichopo ndani jambo ambalo ni hatari kwani siyo kila mmoja ataishia kuangalia na kupita zake."

"Kwa hiyo mimi kuutumia mlango mkubwa labda nijenge ukuta mrefu kuliko nyumba ndipo nitaweza kuutumia bila shaka.”

No comments:

Website counter